24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

SHERIA MPYA KUVIBANA VYAMA VYA SIASA

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

SERIKALI inatarajia kutunga sheria mpya ya vyama vya siasa ili kukidhi mahitaji ya hali iliyopo sasa ya demokrasia ya vyama vingi.

Kutokana na hali hiyo, vyama vya siasa vimetakiwa kuwasilisha maoni yao ndani ya wiki mbili kuanzia sasa ili kuhakikisha mchakato wa kutungwa kwa sheria hiyo unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema sheria iliyopo ina mapungufu mengi yanayoifanya ishindwe kukidhi mahitaji na hali iliyopo sasa ya demokrasia ya vyama vingi.

Alisema lengo la kutungwa sheria mpya ni kuboresha masuala ya usajili wa vyama vya siasa, uratibu wa shughuli za vyama vya siasa na mapato na matumizi ya vyama vya siasa.

“Mapungufu ya sheria ya sasa yapo mengi siwezi kuanza kuyaorodhesha na mchakato wa kuyapitia ulianza muda mrefu.

“Mchakato ulianza tangu mwaka 2013 na ulikwama kutokana na mchakato wa kutungwa kwa katiba mpya na uchaguzi mkuu wa 2015.

“Tulivishirikisha vyama wakaleta maoni, tukakaa nao mara mbili kwenye Baraza la Vyama vya Siasa na tukawa na mkutano wa wadau. Yale maoni ndiyo yametupelekea sisi kupendekeza kwamba itungwe sheria mpya ya vyama vya siasa,” alisema Nyahoza.

Alisema wazo la kutungwa kwa sheria mpya linalotokana na maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya sasa yaliyowasilishwa na wadau kuwa mengi na kwamba endapo sheria itarekebishwa bila kuandikwa upya marekebisho yatakuwa mengi kuliko sheria ya sasa.

Kuhusu kuwapo kwa mitazamo kwamba sheria hiyo inalenga kubana upinzani, alisema hizo ni hisia ambazo hazina msingi wowote.

“Si sahihi kuwa na hisia hizo kwa sababu sisi hatulengi chama chochote, tunataka tuboreshe jinsi ya kuratibu ule mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

“Kwanini wawe na hisia, kitu chochote kinachobadilika kinataka kuwabana wao, kwa nini wasifikirie kwamba kinataka kuwasaidia au kusaidia demokrasia ya vyama vingi, na wao watoe maoni yao na tunakaribisha hata waandishi wa habari walete,” alisema.

Alivitaka vyama vya siasa kuwasilisha maoni kwa kuainisha mambo ambayo wanataka sheria mpya iyazungumzie ili kusaidia kutunga sheria nzuri ambayo itakidhi mahitaji ya sasa na baadaye.

 VYAMA VYA SIASA

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema sheria mpya inalenga kumpa nguvu msajili wa vyama vya siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo.

“Nimeiona barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuvitaka vyama vya siasa vitoe maoni kuhusu utungwaji wa sheria mpya ya vyama vya siasa. Nilijua kwamba jambo hili lingefuata.

“Mahakama Kuu imewahi kutamka bayana katika maamuzi mbalimbali kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa kwa njia yoyote ile. Tusubiri wapitishe uone vyama vitakavyoporwa uhuru wa ndani,” alisema Mtatiro.

 ADC

Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hassan Doyo, alisema hawaoni kama kutakuwa na jambo jipya litakalosaidia kuboresha masuala ya siasa nchini.

“Barua tumeletewa na tutapeleka maoni yetu ingawa hatutarajii kama kutakuwa na jambo jipya. Kwanza ofisi yenyewe ya msajili ina mapungufu mengi ya watumishi na wataalamu wa masuala ya kisiasa,” alisema Doyo.

 ACT – WAZALENDO

Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema: “Tumepokea barua ya kututaka kutoa maoni kuhusu sheria mpya ya vyama vya siasa.”

 SHERIA YENYEWE

Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inaelekeza taratibu, vigezo na masharti yote yanayohusu kusajili vyama pamoja na mambo mengine yanayoendana na hayo.

Hata hivyo kumekuwapo na malalamiko ya ukiukwaji wa sheria hiyo kutoka kwa wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nafikiri siyo sahihi kwa msajili kuingilia maamuzi ya vikao vya vyama ambavyo vinazingatia katiba zake ambazo zinatambuliwa kisheria. Ni wajibu wa serikali kuheshimu misingi ya demokrasia na katiba ya nchi. Nafikiri lililokuwa muhimu kwa sasa kabla ya uchaguzi ni kuweka kwenye katiba haki ya kuwa na tume huru; haki ya kuhoji matokeo ya raisi kama ilivyo kenya endapo kuna upande haujaridhika ili kukidhi misingi ya demokrasia. Ni wakati muafaka sasa spika apotoka kwenye chama tawala makamu wake atoke kwenye chama kikuu cha upinzani kama ilivyo katka bunge la marekani. Hivi karibuni kimekuwa na malumbano mengi yanayohusu uongozi wa bunge. Nadhani hili linaweza kusaidia katika kidumisha dokrasia katika bunge.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles