Na SAMWEL MWANGA,
WAKULIMA wa pamba nchini hususan wa Kanda ya Ziwa huenda wakaondokana na adha ya kupatikana kwa madawa mahususi ya kuua wadudu wanaoshambulia zao hilo baada ya kugundulika kwa mmea wa mwarobaini kuwa mbadala wa dawa nyingine.
Awali wakulima wa pamba nchini walikuwa wameshindwa kupata suluhisho la madawa ya kuua wadudu ambayo yalikuwa yakisambazwa.
Madawa hayo yamekuwa yakibainika kutokuwa na uwezo wa kuua wadudu hali iliyosababisha wakulima wengi kukata tamaa na zao hilo.
Meneja wa Kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Alliance wilayani Bariadi, Boaz Ogola, alisema kwa sasa mmea huo utakuwa ni suluhisho kwa wakulima ikizingatiwa hauna athari zozote kwa mimea na binadamu.
Alisema dawa hiyo haina gharama yoyote kwa mkulima na hutengenezwa kwa kutwanga majani ya mwarobaini kwa
kuyaloweka kwenye maji na kuyachuja kuondoa mabaki ya majanikabla ya kupulizia zao hilo.
“Tanzania ni nchi ya kwanza kwa kuwa na pamba ya asili na kwa sasa pamba hii ina soko kubwa.
Lakini pia mkoa unajiandaa kuzalisha bidhaa za pamba ambazo zinahitaji pamba yetu.
“Sisi kama wazalishaji tumeanza kuzalisha pamba ya asili kwa kuwapa elimu wakulima kutumia dawa za asili kunyunyuzia kuua wadudu,”alisema.
Alisema pia kuwa tatizo la kutokuota kwa mbegu lililokuwapo misimu iliyopita limeonekana kutoweka mmsimu huu kutokana na wakulima kuuza pamba ambayo haikuwekewa maji na mchanga wakati wa msimu uliopita.