27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanza yasuasua uandikishaji watoto walio na umri chini ya miaka mitano

Na Clara Matimo, Mwanza

Ingawa Mkoa  wa Mwanza ni wa pili kuanza kutekeleza mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano tangu mwaka 2015  kwa ajili ya kupatiwa vyeti vya kuzaliwa takwimu zinaonyesha ni asilimia 29.4 tu ndiyo waliosajiliwa.

Hayo yamebainishwa jijini hapa leo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini(RITA), Emmy Hudson, wakati akizungumza kwenye kikao cha tathmini na hamasa  kilichokutanisha viongozi wa wilaya na Mkoa wa Mwanza lengo likiwa ni kuweka mfumo thabiti na makini  wa usajili unaohakikisha kila tukio la kizazi linaandikishwa mahali lilipotokea kwa wakati.

Emmy amesema mkoa wa Mbeya ndiyo ulioanza kutekeleza mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka  mitano mwaka 2013 lengo likiwa ni kufikia asilimia 55  hadi sasa umefikia asilimia 76.1 ukilinganishwa  na Mwanza ulioanza  mwaka 2015 wenye asilimia 29.4, Mkoa wa Pwani unaongoza kwa asilimia 116.3 ingawa ulianza kutekeleza mpango huo mwaka 2019.

“Matokeo haya ambayo hayaridhishi katika Mkoa wa Mwanza  yametokana na sababu mbalimbali ikiwemo usajili kufanyika katika vituo vya tiba tu tofauti na mikoa mingine ambapo ofisi za watendaji wa kata hutoa huduma hiyo maana kuna watoto wanaozaliwa majumbani, kukosekana kwa elimu na hamasa endelevu kwa wananchi, ukosefu wa vitendea kazi na kukosekana kwa mtandao wa simu ambao tunautumia katika baadhi ya maeneo hivyo kuathiri zoezi la kutuma taarifa.

“Sababu nyingine ni elimu potofu kwa wazazi na walezi kuhusu  uhalali wa cheti cha kuzaliwa wengi wakiamini cheti hicho ni cha muda na mtoto akivuka miaka mitano hakitumii tena, kuhama katika maeneo yao ya kazi kwa baadhi ya wasajili wasaidizi na kutokuwepo mfumo mahsusi wa kukabidhi majukumu kwa anayeachiwa ofisi, kufa au kustaafu kazi,”alieleza Emmy.

Naye Kaimu Meneja wa Usajili, Rita, Patricia Mpuya, alisema mpango wa usajili  wa watoto chini ya umri wa miaka mitano ulianza kutekelezwa mwaka 2013 hadi sasa unaendelea katika mikoa 20 ya Tanzania Bara na zaidi ya watoto 5, 962,354 wamesajiliwa pia wameishapatiwa vyeti ya kuzaliwa.

“Idadi  hiyo imewezesha kuongezeka kiwango cha watoto waliosajiliwa kutoka asilimia 13 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 55 mwaka 2020,  tumeandaa program ya maboresho katika mkoa wa Mwanza ili kutatua changamoto zilizokuwepo tunahitaji kiwango cha usajili kipande, tutahakikisha kila tukio la kizazi linasajiliwa muda mfupi baada ya kutokea na kumbukumbu zake zinahifadhiwa ipasavyo, tunaomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi zote.

Rita tunaamini tukishirikiana kikamilifu tutafanikiwa, maana serikali imelipia gharama za cheti hicho na  huduma hiyo imesogezwa karibu na wananchi  sasa wataipata kuanzia ngazi ya kata na tutaendelea kutoa elimu kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara ya viongozi katika maeneo yao, kutuma ujumbe katika simu na matangazo kwa njia ya magari katika kila halmashauri na vifaa vinapatikana kwa urahisi”alisema Patricia.

Aliwataka wazazi na walezi kutambua umuhimu wa cheti hicho kwani ni utambulisho wa awali kisheria utakaomuwezesha mtoto kupata haki nyingine, kupata nafasi za masomo katika elimu ya msingi na sekondari, kuzuia ajira ya watoto na kuwalinda katika masuala ya kisheria.

Pia kinamuwezesha mtoto  kupata nafasi za masomo na mikopo katika vyuo vya elimu ya juu, ni nyaraka ya lazima ili kupata ajira, kinamuwezesha kupata huduma za matibabu kupitia Bima ya Afya ni kiambatisho cha msingi ili kupata nyaraka nyingine za utambulisho kama kitambulisho cha Taifa, pasi ya kusafiria na kitambulisho cha kupiga kura.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Luhumbi, akizungumza wakati akifunga kikao hicho  amesema wataanzisha kampeni maalumu ya kuhakikisha usajili katika mkoa huo unapanda kutoka asilimia 29.4 hadi 100 ndani ya miezi mitatu kwa kutoa elimu kwa wananchi na watendaji wote kuanzia ngazi ya kata kuhusu umuhimu wa cheti hicho cha  mtoto  ili kufikia lengo la Serikali.

“Tuwe na vikao vya kujipima utekelezaji wetu kila baada ya miezi mitatu, tutajifunza mbinu walizozitumia wenzetu waliofanikiwa  katika zoezi hili kwa kubadilishana uzoefu  sio vibaya  tukijifunza kwa walioshinda, kuna  tabia ya kukaa vikao visivyo na muendelezo wa maazimio  vikao vya aina hiyo katika mkoa huu havina nafasi.

“Maazimio yote ya leo tutayafanyia kazi ili kutatua changamoto hii,  viongozi tunahamishwa maeneo yetu ya kazi lakini tuweke msingi mzuri ili atakayekuja anakuta utaratibu wa vikao vya utekelezaji upo naamini na yeye atauendeleza,”alisema Mhandisi Gabrieli.   

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles