24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Baba wa kambo amtaka mtoto ajichagulie aina ya kifo

Na Nyemo Malecela, Kagera

Wakati Juni 16, mwaka huu Tanzania ikiungana na Mataifa mengine kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika, huko Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Mtoto Yusuphu Muganyizi Hashimu (14) amesimulia jinsi alivyonusurika kifo baada ya baba yake wa kambo kumtaka achague atakufa kwa kifo kipi kati ya kukatwa mapanga, kuchomwa kisu au kumeza betrii la saa.

Yusuph ambaye alikuwa akiishi na mama yake mdogo ameiambia Mtanzaia Digital kuwa alikutwa na mkasa huo baada ya kwenda kumtembelea mama yake mzazi ambaye alikuwa akiishi na baba wa kambo mitaa ya Kachuko Manispaa ya Bukoba na alipofika nyumbani hapo hakumkuta mama yake.

“Sikujua kama mama na baba yangu wa kambo wameshatengana hivyo niliendelea kukaa pale nyumbani hadi usiku ambapo baba wa kambo alinishika na kunifunga kamba mikono, miguu na kuniziba na kitambaa mdomini, aliniambia nisali sala yangu ya mwisho na nichague nitakufa kifo kipi kati panga, kisu au kumeza betri la saa.

“Kwa jinsi nilivyokuwa nimefungwa niliona hatanii, hivyo nilichagua aniue kwa kumeza betrii la saa ambapo alinifungua kitambaa na kunimezesha betrii hilo kwa nguvu, baada ya dakika chache nilihisi tumbo limevurugika.

“Alinibeba na kunipeleka kwenye jumba ambalo lilikuwa linajengwa mbali na nyumbani na nilivyoona anaendelea kunilinda nilijifanya nimepitiwa na usingizi jambo lililosababisha aondoke na kuniacha peke yangu,” amesimulia Hashimu.

Yusuph amesema kuwa baada ya kuona baba yake wa kambo ameondoka alijiburuza na kwenda kujisalimisha kwa jirani ambaye naye alianza kumshangaa kwa jinsi alivyokuwa amefungwa akidhani kuwa amefanya uhalifu na kuadhibiwa.

“Nililala kwa jirani huyo ambaye ndiye aliyeniambia kuwa mama alikuwa ametengana na baba yangu wa kambo na kunisaidia kumtafuta mama kwa ajili ya kumpa taarifa zangu za kunusurika kifo.

“Chakushangaza mama alipofika nilijikuta nashindwa kuongea naye kutokana na hasira baada ya kuniambia baba yangu mzazi yupo kijijini, jambo ambalo hakuwahi kuniambia na nilipomnyamazia akaniambia nina kibuli ndio maana baba wa kambo ambaye siku zote nilijua ni baba yangu mzazi alinifanyia ukatili huo,” ameeleza Yusuph.

Amesema licha ya kufanyiwa ukatili huo bado mama yake alimuambia aendelee kuishi nyumbani hapo licha ya mama yake huyo kuwa mlevi wa kupindukia hadi kufikia hatua ya kulala kwenye vilabu vya pombe, kwa madai kuwa atamfuata baadae ili wakaishi wote kijijini.

Jambo ambalo lilimlazimu kuanza kuishi mtaani na baadaye akaenda kuomba hifadhi katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Tumaini kilichopo Kasarani Manispaa ya Bukoba ambao walimpokea na kumlea kisha kumpeleka shule kwani kwa sasa mama yake ameshafariki.

Katibu Tawala wilaya ya Bukoba, Kadole Kilugala, amesema ili kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto, Halmashauri zinatakiwa kuwashirikisha wazazi na wananchi wa kawaida katika matukio yanayowahusisha watoto ili waweze kujifunza madhara yanayowapata watoto na kupunguza vitendo hivyo kwenye jamii.

“Mfano ni siku ya Mtoto wa Afrika, katika mahadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa ‘Mayunga’ walihudhuria watoto kwa kiwango kikubwa wakati watu wazima wakiendelea na shughuli zao mtaani, jambo ambalo haliwezi kusaidia kubadilisha mtazamo wa jamii wa kukomesha ukatili kwa watoto kwa kuwa hawakushiriki kusikiliza changamoto wanazokutana nazo watoto pamoja na ushuhuda wao,” amesema Kadole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles