*Kiongozi mbio za Mwenge aumwagia sifa
Na Clara Matimo, Mwanza
Mkoa wa Mwanza umekuwa wa kwanza kupata hati safi (clean sheet) kati ya mikoa 18 ambayo imepitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 kutokana na ubora wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
Hayo yamebainishwa leo Julai 20, 2022 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Geraruma, wakati akizungumza kwenye makabidhiano ya Mwenge huo kutoka Mkoa wa Mwanza kwenda mkoani Geita yaliyofanyika katika uwanja wa Sabasaba uliopo Kata ya Kasamwa Halmashauri ya Mji wa Geita.
Kwa mujibu wa Geraruma, tangu wameanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru Aprili 4, mwaka huu mkoani Njombe wamepita Mikoa 18 na halmashauri 109 lakini hakuna mkoa ambao umesimamia vizuri miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika halmashauri zake kama Mkoa wa Mwanza.
“Tangu tumeanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru hadi leo hakuna mkoa ambao umepita salama isipokuwa Mkoa wa Mwanza hakika ni mkoa wa kuigwa nawapongeza sana viongozi wa mkoa mkiongozwa na Mhandis Robert Gabriel kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo kwani ina ubora unaoridhisha na thamani halisi ya fedha inaonekanana.
“Kwa sababu Geita walikuwa ni watoto wa Mkoa wa Mwanza taafrifa zao tunazo na tunajua na ndiyo jinsi ilivyo wakubali wasikubali mtoto hucopy kwa baba na siku zote tofali lazima lifanane na kibao hivyo sitegemei tofali na kibao vipishane itakuwa jambo la ajabu, nategemea Mkoa wa Geita mtakuwa kama baba yenu kwanza ukizingatie Mhandisi Gabriel aliishawahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, hapa Mwanza jitihada zake za kusimamia miradi zinaonekana na ndiyo zimeufanya mkoa kuwa wa kwanza kupata clean sheet,”ameeleza Geraruma.
Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuzingatia na kutekeleza maagizo yote yaliyoachwa na Mwenge wa uhuru kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwaelekeza wananchi umuhimu wa kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu kama Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, 2022 inavyosema ‘Sensa ni Msingi wa Mpango wa Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Malengo ya Taifa.
“Na wananchi wahamasishane wao kwa wao ili kuhakikisha wote tunashiriki katika zoezi hilo muhimu la sensa ya watu na makazi kwa mustakabali wa taifa letu ikiwa ni pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya malaria, Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, dawa za kulevya, rushwa bila kusahau uzingatiaji wa lishe bora kwa afya na uchumi imara,” amesema Geraruma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge huo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gabriel alieleza kwamba ukiwa mkoani humo utakimbizwa kilomita 785.4 katika halmashauri zote sita, utapitia miradi ya maendeleo 65 yenye thamani ya Sh bilioni 10.9 kati ya miradi hiyo 28 itakaguliwa, 21 itazinduliwa, 14 itawekewa mawe ya msingi na miwili itafunguliwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gabriel alisema waliupokea Mwenge huo Julai 12, 2022 katika kijiji cha Mwamhembo kilichopo Kata ya Malya wilayani Kwimba mkoani humo na kwamba umekimbizwa kilomita 563 eneo la nchi kavu na nautical miles 86.3 eneo la maji Ziwa Viktoria, umeifikia miradi ya maendeleo 52 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 18.7 katika Sekta za Elimu, Afya, Miundombinu na Maji, kati ya hiyo29 imezinduliwa, 15 imewekewa mawe ya msingi, mitano imekeguliwa na 3 imefunguliwa.