29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MWANO, MORANI; VIKUNDI VYA ULINZI VINAVYOCHOCHEA MIGOGORO MVOMERO

Na BETTY KANGONGA, MVOMERO


MIGOGORO ya ardhi ni kitendo cha pande mbili kutokuwa na maelewano juu ya umiliki au mipaka ya ardhi.

Wilaya ya Mvomero hasa vijiji vya Dihombo, Dihinda, Hembeti, Mkindo Bungoma na Kambala vimekuwa na mgogoro wa ardhi wa kugombea Bonde la Mgongola kwa kipindi cha miaka 20 sasa.

Mgogoro huo umesababisha athari mbalimbali ikiwamo vifo ambapo Desemba 12, mwaka 2015 mtu mmoja aliuawa katika Kijiji cha Dihinda Kata ya Kanga.

Taarifa zilizotolewa na wakazi wa Dihinda na kutangazwa katika vyombo vya habari zilionyesha kuwa zaidi ya mbuzi na kondoo 200 huko Kijiji cha Dihinda, Wilaya ya  Mvomero, mkoani Morogoro, wameuawa na walinzi wa jadi wanaojulikana kwa jina la ‘Mwanu.’

Wakazi wa Vijiji vya Dihombo, Mkindo Bungoma, Hembeti, Dihinda wanaelezea athari za vikundi vya kifugaji hasa Morani vinavyosababisha kuwapo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo hayo.

Wanaeleza athari ya uharibifu wa mali zikiwamo nyumba zaidi ya tano kuchomwa moto katika Kijiji cha Dihinda mwaka 2015 huku wakazi zaidi ya 3000 wa Kijiji cha Boga wakikimbia maeneo yao, baada ya kundi wanalodai kuwa ni Morani kuvamia na kuchoma moto nyumba za wakulima.

Wakazi wa Kijiji cha Kambala wanaeleza athari za kuwapo kwa kikundi cha wakulima kinachoitwa Mwano, kilichosababisha migogoro ya ardhi na kupoteza mifugo yao.

Wakulima nao wanaamini kuwapo kwa kundi la Mwano kumewaletea manufaa kwa kuwa limeweza kuwadhibiti wafugaji wanaoingiza ng’ombe katika mashamba yao.

Mkulima na Mkazi wa Dihombo, Amina Said anasema bila kuwapo kwa kundi hilo mazao yao yangeteketea kutokana na ng’ombe kuingizwa nyakati za usiku.

“Mwaka 2015 tulipoteza hekari 30 za mpunga ambazo zililiwa na ng’ombe, mwaka huu tumelima hekari 10 ambazo tunatarajia kuvuna magunia 80; hii ni baada ya kuweka ulinzi wa kulinda mazao yetu,” anasema.

Clemence Fabian mkulima na mkazi wa Mkindo, anashangazwa na uongozi wa serikali kupiga marufuku vikundi vya wakulima huku vile vya wafugaji ambao ni Morani wakiendelea na shughuli zao.

“Kama serikali inahitaji kuona amani katika maeneo haya, basi ni vema wenzetu wakaacha kutembea na silaha. Hii inaweza kupunguza vurugu, lakini hatua ya kuwaacha wao wajilinde hilo linaweza kuendeleza migogoro katika vijiji vyetu,” anasema.

Chang’andu Said Ngwamba mkulima na mkazi wa Mkindo Bungoma, analalamikia vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kufanywa na vikundi vya wafugaji ambao wanaingiza ng’ombe mashambani, pindi wanapokamatwa hutoa fedha kwa viongozi na kuachiwa huru.

Anasema walilazimika kuanzisha vikundi vya ulinzi kwa wakulima kutokana na kukosa imani na jeshi la polisi wilayani humo.

“Mara nyingi mkulima akiliwa mazao yake akienda kulalamika hakuna hatua zinazochukuliwa, hiyo ni kutokana na wafugaji kuwa na fedha. Hivyo basi, kuanzishwa kwa Mwanu kulikuwa na faida kwa wakulima,” anasema.

Naye Salum Ramadhan mkulima wa Mgongola na mkazi wa Mkindo, anaeleza namna alivyowakuta ng’ombe katika shamba lake Machi, mwaka huu na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ambao walimtaarifu mkuu wa kituo cha polisi Mkindo.

Anasema baada ya hapo hakuna hatua zilizochukuliwa, akalazimika kwenda shambani kwake na kuwafukuza ng’ombe hao ambao walianza kula mpunga wake.

“Matukio ya wakulima kupigwa wakiwa shambani ni ya kawaida, Aprili mwaka huu walipigwa wakulima wawili eneo la vibanda sita na kikundi cha Morani, baadae walikamatwa na kuachiwa huru,” anasema.

Elizabeth Anania, mfugaji na mkazi wa Kambala, anaeleza kuwa kikundi cha Mwano kilikuwa chanzo cha migogoro ya ardhi wilayani humo.

“Mwano anakamata ng’ombe hata kama hawajaingia katika shamba la mkulima na kuwapeleka ofisi ya kijiji, huko mfugaji anapaswa kulipa faini kwa kila ng’ombe Sh 15,000 fedha ambazo ni ngumu kuwa nazo,” anaeleza.

Anasema baadhi ya viongozi wa vijiji waligeuza wafugaji kama mradi wao, hali iliyosababisha wafugaji wabaki maskini.

Anania anasema baadhi ya wakulima walikuwa wakitumika kama chambo katika bonde hilo kutokana na viongozi wa serikali (hawataji) kulihitaji kwa manufaa yao.

Naye Shumari Sendewu mfugaji na mkazi wa Kambala anasema kikundi cha Mwano kilinufaika zaidi kutokana na wafugaji kukosa njia za kupita wakati wa kupeleka mifugo yao malishoni.

“Wakiona ng’ombe wanapita lazima kikundi hicho kikukamate na kuanza kuwapeleka wanapojua wao, hapo ndipo mapigano huanza,” anasema.

Mwajuma Mshitu, mfugaji wa Kijiji cha Kambala, anasema hakuna sababu ya kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi iwapo wakulima na wafugaji watakubali kuheshimu mipaka na kufuata utaratibu uliowekwa na uongozi wa Kambala wa kulima katika bonde la Mgongola.

Baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo ambao walishiriki kuunda kundi la Mwano, wakizungumza kwa sharti la kutotaja majina yao, wanasema kikundi hicho ni cha jadi cha wakulima wa Kabila la Kikagulu kinachohusika na ulinzi dhidi ya kikundi chochote vikiwamo vya Morani wa Kimasai, ambao huvamia mashamba na kuharibu mazao.

Wanasema Mwano walikuwa hawana uhusiano mzuri na Wamasai, Wamanga’ti na Wasukuma, sababu kubwa ikiwa ni tabia ya kuharibu mazao shambani mwao.

“Uhusiano mbaya uliokuwapo baina ya Mwano ya Morani, ulisababisha vifo vingi vya wakulima na wafugaji hasa kipindi cha mwaka 2014 yalipotokea mapigano.

“Mapigano hayo yalisababisha mifugo kuuawa, watu kupata ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali, hivyo serikali ikaamua kusitisha kuwapo kwa vikundi hivyo,” anasema mmoja wa wananchi hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

Ofisa Sera na Utetezi wa Muungano wa Vikundi vya Wakulima (MVIWATA) Morogoro, Thomas Laiser anasema migogoro ya ardhi ilikuwa sehemu ya ulaji wa baadhi ya watendaji na viongozi wa serikali.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mvomero, Julius Lukindo anasema migogoro ya wakulima na wafugaji kwa sasa imekwisha kutokana na kudhibitiwa kwa vikundi vilivyokuwa vikichochea hali hiyo.

Anakiri kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wakulima na wafugaji wakilaumu Jeshi la Polisi kupendelea.

“Polisi imekuwa ikifanya kazi katika wakati mgumu, hasa inapotokea migogoro ya ardhi. Ukiangalia katika ukamataji, mtu amepigwa halafu mkulima au mfugaji hawataki kutoa ushirikiano, sasa polisi tufanye nini?” anahoji na kuongeza:

“Haya matatizo chanzo chake ni nini? Je, ni mashamba kwenda kwa wafugaji au ni mifugo kwenda kwenye mashamba ya mkulima?”

Anasema jeshi ni lazima litapewa lawama kwa sababu haliwezi kufanya kazi kama jamii inavyotaka.

“Jamii ingekuwa inatoa ushirikiano na kusema aliyempiga mkulima ni fulani au aliyeua mifugo ni Fulani, basi tungeweza kukamata wahusika halisi lakini kwa sasa tumekomesha kabisa vikundi hivyo,” anaeleza.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Mohamed Utali anasema Mwano ilikuwa chachu ya vurugu wilayani humo.

Anasema hivi sasa mwenye mamlaka ya kufukuza ng’ombe pindi anapoingia shambani ni mtendaji wa kijiji pekee, ndiye aliyepewa mamlaka hayo.

Utali anasema uamuzi huo wa kuondoa vikundi vyote vya ulinzi vilivyoanzishwa katika maeneo hayo na kuweka jukumu la kufukuza ng’ombe kwa kiongozi wa kijiji, imesaidia kuleta amani Mvomero.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles