KIGALI, Rwanda
MWANDISHI wa habari wa kujitegemea, Phocus Ndayizera ameonyeshwa mbele ya vyombo vya habari na polisi wa upelelezi nchini hapa wiki moja baada ya kutoweka huku akidaiwa kujihususha na vitendo vya ugaidi.
Msemaji wa idara ya polisi ya upelelezi nchini hapa alisema juzi kwamba mwandishi huyo anatuhumiwa makosa ya ugaidi na alikuwa akifuatiliwa.
Mwandishi huyo ambaye amewahi kufanyia kazi vyombo vya habari mbalimbali na mara kwa mara amekuwa akiripoti pia katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi, alisema kwamba hajui kwa nini anashikiliwa.
Mwandishi wa BBC mjini hapa, Yves Bucyana, alisema Ndayizera alipoonekana mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya idara ya polisi inayohusika na upelelezi, alikuwa amefungwa pingu na hali yake ilionyesha uchovu.
Alisema, mwandishi huyo alifahamika katika vyombo vya habari mbalimbali na mara kwa mara aliifanyia kazi BBC idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi kama mwandishi wa kujitegemea.
Alisema mara ya mwisho kwa Ndayizera kuiripotia BBC ilikuwa Juni mwaka huu.
Alipotakiwa na polisi kuwambia waandishi wa habari tuhuma dhidi yake, Ndayizera alisema hana habari yoyote kuhusu mashitaka dhidi yake.
Ndayizera alisema alikamatwa katika mtaa wa Nyamirambo jijini hapa alipokwenda kumuona jamaa yake na kupelekwa sehemu isiyojulikana kabla ya kujikuta katika mahabusu ya polisi Kituo cha Remera.
Msemaji wa Idara ya Upelelezi, Modeste Mbabazi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi.
Polisi wa upelelezi wamekiri kuwa ndiyo waliokuwa wanamshikilia mwandishi huyo kwa wiki nzima.
Msemaji huyo wa Idara ya Upelelezi, Mbabazi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, walikuwa na taarifa za mipango ya watuhumiwa kuhatarisha usalama wa Rwanda.
Msemaji wa Polisi alisema walisubiri siku kadhaa kutangaza kumshikilia mwandishi huyo kwa sababu makosa ya ugaidi yanafuatiliwa kwa njia ya pekee tofauti na makosa mengine.
Haijafahamika ni lini mwandishi huyo na wengine wanaotuhumiwa watafikishwa mahakamani.