Mwanamke aliyekabiliwa na uraibu wa ngono, kujichua NASHAMI Wangara (38), maarufu kwa jina la Florence, ni mzaliwa wa magharibi mwa Kenya, ambaye ameamua kuandika kitabu kuhusu maisha yake na kukipa jina la “My Story for his Glory.” (Hadithi yangu kwa Utukufu wake).
“Nilipokuwa msichana mdogo nilikuwa mnyenyekevu na sikujua mambo mengi kuhusu maisha, lakini nilipofikisha miaka 18 mambo yalibadilika,” anasema.
Anaongeza kuwa wakati mwingine alikuwa anatoroka nyumbani na kurejea asubuhi hadi siku moja ambapo mama yake mzazi alipomwambie aamue moja kama kuendelea kuishi naye au kuondoka, ambapo msichana huyo aliamua kuondoka.
Anasema alianza uhusiano wake wa kimapenzi wa kwanza na mwanamume na hatimae akaanza kuishi naye pindi alipoondoka nyumbani kwao.
Haikuchukua muda mrefu, uhusiano hu ulianza kukumbwa changamoto, hali iliyosababisha waachane baada ya kushindwa kusuluhisha tofauti zao.
Hatua hiyo anasema ilimuathiri. ‘’Niliamua kutojiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na mtu mmoja,’’ anasema.
Akiwa na umri wa miaka 21 akaamua kuwa kila wakati atakuwa na wapenzi zaidi ya wawili ili mmoja akimuudhi awe na wengine.
Na hapo ndipo alianza kutekwa na uraibu wa ngono.
‘’Nilianza kama mchezo kwa kuwa nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume zaidi ya wawili,’’ anasema Nashami.
Anasema ilikuwa rahisi kutimiza matamanio yake kwa kuwa ni kitu alichohitaji kufanya kila wakati alipokuwa na mpenzi wake.
Kwa muda wa miaka sita, alikabiliwa na hali ya kufanya ngono kama uraibu. Ukombozi wake kwa ngono kati ya mume na mke.
Aliamua kuokoka baada ya kuvutiwa na huduma ya uimbaji na uadilifu wa watu walioimarisha imani yao kidini. Lakini kwa sababu dini ya Kikristo hairuhusu ngono nje ya ndoa, alijikuta akiingia kwenye uraibu mpya wa kupiga punyeto.
‘’Nilikuwa naweza kujipiga punyeto kama mgonjwa aliyeandikiwa dawa na daktari, asubuhi mbili jioni mbili,” anasema Nashami.
Alikuwa mmoja ya waimbaji wa kwaya kanisani na hali hiyo ilimfanya ajihisi mchafu na asiyekuwa na dhamana.
Ni tabia ambayo yeye mwenyewe hakuipenda na kila mara ilimfanya ahisi aibu wa kwa kuwa mateka kwa miaka kumi.
Anasema alibadilika baada ya kupata maombi maalum. Pia alikuwa anaandamana na watu ambao hawakumhukumu bali walimpatia mawaidha ya jinsi ya kuondokana na hali hiyo.
Anasema kuwa siyo rahisi kujiondoa katika uraibu wa ngono na punyeto, lakini inawezekana.
Kwa sasa anawahamasisha vijana kutojiingiza katika hali kama yake.
Mtazamo wa ngono na ponyeto kama uraibu kimatibabu ni upi?
Mwanasaikolojia, Cate Mathea, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Uraibu wa Ngono, anasema njia rahisi ya kugundua kuwa mtu ametekwa na uraibu huo ni kutathmini maongezi yake.
Kichochezi kikuu anasema ni mawazo ya mtu kuwa kwenye masuala ya ngono na jinsi ya kujichua.
“Kupiga punyeto sio tabia mbaya lakini mtu anapoifanya kila wakati na inapokuwa tu ndicho kitu mtu anachokifikiria kila mara kila wakati inageuka na kuwa uraibu,” anasema.
Daktari Mathea anasema punyeto hutumiwa zaidi na vijana wanapovunja ungo kama njia ya kuondoa ule msukumo wa kawaida wa mwili.
Anasema homoni aina ya estrogen huwa kwa mwili wa kila binadamu, kusaidia katika shughuli za ngono kwa watu wazima.
‘’Homoni ya estrogeni ikiwa nyingi mwilini, mtu anakuwa na hamu ya kufanya ngono kupita kiasi,’’ anasema mtaalamu huyo.
Anaongezea kuwa hali hiyo hudhibitiwa kwa dawa ambazo mtu hupewa ili kupunguza nguvu ya homoni ya estrogen mwilini.
Unawezaje kujiepusha na uraibu wa ngono?
Mwanasaikolojia Cate Mathea, anashauri watu kutotazama filamu za ngono kila wakati.
Pia anasema asilimia 80 ya watu wanaokabiliwa na uraibu wa ngono ni wale ambao walidhulumiwa kingoni wakiwa watoto wadogo.