MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, tukio hilo lilitokea jana usiku chuoni hapo.
“Mwanafunzi huyo alisikika akipiga kelele za kuomba msaada na walinzi walipokwenda eneo la tukio, walimkuta akigalagala chini.
“Walinzi walimpa huduma ya kwanza na kumkimbiza hospitalini lakini alifia njiani.
“Inavyoonekana, alipigwa na watu wasiofahamika kwa sababu katika mwili wake amekutwa na majeraha makubwa,’’alisema Kamanda Mambosasa.
Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambaye anasomea sayansi ya jamii ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Fredrick alikuwa akitoka katika matembezi yake ya kawaida.
“Ulikuwa ni utaratibu wake wa kila siku kwenda kunywa pombe kisha kuanza kuleta vurugu hapa.
“Kwa hiyo, inawezekana alipigwa na wale watu aliokuwa akinywa nao pombe,” alisema mwanafunzi huyo.