21.4 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

MWAMUZI YANGA, SIMBA AFUNGASHIWA VIRAGO

Martin Saanya
Martin Saanya

THERESIA GASPER NA ADAM MPWEPU – DAR ES SALAAM

KAMATI ya Usimamizi na Uendeshaji ya Bodi ya Ligi, imewaondoa katika ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, waamuzi Martin Saanya na Samwel Mpenzi waliochezesha mchezo namba 49 kati ya Simba na Yanga uliofanyika Oktoba Mosi, mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Simba kuwasilisha malalamiko dhidi ya waamuzi hao, wakipinga uhalali wa bao lililofungwa na mshambuliaji wa Yanga, Amisi Tambwe, ikidai kwamba kabla ya mchezaji huyo kufunga aliunawa mpira.

Mbali ya kuwaondoa kwenye ratiba ya ligi hiyo, kesi dhidi ya waamuzi hao itafikishwa Kamati ya Waamuzi kwa hatua zaidi.

Uamuzi wa kuwatosa waamuzi hao, umefanyika baada ya kamati hiyo kupitia ushahidi wa mkanda wa mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuwahoji wahusika.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema jana kuwa kamati hiyo imebaini upungufu mkubwa wa kiutendaji uliofanywa na waamuzi hao na hivyo kuitaka kamati inayowasimamia ishughulikie.

“Baada ya kamati kukaa, imebaini mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo, hivyo imeamua kuwaondoa wasichezeshe michezo ya Ligi Kuu, pia suala lao litapelekwa Kamati ya Waamuzi ili lishughulikiwe kitaalamu,” alisema Lucas.

Alisema mwamuzi mwingine aliyeondolewa kuchezesha ligi hiyo ni Rajabu Mrope, aliyechezesha mchezo namba 108 kati ya Mbeya City na Yanga kwa kosa la kushindwa kuumudu mchezo huo. Alikubali bao, akalikataa kisha akalikubali tena.

Lucas alisema kwa upande wa Ligi Daraja la kwanza, mwamuzi  Thomas Mkombozi ameondolewa kuchezesha ligi hiyo kwa kushindwa kuumudu mchezo namba 15B kati ya Coastal Union na KMC.

“Mombozi ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kutokana na kushindwa kuudhibiti mchezo na kutoshirikiana na wasaidizi wake, hakuwa makini katika maamuzi yake mengi, hatua iliyosababisha mchezo huo kumalizika kwa vurugu,” alisema Lucas.

Alisema mbali ya mwamuzi huyo, klabu ya Coastal Union nayo imepewa adhabu ya kucheza mechi mbili za nyumbani bila mashabiki na nyingine moja ya nyumbani italazimika kucheza ugenini.

“Coastal Union imepewa adhabu ya kucheza mechi mbili bila mashabiki, na mechi moja ya nyumbani itachezwa ugenini kutokana na mashabiki wao kumshambulia mwamuzi Thomas Mkombozi na kumsababishia majeraha na maumivu makali,” alisema.

Lucas alisema waamuzi wote masula yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi ili iwapangie madaraja mengine, akiwamo Ahmed Seif aliyechezesha mchezo wa African Lyon dhidi ya Mbao FC, ambaye naye ametolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu.

Wakati huo huo, Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania Bara (FRAT), leo kimepanga kutaja majina ya waamuzi waliovurunda katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles