ANDREW MSECHU -DAR ES SALAAM
WAKATI baadhi ya wadau wakipinga hatua ya Spika Job Ndugai, kumtambua Cecil Mwambe kama Mbunge wa Ndanda, mwanasiasa huyo ambaye alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM, amesema wiki ijayo ataanza rasmi kuingia bungeni.
Mei 6 Spika Ndugai alisoma bungeni barua ya Katibu Mku wa Chadema, John Mnyika, iliyokuwa ikimweleza juu ya Mwambe kujiondoa Chadema na hivyo kutaka mwanasiasa huyo asilipwe stahiki kama mbunge.
Hata hivyo Ndugai alisema barua hiyo ya Mnyika haina mashiko kwasababu hajaiambatanisha na ushahidi wa Mwambe kujiuzulu ama kuvuliwa uanachana na vikao halali vya chama hicho.
Jana Mwambe aliliambia gazeti hili kwamba hajaingia bungeni tangu alipopea majukumu hayo upya na Spika, lakini amekuwa akiendelea na shughuli za kibunge na kuweka sawa ratiba alizokuwa akiendelea nazo.
“Ni kweli sijahudhuria bungeni kwa vile vikao vya ndani, lakini ieleweke kuwa shughuli za kibunge ziko nyingi. Nilikuwa naendelea kuhudhuria vikao vya kamati na nikaomba udhuru kurejea jimboni kwa ajili ya kuweka mambo yangu sawa.
“Nilikwenda bungeni baada ya kupata wito wa Spika, nikakabidhiwa majukumu yangu rasmi. Ila baada ya pale nililazimika kuomba udhuru kwa kuwa kuna mambo yalikuwa yakiendelea jimboni hivyo nilirudi ili kuyaweka sawa.
“Kimsingi ni kwamba nilikuwa nikiendelea na shughuli za kibunge jimboni kwa sababu jimbo langu bado lipo pale pale, lakini pia kuna mambo yangu binafsi ambayo nilihitaji kuyaweka sawa.
“Mimi ni mkulima na katika kipindi chote ambacho sikuwa bungeni nilikuwa naendelea na shuguli za kilimo, kwa hiyo pia kuna ratiba zangu ambazo zilikuwa zikiendelea na ilibidi niziweke sawa kwa kuwa ilikuwa lazima katika suala la usimamizi niwepo mwenyewe, ila sasa narejea rasmi kwenye vikao vya ndani vya bunge,” alisema.
Mwambe alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya taarifa kuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Paul Revocatus Kaunda amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Spika Ndugai, yeye mwenywe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akiizungumzia hilo, Mwambe alisema bado hajapata nakala au taarifa ya wito ila yeye pia ameona taarifa hiyo ikizunguka kwenye mitandao ya kujamii hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.
“Ni kweli hata mimi nimeona taarifa kama hiyo ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii ila sijapata taarifa yoyote rasmi, hivyo siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa. Kama ni kweli nikipata nakala ya wito nitaweza kuzungumza ila kwa sasa tuendelee kusubiri,” alisema.
Katika taarifa ilyotolewa na Kituo cha Sheria na Hakiz a Binadamu (LHRC) jana, ilieleza kuwa katika kesi hiyo ya kikatiba namba 10 ya mwaka 2020, Wakili Kaunda anaiomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika ya kumtambua Mwambe kama mbunge halali, ilihali aliushautangazia umma kwamba amejivua uanachama wa chama chake cha Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ilieleza kuwa kauli hiyo ya Mwambe pia iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally Kakurwa aliyempokea rasmi Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM na Mwambe naye kumkabidhi Katibu Mkuu wake mpya kadi yake ya Chadema.
Wakili Kaunda alisema, kitendo cha Spika kumtambua Mwambe kama mbunge halali wakati alishajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama mbunge wa Jimbo la Ndanda (2015-2020), ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa kumrudisha bungeni mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe aliamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.
Taarifa hiyo ya LHRC ilieleza kwamba kesi hiyo ya kikatiba imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu litakaloongozwa na Jaji Issa Maige. Wengine ni Jaji Stephen Kirimi Magoiga na Jaji Seif Kulita.
Wakili Kaunda, katika kesi hiyo, atawakilishwa na jopo la mawakili sita litakaloongozwa na wakili mwandamizi Mpale Kaba Mpoki akisaidiwa na mawakili Daimu Halfani, Fulgence Massawe, Prisca Chogero, Stephen Msechu pamoja na Stephen Ally Mwakibolwa.