Magufuli, Kenyatta wamaliza mvutano

0
657

 FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wamewaagiza mawaziri wa uchukuzi na wakuu wa mikoa iliyopo katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo.

Ikumbukwe Tanzania na Kenya zimekuwa kwenye mvutano ambapo siku chache zilizopita umeibuka mgogoro katika vituo vya mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mikoa ya Mara, Tanga, Arusha na Kilimanjaro baada ya malori ya mizigo ya kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa madai ya madereva wanaopimwa kukutwa na corona.

Awali, Kenya ilikuwa ikiwatuhumu madereva wa malori yanayotoka Tanzani kuwa wanamaambukizi ya virusi vya corona hatua ambayo ilipekea kufunga mpaka wake, kabla ya Tanzania kujibu mapigo hayo.

Rais Magufuli akizungumza mkoani Singida jana wakati akirejea kutoka Chato mkoani Geita kuelekea jijini Dodoma, alisema Rais Kenyatta alimpigia simu juzi na jana ambapo amempa pole ya msiba wa dada yake na pia wamekubalina kuwa viongozi wa pande mbili wanapaswa kukutana na kutatua mgogoro uliopo mpakani haraka ili Watanzania na Wakenya waendelee kufanya biashara kama kawaida, na kwamba kuzuiwa kwa malori ya Tanzania yanayokwenda Kenya ama kuzuiwa kwa malori ya Kenya kuja Tanzania hakukubaliki.

“Haiwezekani madereva wetu wote wawe na corona, haiwezekani magari ya Tanzania yakwamishwe kwenda Kenya na magari ya Kenya yakwamishwe kuja Tanzania, tunataka tutumie mpaka huu kufanya biashara sisi na ndugu zetu Wakenya, tusichonganishwe na corona.

“Nimezungumza naye akanieleza na mimi nimekubaliana naye, Wakenya ni marafiki zetu kuna Wamasai Kenye kuna Wamasai Tanzania, kuna Wajaluo Kenya kuna Wajaluo Tanzania. Corona isije ikawa chanzo cha migogoro, tumekubaliana kwamba mawaziri wetu wa uchukuzi na wakuu wa mikoa ya mipakani watakutana na wenzao wa Kenya wajadili hili suala walimalize, tunahitaji biashara, Wakenya nao wanahitaji biashara huku, na hii corona isije ikawa chanzo cha mgogoro haiwezekani kila dereva anayekwenda huko awe na corona.

“Lakini najua haya yatatatuliwa vizuri, kwahiyo tumemuachia Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania na Kenya na wakuu wa mikoa wa mipakani wayamalize haya matatizo ni madogo ilikusudi Wakenya wafanyebiashara na Watanzania wafanyebiashara.

“Nilikuwa naambiwa kuwa kulikuwa na magari kule yamekwamishwa ya Wakenya, haiwezekani tukawakwamisha sababu wamekuja kufanyabiashara lakini pia magari ya Watanzania hayawezi yakakwamishwa kwenda Kenya,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha kuwa hawatatui mgogoro huo kwa jaziba badala yake waweke Utanzania na Ukenya mbele.

“Niwaombe viongozi walioko mikoa ya mipakani wasitatue matatizo yao kwa jazba, waweke Utanzania na Ukenya mbele, wazingatie uchumi wa nchi zetu, nafahamu mtu ukichokozwa umenyamaza nawewe unachokoza kidogo, lakini nawaomba na kwa vile tumezungumza vizuri na Rais Kenyatta sisi tumeyamaliza, wakae viongozi watatue hili tatizo na watu wafanyebiashara katika pande zote mbili, haiwezekani mtu anasafiri kwenda nchi jirani anaambiwa akae mpakani asubiri wakati anabidhaa, huu ni wakati wa kujenga uchumi na corona haikuanzia Afrika.

“Ilianzia huko mbali na corona iliwacoronea wengi kweli hata wale wenye uwezo, sasa tusije tukafika sisi ndani ya Jumhiya ya Afrika Mashariki tukachonganishwa tukapata kirusi cha kushindwa kufanyabiashara kwa kisingizo cha corona, hivyo niwaombe viongozi niliowataja kushughulikia jambo hili ndani ya wiki moja tunataka bidhaa za hapa ziende mpaka Kenya huo ndiyo uchumi, hivyo niwatake madereva kuendelea kuwa watulivu,” alisema rais Magufuli.

KUHUSU CORONA

Akizungumzia hali ya virusi vya corona nchini, Rais magufuli alisema janga hilo kwasasa limepungua hapa nchini huku akiwahimiza Watanzania kuendelea kuomba.

“Nilikuwa hapa nimeopewa taarifa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, (Dk. Rehema Nchimbi), tunatatizo la ugonjwa wa corona na bahati nzuri niliwaomba ndugu zangu Watanzania kuomba kwa siku tatu mfululizo na mmekuwa mkiendelea kuomba na ndugu zetu Waislamu wamekuwa wakiendelea kuomba katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ili Mungu atuondolee janga hili.

“Napenda kuwathibitishia kwamba janga hili sasa limepungua sana, limepungua sana pamoja na kwamba bado halijaisha, kwa hiyo ndugu zangu wanasingida na Watanzania tuendelee kuchukua hatua. 

“Nimeambiwa kwa taarifa zilizopo katika Mkoa wa Singida katika vituo vyetu wamebaki wagonjwa watatu na hao watatu wanaendelea vizuri bado tu hawajapimwa negative lakini wanaendelea vizuri kwa mkoa wa Singida.

“Hizi ni taarifa nzuri kwahiyo tuendelee kuomba, tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotakiwa ambazo tumekuwa tukishauriwa na wataalamu wetu, mimi nina uhakika kwa nguvu za Mwenyezi Mungu ni kwa kuchukua tahadhari hizo zote ambazo tumeambiwa ugonjwa huu wote siku moja utaisha.

“Na mimi nataka niwahakikishei ndugu zangu ziku moja ugonjwa utaisha kwasababu Mungu yuko pamoja na sisi, tuisogope, tusitishane na bahati nzuri hata Singida hapa nawaona hamja ogopa sana hata waliovaa barakoa nawaona wachache hata mimi sikuvaa, hata ninyi hamkuvaa, hata Mkuu wa Mkoa hakuvaa kwasababu Mungu wetu yuko pamoja na sisi kwa hiyo endeleeni kuchukua tahadhari,” alisema Rais Magufuli.

KWANINI ALIKATAA LOCKDOWN

Alisema hakutaka kuruhusu Watanzania kukaa ndani ‘lockdown’ kutokana na kile alichoeleza kwamba virusi vya corona mtu akikaa ndani kinga yake ya kupambana na magonjw ainapotea.

“Lakini cha pili tumeambiwa ugonjwa huu ukijifungia kinga yako ya kupambana na magonjw inapotea, kwa hiyo tunatakiwa tuwe huru na ndiyo maana sikutaka kuwafungia watu majumbani, wewe unayeuza nguo zako pale ningekufungia majumbani ungekula nini? Watu wanaohangaika kwenye mipunga wangelima nini? biashara zetu kwenye masoko wangefanyaje? ndiyo maana kwa niaba yenu nikasema Tanzania hatutafunga wanaiita kwa kisukuma ‘Lockdown’.

“Nikasema sisi tutaendelea kuchapa kazi kwasababu tunataka kwenda mbele, hizi taa zimefungwa wiki moja kwahiyo zimefungwa wakati wa corona sasa hao waliofunga hizi taa tungewafungia wangezifunga hizi taa? Ndiyo maana nawambia watu wa Singida tuchape kazi uchumi wetu ni muhimu sana kuliko vitu vingine, ninawaomba sana,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa hatua mbalimbli za maendeleo zinazoendelwa kwasasa nchini ni kutokana na kutokuruhusu wananchi kukaa ndani badala yake inatokana na uchapaji kazi huku akitangaza siku tatu za maombi kwa ajili ya corona.

“Nilipita kuwasalimu lakini nimefurahi singida inavyopendeza nikama Dar es Salaam, na ndiyo maana mnaweza mkaona mabadiliko haya, msione vyaelea vimeundw ana waundaji ni ninyi wananchi na nataka kuwaahakikishia kuwa Serikali ninayoiongoza iko pamoja na ninyi na ndiyo maana tunaendelea na miradi ya kimkakati ya nguvu.

 “Tutakuwa na siku tatu za kufunga kuanzia Ijumaa hadi Jumapili kumshukuru Mungu kwa maajabu aliyoyafanya katika taifa hili ya kutuepusha na janga la corona na nina uhakika katika siku chache zijazo corona itapotea Tanzania na itabaki kuwa ni historia, tusitishike tukubali kuishi nayo kwasababu tumeshaishinda na katika Mungu ushindi unakuwepo,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka Watanzania kuendelea kushikamana na kutokubaguana kwa itikadi za vyama huku akieleza kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa kwenye uchumi na kwamba kwasasa ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika.

Katikia hatua nyingine Rais Magufuli alitaka wakulima kutokudhulumiwa kisingizo cha AMCOS kwa kuwauzia bei ya chini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here