27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mvutano bungeni Muswada wa Habari

nape

Bakari Kimwanga na Gabriel Mushi-DODOMA

MUSWADA wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 umewasilishwa kwa mara ya pili bungeni ukiwa na mabadiliko ya baadhi ya vipengele huku Rais Dk. John Magufuli akisema ukifika mikononi mwake atausaini siku hiyo hiyo.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari Ikulu, Dar es Salaam jana tangu aapishwe Novemba 5, mwaka jana, Magufuli, alisema muswada huo ni wa siku nyingi na hata wanahabari wakiongozewa miezi mitatu mingine ya kutoa maoni bado hautakamilika.

Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Henry Muhanika, lililohusiana na muswada huo.

“Nikiletewa ofisini kwangu nitausaini siku hiyo hiyo, mbona muswada huu una mambo mazuri kwa ajili yenu (waandishi wa habari), nataka muwe wamoja, muwe na bodi kama ilivyo kwa wakandarasi, bodi hii sauti yenu.

“Tena wewe (Muhanika) ni mjanja umekwepa kutaja jina, kama kuna rushwa imefanyika kwa wabunge ili waupitishe muswada huo kuna taasisi ya kufuatilia. Haiwezekani chama kimoja kijifungie kwa mambo yao halafu aje mtu mwingine aseme hapa, kama ni hivyo angeenda kujiunga nao,” alisema Magufuli.

Muswada huo unaopingwa vikali na wadau wa habari kwa hoja kwamba ni hatari kwa tasnia nzima ya habari hapa nchini uliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, baada ya mara ya kwanza kuuwasilisha katika vikao vya Bunge vilivyofanyika Septemba, mwaka huu huku wanahabari watakaobainika kuripoti taarifa za kashfa huenda wakajikuta wakiishia jela.

Hata hivyo, Nape, alisema pamoja na hali hiyo lakini bado waandishi wa habari hawatakiwi kuwa na hofu kwa sababu Serikali itakuwa mlinzi wao namba moja.

Alisema muswada huo ulikuwa ukipigwa danadana kwa muda wa miaka 23 na sasa ni wakati muafaka kuwa na sheria itakayokuwa mwongozo kwa waandishi na wadau wa habari nchini.

Nape alisema moja ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika vipengele vya muswada huo ni kuviondolea vyombo vya habari au wamiliki wake adhabu katika baadhi ya makosa yatakayosababishwa na uzembe wa mwandishi wa habari.

“Kwa sheria hii sasa mwandishi kama mwanataaluma kamili anaweza kuwajibishwa na Bodi ya Ithibati kwa makosa ya kimaadili badala ya mtindo wa sasa wa kila kosa la mwandishi kubebwa na chombo cha habari au mmiliki.

“Vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya mwanahabari, badala yake kama kuna tuhuma kwamba chombo chochote kimetenda kosa na kuna haja ya kuzuia baadhi ya vifaa vyake kama sehemu ya vielelezo vya kesi, basi kazi hiyo ya upekuzi ifanywe na polisi kwa mujibu wa mfumo uliopo sasa wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),” alisema Nape.

Kuhusu suala la mitambo kuhusika moja kwa moja kutokana na kosa la gazeti, alisema wamelazimika kukiondoa kipengele hicho kwa sababu awali wachapashaji walikuwa wanahusishwa katika makosa yanayotokana na maudhui yaliyoandaliwa na watu wengine.

Nape alisema isipokuwa pale tu itakapobainika kuwa katika suala mahsusi mwenye mtambo analijua kuhusu maudhui yenye kasoro au alijulishwa lakini akaendelea kuchapa kazi hiyo.

Pia alisema muswada huo umegawanyika katika sehemu kuu nane huku ya kwanza ikiwa inahusu masharti ya awali ambayo ni jina la sheria, tarehe ya kuanza kutumika, matumizi na tafsiri ya misamiati na maneno yaliyotumika.

“Sehemu ya II, inahusika na Idara ya Habari kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, majukumu ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari, aina za umiliki wa vyombo vya habari, haki na wajibu kwa vyombo vya habari kutoa habari kwa umma na Serikali. Kuainisha wajibu wa vyombo vya habari binafsi kutoa habari na kulinda maadili ya kitaaluma ya vyombo vya habari na utoaji leseni kwa magazeti,” alisema Nape.

Alisema katika Sehemu ya III ya muswada huo inaainisha maadili ya kitaaluma ya vyombo vya habari na utoaji leseni kwa magazeti.

“Bodi ya Ithibati itaanisha sifa za kitaaluma na nyinginezo za mwanahabari kwa kushirikiana na wadau wenyewe wakati wa hatua ya Waziri kutunga kanuni. Kimsingi sehemu hii itataka wanahabari wenye elimu na uelewa wa kutosha kama alivyotuasa hayati Mzee Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini.

“Alisema a critical independent and investigative press is the blood of any democracy, hatuwezi kuwa na critical press bila kuwa na wanahabari wenye sifa za kitaaluma na maadili.

“Sehemu ya V inahusika na masuala ya kashfa. Jambo lolote litakalochapishwa na kutangazwa na mtu na kubabisha kuharibu sifa ya mtu au kuchafua sifa ya mtu au kuchafuliwa jina lake. Mtu huyo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria.

“Sehemu hii imeanisha utangazaji wa mambo yenye kashfa yanayoruhusiwa ikiwa mambo hayo yatatangazwa na Rais, Serikali au Bunge au jambo lolote litakalotangazwa mahakamani wakati wa kusikiliza shauri la kutangazwa kwa jambo lolote kwa mujibu wa sheria,” alisema Nape.

Licha ya kutoa ufafanuzi wa vifungu tata vilivyopo katika muswada huo, alisema katika sehemu ya VII itahusu makosa mbalimbali yanayohusu vyombo vya habari na eneo hilo litahusu utangazaji uliopigwa marufuku wa habari za kuchochea uasi, makosa ya uchochezi na utangazaji wa habari za uongo au kutia hofu jamii.

Nape aliwasilisha muswada huo huku akinukuu maandiko ya wanasiasa mbalimbali akiwamo Mahatma Gandhi wa India na Rais wa zamani wa Marekani Thomas Jefferson ili kupata uungwaji mkono wa muswada huo.

“Pale ambapo muswada huu umeweka makosa mbalimbali na adhabu kwa  wanahabari basi si kwa nia ovu ya kuzuia haki za binadamu za wanahabari bali kutekeleza matakwa haya ya sheria za kimataifa ambazo zinawapa wanahabari wajibu pia wa kulinda haki nyingine za raia na usalama wa nchi.

“Wanahabari wakisimama katika maadili yao na kutii sheria hawana sababu ya kuhofu vifungu hivi, Serikali itakuwa mlinzi wao namba moja,” alisema Nape.

MAONI YA KAMATI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, alisema walipendekeza pamoja na uvaaji wa vitambulisho ni vyema kanuni ikaeleza kuhusu mavazi ya sare kwa waandishi wa habari.

Akisoma mapendekezo hayo jana alisema mwana tasnia ya habari ni kioo cha jamii hivyo wana kila sababu ya kuonyesha mfano katika mambo mengi.

“Kuna mifano mizuri ya kuigwa kutoka kwa wanataaluma nyingine nyingi wakiwemo wanasheria, madaktari na wauguzi kwa uchache,” alisema Serukamba

Alitoa rai kwa vyombo vya habari kutoa habari kwa kuzingatia misingi bora ya taaluma hiyo huku akipendekeza kufanyika kwa marekebisho ya lugha katika baadhi ya vifungu katika muswada huo.

WAPINZANI WAUPINGA

Akisoma hotuba ya upinzani, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, alisema muswada huo hautakiwi kupitishwa na Bunge kwa sababu unakiuka Katiba ya nchi.

“Katika mapitio ya muswada hakuna kifungu chochote kinachotoa ulinzi wa waandishi wa habari. Imekuwa ni jambo la kawaida kwa wanataaluma kupewa vitisho na wakati mwingine kudhuriwa miili yao na hata kuuawa kutokana na kazi za kufichua uovu kupitia taaluma yao ya uandishi wa habari.

“Kutokana na ukweli huo Kambi ya Upinzani inapendekeza kiwepo kifungu mahsusi cha kuwalinda wanahabari dhidi ya vitendo viovu vinavyoweza kufanywa dhidi yao,” alisema Mbilinyi.

 MICHANGO YA WABUNGE

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema muswada huo unatakiwa kuangaliwa upya kwa kuwa una lengo la kuua vipaji na tasnia ya habari.

Akichangia hoja katika muswada huo Zitto aliyekuwa mchangiaji wa kwanza alisema muswada huo ulipaswa kujibu malalamiko ya sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976.

“Unapoandika sheria mpya ina maana sheria iliyopo inahitaji maboresho, haitoshelezi au haitakiwi. Ujio wa muswada huu ulitakiwa kujibu malalamiko ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976. Sheria hiyo ilitoa mamlaka kwa waziri kifungu cha 25 (i) kufungia gazeti lolote,” alisema Zitto na kuongeza:

“Tulitarajia sheria hii mpya ingekuja na ubora lakini katika kifungu cha 55 cha muswada huu kimemrudishia mamlaka waziri ya kuzuia andiko lolote hata sio gazeti tena. Muswada huu hauna ubora wowote, kuna haja ya kufanyia kazi zaidi muswada huu kwani hatuoni tofauti kubwa na sheria ya mwaka 1976.

“Sheria ya mwaka 1976 haimpi mamlaka waziri ya kuelekeza taarifa gani ya kuchapisha ila cha ajabu muswada huu unampa mamlaka habari gani ya kuchapisha katika chombo chochote.

“Nataka niwakumbushe kuwa miaka ya Mwalimu Nyerere hapakuwa na ithibati ndio maana tukampata Rais mstaafu Benjamini Mkapa, baada ya kurudi Makerere Uganda, Mwalimu Nyerere akampa uhariri wa magazeti ya Serikali. Tungekuwa na sheria hii tunayoitaka tusingekuwa na Dk. Harrison Mwakyembe mwanasheria ambaye awali alianza kwa kuwa mwandishi wa Uhuru.

“Vilevile mwaka 1996 kulipotokea ajali ya Mv Bukoba Serikali ilipata taarifa kutoka kwa machinga, Kampuni ya Habari Corporation sasa New Habari (2006) Ltd. Ilimtumia machinga huyo Mbaraka Islam katika kutoa taarifa hiyo kwa kina na baada kumwongezea elimu na kumuajiri sasa ni mwandishi bora wa habari za uchunguzi,” alisema Zitto.

Pia alisema lengo la dola ni kudhibiti uandishi wa habari hivyo utaua vipaji vya vijana.

“Nataka niwaambie uandishi wa habari ni passion, hata kama tutahitaji ithibati lakini sio kwa njia hii, tunaweza kutoa jukumu hilo kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT).  Nimesikitika kusiki Nape akisema hakuna mbunge ambaye hajajeruhiwa na vyombo vya habari, hata mimi nimejeruhiwa tena sana ila nawaomba tusitumie hasira, hata vitabu vya dini vimeandika. Hivyo muswada huu uangaliwe upya,” alisema Zitto.

Naye Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema), alisema muswada huo haukuwashirikisha wadau wakuu wa habari.

“Zile klabu za waandishi wa habari ziliomba kuongezewa muda lakini mmekataa na kutegemea wa Dar es Salaam jambo ambalo si halali.

“Nataka niwaambie Dk. Mwakyembe asingetakiwa kuchunguza kashfa ya Richmond kwa sababu uliibuliwa na gazeti la Mwananchi, pia kusingekuwa na uchunguzi wa mauaji ya wafanyabiashara watatu na yule dreva teksi kwa sababu waliyechunguza na kutoa taarifa ni wanahabari. Kiujumla vifungu hivi vinakinzana na utawala bora na hata mkataba ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo Serikali imesaini.

“Kumeibuka suala la mavazi yaani mnataka mwandishi anayekwenda kuripoti vita avae suti, au anaekwenda kuripoti masuala ya michezo au mashindano ya Miss Tanzania avae suti? Hili ni jambo wanalolifahamu ndiyo maana hawaendi Ikulu na suruali ya jinzi au bukta au hapa bungeni hawaingii kwa nguo za namna hiyo.

“Pia tunaua wachangiaji ambao ni watalaamu wa masuala mbalimbali kwa mfano uchumi na gesi, tungeweza kupata mawazo yao lakini sasa wanatakiwa kuwa na leseni ndio watoe mchango wao gazetini. Kuna suala la wawekezaji kutakiwa kumiliki asilimia 49 pekee na sio asilimia 100, kama mnataka hivyo anzisheni vyombo vyenu, kwa sababu mbona kampuni za madini na gesi zinamiliki kwa asilimia 100?,” aliuliza.

Naye Mbunge wa Babati Mjini, Paul Gekuli (Chadema), alisema muswada huo unakwenda kuzika tasnia ya habari kwa sababu vifungu vyote vina upungufu na unakwenda kinyume cha ibara ya 18 (d) ya Katiba nchi.

“Mngetakiwa kuzungumzia masuala ya maslahi na bima, lakini sasa naona mnakamilisha muvi yenu baada ya kuzuia Bunge ‘live’, kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano na sasa mnazuia wananchi kupewa taarifa kama ambavyo mnataka kuhakikisha kila kiongozi wa kundi la mtandao wa whatsapp kutakiwa kuwa na leseni.

“Muswada huu ni wa kuogopwa kwa sababu kifungu cha 7(i) kingetoa adhabu ya kutoza faini kwa TBC kwa kutangaza habari kwa ubaguzi.

“Huu muswada unalenga kufunga midomo vyombo binafsi ili tu waziri na rais wasikosolewe kwa chochote ndiyo maana hata vijana wetu sasa wakiandika chochote wanakamatwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alisema tasnia ya habari haikuwahi kulindwa, kuenziwa wala haikuwahi kuheshimiwa.

“Tunataka ipewe heshima inayostahili. Nimesikitishwa na Zitto kwa kufananisha wakati huu na ule wa miaka 1966, huu ni mwaka 2016 nataka niwaambie muswada huu una mambo mazuri kwa wanahabari na Taifa kwa ujumla,” alisema Mapunda.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM), alisema muswada huo umefanyiwa marekebisho makubwa na sasa umekaa vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles