LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema mvua inayoendelea kunyesha jijini humo imesababisha vifo vya watoto wawili.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa, alisema Mei 5 mwaka huu alasiri maeneo ya Matosa Goba Wilaya ya Kinondoni ulipatikana na mwili wa mtoto Francis Byabato baada ya kutoweka kwa siku mbili.
Kamanda Mambosasa alisema mtoto huyo alipatikana akiwa amefariki dunia ndani ya kisima cha futi 30 kilichokuwa wazi, nyumbani kwao.
“Tukio jingine ni la Mei 12 maeneo la Mongo la Ndege, ambako uliokotwa mwili wa mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne hadi mitano ambaye hajafahamika jina.
“Mwili huo ulikuwa ukielea katika Mto Msimbazi ukiwa hauna jeraha lolote, mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Mambosasa.
Alisema mvua hiyo inayoendelea kunyesha pia imesababisha uharibifu wa majengo ya Shule ya Msinge Mwale na Majani ya Chai zote za Kiwalani Wilaya ya Ilala na Shule ya Sekondari Kibasila katika Wilaya ya Temeke ambayo imejaa maji na kusababisha kusimamishwa kwa muda.
“Pia mvua hii imesababisha kufungwa baadhi ya barabara ikiwamo Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani ambayo ilifungwa tangu saa 10 alfajiri na barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni ambayo magari madogo hayaruhusiwi kupita mpaka maji yatakapopungua na kujiridhishakuwa eneo hilo ni salama.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari dhidi ya mvua inayoendelea kunyesha, sambamba na kuwa makini na watoto wenye umri mdogo. Pia tunaendela kufuatilia taarifa ya mvua inayoendelea kunyesha,” alisema Mambosasa.
Mapema jana asubuhi, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kampuni ya UDA-RT, Deus Buganywa, alitoa taarifa ya kusimamishwa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kati ya Kimara – Kivukoni, Kimara – Gerezani, Morroco – Kivukoni na Morroco – Gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, huduma hizo zilisimamishwa kuanzia saa 10: 30 alfajiri ya jana kutokana na eneo hilo la Jangwani kujaa maji.
“Huduma zinazotolewa sasa ni kati ya Kimara – Mbezi, Kimara – Magomeni Mapipa, Kimara – Morroco, Gerezani – Muhimbili, Kivukoni – Muhimbili na Gerezani – Kivukoni.
“Tunaendelea kufuatilia hali ya maji katika eneo husika, maji yakipungua huduma zitarejea katika hali ya kawaida. Tunaomba radhi kwa usumbufu unatokana na kusimamishwa safari hizo,” alisema.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la kuwapo mvua kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba kuanzia leo hadi Mei 18 mwaka huu.
Taarifa ya TMA pia metoa angalizo la kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani kwa kipindi chote cha kuanzia leo.
Jana, MTANZANIA lilishuhudia msongamano mkubwa wa magari katika barabara nyingi za kuingia na kutoka katikati ya jiji hilo, ikiwamo barabara ya Bagamoyo, kutokana na magari mengi kulazimika kutumia njia hiyo baada ya kufungwa barabara ya Morogoro.
Katika eneo la Jangwani licha ya kufungwa, wananchi wengi walionekana wakivuka kwa miguu na baadhi yao wakitumia mikokoteni maarufu, kwa jina la guta, ambayo iligeuka biashara kubwa.