29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Spika Ndugai aishangaa Serikali

  • Wabunge CCM, upinzania waja juu
  • Waziri atoa sababu kusuasua bandari Bagamoyo

ARODIA PETER-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameishangaa Serikali kusitasita kuanza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo akisema Wachina wanatushangaa kwa kuanza kujenga reli ya kisasa kabla ya bandari.

Ndugai alisema hayo jana bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akisisitiza kuwa mradi huo wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni ukombozi kwa taifa.

Katika kitabu cha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, Serikali ilitoa sababu za kusitisha mradi huo kuwa ni kutokana na wawekezaji, Kampuni ya China Merchant Holdings International Limited (CMHI) na State General Reserve Fund (SFRF) ya Serikali ya Oman kuweka masharti yasiyokuwa na masilahi kwa taifa.

“Binafsi sielewi ni nini kimekwamisha mradi huu wa Bagamoyo,  labda waziri kama atapata muda anaweza akatufafanulia vizuri, yeye yupo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuelezea jambo hili.

“Lakini niliwahi kwenda China mwaka juzi kwa jambo jingine kabisa katika Jiji la Shenzhen nikiwa na baadhi ya wabunge humu ndani, na kumbe bahati nzuri makao makuu ya wale China Merchant (China Merchant Holdings International Limited) ambao ndo walikuwa wajenge Bandari ya Bagamoyo yapo Shenzhen pale, kwa hiyo baada ya ziara yetu kwisha balozi wetu akasema ni vizuri tukawapitia hawa jamaa tukasikia wanachokisema.

“Wakatufanyia ‘presentation’ kubwa nzuri sana, ndo maana nasema sijui upande wa Serikali kuna nini, lakini ukisikiliza ile ‘presentation’ huwezi kuacha kuunga mkono ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

“Ni mradi mkubwa mno, na wale jirani zetu wanaotukabakaba pale juu sitaki kuwataja tutakuwa tumewabana vizuri, kwa kifupi Wachina walisema ‘tunawashangaeni sana Watanzania, ninyi rafiki zetu, ndugu zetu, sijui kwanini yanapofika mambo makubwa kama haya mnatia miguu, hamuamui.

“Na wakasema kwenye kampuni yao ile bodi wameshabadilika sana, waliobakia ambao ni watu wazima na wana ‘soft touch’ na Tanzania katika ile bodi yao walikuwa ni wawili tu, na wao walikuwa na kama miaka miwili wataondoka, kinakuja kizazi ambacho hakijui hii maneno, wakawa wanasema msipotumia fursa ya sisi tunaoondoka sasa hivi mkafanya maamuzi shauri yenu.

“Lakini mwisho wakasema tunakushangaeni eti mnajenga reli ya kisasa SGR, kwa maoni yao wao wanasema kama marafiki, wanasema ni kama kugeuza mkokoteni, kwa hiyo wanasema mnachofanya ni sawa na kuweka mkokoteni mbele alafu ng’ombe nyuma, kwa sababu wanasema unaanza kujenga bandari ndiyo unajenga reli, ninyi mnaanza reli kabla ya bandari.

“Wanasema kwahiyo tunawaangalieni marafiki zetu, kwakweli sijui kinachokwamisha labda kuna vitu vingine, lakini si mradi wa kuacha jamani chondechonde, na hao wafanya maamuzi wakae waamue, yaani ‘is a grand project’, bandari kubwa ya kisasa hakuna Afrika Mashariki hapa, mpaka Msumbiji huko hakuna, viwanda vingi, ni mji wa viwanda, alafu karibu hela zote wanatoa wao.

“Narudia tena sijui kilichopo serikalini, inawezekana kuna mambo ya msingi sana ya kuyatazama, lakini ni kitu ambacho ni vizuri tukakipa macho mawili, tukaacha mambo mengine yote, mradi kama huu ni uchumi mkubwa, tukafungua uchumi tukambana jirani yetu anayetukaba kila wakati,” alisema Ndugai.

KAULI YA WAZIRI

Akihitimisha mjadala wa hotuba yake, Waziri Isack Kamwelwe alisema majadiliano yanaendelea kuhusiana na mradi mpya wa Bandari ya Bagamoyo.

“Katika michango ya wabunge wamezungumzia kwa uchungu sana kuhusu utaratibu wa majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali na mwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo, nilichojifunza kutoka kwa wabunge ni kwamba Serikali ifanye haraka kuhakikisha kwamba majadiliano yanakamilika.

“Napenda kutoa taarifa kwamba majadiliano yangali yanaendelea ingawa kuna baadhi ya wabunge walisema Serikali imekataa, sina taarifa ya hilo.

“Baada ya kusitisha Bunge, nilijaribu kuwasiliana na mamlaka kuulizia kama majadilianao yamefikia ukomo, lakini ni kwamba majadiliano yanaendelea kati ya Serikali na mwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo ila yamechelewa kutokana na masharti ambayo yalionekana hayana masilahi kwa Tanzania,” alisema.

Mwishoni mwa wiki, akisoma bajeti yake Waziri Kamwelwe alisema masharti ya wawekezaji hao ndiyo yanachelewesha mazungumzo.

 “Masharti hayo ni pamoja na wawekezaji kudai kuachiwa jukumu la kupanga viwango vya tozo na kutoruhusu wawekezaji wengine katika eneo la kati ya Bagamoyo na Tanga na kuongeza kuwa majadiliano hayo yanaweza kuendelea iwapo wawekezaji watayaondoa masharti hayo,” alisema Kamwelwe. 

MICHANGO YA WABUNGE

Wakichangia mjadala wa hotuba hiyo bungeni jana, wabunge walio wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani walitaka maelezo ya kina juu ya sababu za kusitishwa  mradi huo wakidai una umuhimu kwa uchumi wa nchi.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussen Bashe (CCM) alisema uwekezaji wa kiuchumi wa Bandari ya Bagamoyo ulikuwa na uwezo wa kuingiza kwenye uchumi wa nchi Dola za Marekani milioni 10.

“Na ni vizuri Serikali inapokuja kuhitimisha bajeti yao, watueleze kinagaubaga nikwanini mradi huo unasimama,” alisema.

Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) alisema. “Bandari za Mtwara, Dar es Salaam, Bagamoyo na Mwambani kwa upande wa Tanzania itakuwa muhimu kwa kuunganisha nchi za maziwa makuu,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, aliishauri Serikali kutafuta mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kugharimia mradi huo kuliko mkopo wa hivi sasa ambao utaanza kulipwa kabla ya mradi huo kukamilika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF) alisema. “Kwanza tuondokane na dhana kwamba ni bandari, ni zaidi ya bandari, ni mji, ni ajira ni kufunguka uchumi wa Tanzania.

“Kutakuwa na viwanda zaidi ya 800, mizigo inapakiwa inakwenda kwenye meli hadi kwenye reli mpya ya SGR. Lakini pia utajengwa mji wa kisasa wa watu kuishi ambapo pia Dar es Salaam itapumua.

“Bandari hiyo ikijengwa kutakuwa na logistics za transit trade ambapo itaweza kuchukua makontena milioni 420 kwa mwaka.

“Sasa hivi bandari kubwa duniani Rotterdam inachukua milioni 11.87, kwa maana hiyo bandari ya Bagamoyo ingebakia kuwa kubwa pengine kwa miaka mamia ijayo kwa dunia nzima,” alisema.

Mbunge wa Bagamoyo, Jumanne Kawambwa (CCM) katika mchango wake alisema mradi huo unajumuisha bandari, viwanda na kituo maalum cha uwekezaji,

Alisema kazi kubwa ilikwishafanywa na viongozi na wataalamu kwa miaka iliyopita  kuanzia mwaka 2012, 2013 na 2015 ambapo jiwe la msingi la ujenzi wa bandari liliwekwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

“Ni faraja sana kupata wawekezaji hao, China na Serikali ya Oman, ni rafiki zetu tutumie fursa hizi na wamekubali kuwekeza jumla ya dola za Marekani bilioni 10 sawa na trilioni 23 za Tanzania kwa ujenzi wa bandari na viwanda, na kwa kuanzia vitajengwa viwanda vikubwa 190 na vitatoa fursa za ajira takribani 270,000,” alisema.

Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya eneo la Pwani lenye uwezo wa kujengwa bandari kubwa ya kisasa.

 “Hata China walivyotaka kuendeleza nchi yao walianzia China Mashariki wanapopakana na bahari kuanzia Djibout hadi Afrika Kusini. Tanzania tuna nafasi kubwa ya kujenga bandari itakayoweza kuhudumia meli ya kizazi cha nne itakayoleta mzigo Bagamoyo na kwenda kwenye bandari nyingine ndogo,” alisema Ghasia.

Naye Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM) yeye alizungumza kwa kifupi akimwomba Spika Ndugai aite timu ya majadiliano kwenye mradi huo kufika bungeni kueleza sababu zilizokwamisha mradi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles