27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada vyama vya siasa kiboko

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MUSWADA wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 umejadiliwa na kupitishwa na Bunge huku kambi rasmi ya upinzani ikipinga mambo 12 yaliyowasilishwa na Serikali na Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ikija na mambo saba.

Akiwasilisha muswada huo alioutaja kuwa ni kiboko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema kifungu cha 15 kinakusudia kuweka kifungu kipya cha 10B ili kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kuhakiki chama cha siasa wakati wowote.

Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha chama kinakuwa na sifa za usajili wakati wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili kuhakiki muda wowote utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kuhakikisha kila chama kinazingatia kutekeleza masharti ya msajili.

Vile vile waziri huyo alisema muswada huo unalenga  kuweka kifungu kipya cha 11C kinachoweka masharti na utaratibu wa vyama kushirikiana.

Alisema lengo ni kuhakikisha vyama vinaacha mazoea ya kufanya ushirikiano kiholela ili kuviepusha kuvunja sheria nyingine za nchi.

 “Kifungu cha 18 cha muswada huo kinarekebisha  kifungu cha 11C cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinachozuia kupeperusha bendera za vyama vya siasa katika maeneo ambayo Sheria ya Vyama vya Siasa imekataza kufanyika,” alisema.

Mhagama alisema kifungu cha 21 cha muswada huo kinakuja kuweka kifungu kipya cha 21C  cha Sheria ya Vyama vya Siasa ili kuvitaka vyama kuwasilisha kwa msajili tamko la mapato na matumizi.

Alisema lengo la marekebisho hayo ni kumwezesha msajili kujua mapato na matumizi ya chama wakati wa mchakato wa usajili ili kuhimiza suala la uwazi katika mapato na matumizi.

Pia alisema kifungu cha 22 kinarekebisha kifungu cha 13 ili vyanzo vya mapato kuwekwa wazi kwa lengo la kuratibu vyema mapato na matumizi ya vyama vya siasa.

Aidha alisema mapendekezo katika muswada huo yanavitaka vyama vya siasa kuteua ofisa masuhuli atakayesimamia mali za chama, kuwezesha kila chama kuwa na mtu atakayewajibika katika mapato na matumizi ili kukidhi matakwa ya mfumo wa uwajibikaji katika utunzaji wa mali za taasisi.

Alisema kifungu cha 23 cha muswada kinakuja kurekebisha kifungu cha 15 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kutaka kila chama kinachopata ruzuku ya Serikali kuwa na akaunti maalumu ya benki ya kuweka na kutumia fedha za ruzuku ili kuhakikiha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sheria.

“Kifungu cha 24 cha muswada kinarekebisha kifungu cha 18 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kimelenga kumpa msajili mamlaka ya kusitisha ruzuku kwa chama kilichoshindwa kusimamia matumizi ya fedha hizo ili kulinda fedha za umma zisitumike vibaya.

 “Kifungu hicho pia kinampa msajili mamlaka ya kumuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa mapato na matumizi ya chama lengo likiwa kumwezesha msajili kubaini upungufu uliopo katika mapato na matumizi ya chama cha siasa,” alisema.

Waziri huyo alieleza kuwa kifungu cha 25 cha muswada kinakusudiwa kufuta na kuweka kifungu cha 18A cha Sheria ya Vyama vya Siasa ili kuweka masharti kwamba mwaka wa fedha wa kila chama cha siasa unapaswa kuwa mwaka wa fedha wa Serikali.

 “Kifungu hicho kitakuwa kikikitaka kila chama cha siasa kuwasilisha taarifa za hesabu zake kwa CAG kwa ukaguzi kisha kuwasilisha taarifa ya hesabu zilizokaguliwa kwa msajili, lengo likiwa ni kuboresha utaratibu wa kukagua hesabu za vyama ili iendane na ratiba ya ukauzi ya CAG,” alisema.

Alisema kuwa kifungu cha 30 cha muswada kinakusudiwa kurekebisha kifungu cha 21B cha Sheria ya Vyama vya Siasa kuainisha vyanzo vya fedha za kuendesha Baraza la Vyama vya Siasa.

Aidha alibainisha kuwa kifungu cha 21E kinaweka utaratibu wa kudhibiti mwanachama wa chama cha siasa anapokiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ili kumwajibisha kwa kufanya kitendo ambacho hakistahili na kuepusha kukiadhibu chama kwa kosa ambalo anastahili kuadhibiwa mwanachama.

Alisema katika marekebisho ya kifungu cha 8D, kinaeleza lengo ni kufanya katiba za vyama vya siasa kuwa bora na kukidhi matakwa ya sheria huku kifungu cha 8E kikiweka katazo kwa chama cha siasa kuanzisha kikundi cha ulinzi na usalama au kuendesha mafunzo ya kutumia nguvu au silaha ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu yeyote yule.

Mhagama alisema lengo ni kuzuia vikundi hivyo kuingilia kazi za vyombo vya ulinzi na usalama vilivyowekwa kisheria.

MAONI YA UPINZANI

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika ofisi ya Waziri Mkuu, Ester Bulaya, alisema wanasikitika muswada huo umekuwa si rafiki kwa vyama vya siasa.

Bulaya alisema dhana kuu ya muswada huo ni kumpa msajili wa vyama vya siasa nguvu kubwa ya kuingilia uendeshaji wa vyama na hadi kuwavua uanachama wanachana na viongozi.

“Nguvu hii inapitiliza na inampa uwezo zaidi ya ule ambao katiba za vyama zinautoa kwa wanachama na viongozi wake.

“Msajili ni mlezi wa vyama, katika hilo tulitarajia angalau alete muswada ambao utaweza kutatua mizozo baina ya viongozi ndani vyama, baina ya vyama na baina ya vyama na Serikali na au Tume ya Uchaguzi.

“Mheshimiwa Spika, kuanzia mwanzo wa muswada katika vifungu vyote vinavyotoa adhabu, hakuna kifungu chochote kinachotoa haki ya kusikilizwa na haki ya kukata rufaa pale mhusika anapoona kuwa hakutendewa haki. Tukumbuke kuwa haki ya kusikilizwa na kukata rufaa ni haki ya msingi kwa mhusika,” alisema.

Bulaya alisema kifungu cha 3(c) cha muswada huo kinatoa mamlaka kwa msajili wa vyama vya siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani ya chama, jambo ambalo linapunguza uhuru wa vyama kufanya uchaguzi bila mashinikizo kutoka katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

“Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kifungu hicho kifutwe na badala yake msajili awe na jukumu la kukuza demokrasia na utawala bora ndani na miongoni mwa vyama vya siasa. Kwa maana hiyo kifungu hicho kisomeke kama ifuatavyo: ‘to promote democracy and good governance within and among political parties’,” alisema Bulaya.

ELIMU YA URAIA

Msemaji huyo wa upinzani alisema elimu ya uraia ni haki ya kila Mtanzania bila kujali kama ni mwanachama wa chama chochote cha siasa au la.

Alisema elimu hiyo hutolewa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu na kwamba kwa mantiki hiyo, hii si kazi ya msajili wa vyama vya siasa.

“Kwa kuwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais Tamisemi, hata kama muswada huu ulimaanisha elimu ya mpigakura, bado jukumu hilo lingekuwa chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na si msajili wa vyama vya siasa.

“Kifungu cha 3(g) na kikisomwa pamoja na kifungu cha 5A vyote vinazungumzia kuhusu elimu ya uraia.

“Wakati kifungu cha 3(g) kinampa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kudhibiti elimu ya uraia, kifungu cha 5A kinaweka masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia.

“Kifungu cha 5A (1) kinatoa masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia kwa kumtaka mtoaji wa elimu hiyo, iwe ni mtu yeyote au taasisi ya ndani au nje ya nchi, kutoa taarifa ndani ya kipindi cha siku 30 kwa msajili wa vyama vya siasa ikiainisha aina ya mafunzo, watakaohusika na mafunzo, zana za kufundishia pamoja na malengo yanayolengwa kufikiwa na mafunzo hayo.

“Masharti hayo hayakutilia maanani kuwa vyama vya siasa vina mahusiano ya kiitikadi na vyama rafiki toka nje ya nchi, na ni haki yao ya msingi ya kueneza itikadi za vyama vyao bila kujali mipaka ya nchi.

“Kifungu kidogo cha (2) kinaweka masharti kwamba msajili anaweza kukataa maombi ya kutoa mafunzo hayo na kutaja sababu za kukataa. Muswada huu haujaainisha popote sababu za msajili wa vyama kukataa maombi ya kutoa mafunzo hayo chini ya kifungu cha 5A(1).

“Huu ni upungufu mkubwa kwani msajili anaweza kukataa tu kutokana na matashi yake bila kuongozwa na sheria inayopendekezwa.

“Kifungu cha 5A pia kimejaa adhabu za faini na vifungo kwa atakayekiuka masharti ya kifungu hicho.

 “Yote haya tunayatafsiri kama hila mbaya ya kuvizuia hasa vyama vya upinzani kushirikiana na vyama rafiki katika kueneza itikadi zao na kupata mafunzo ya namna bora ya kuendesha siasa za kistaarabu na kushamiri.

“Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwamba kifungu chote cha 5A na vipengele vyake kifutwe,” alisema Bulaya.

MSAJILI KUWA NA MAMLAKA MAKUBWA

Mbunge huyo alisema kifungu kipya ya 5B cha muswada kinampa mamlaka makubwa msajili wa vyama kutaka taarifa yoyote kutoka kwenye chama au kiongozi wa chama.

Bulaya alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inapinga msajili kutaka taarifa yoyote kwani taarifa nyingine ni siri kwa ajili ya masilahi na ustawi wa chama.

Alisema mathalani haitakuwa afya chama cha siasa kikatakiwa kutoa taarifa ya mikakati yake ya kushinda uchaguzi na kuitoa kwa mamlaka za Serikali iliyoko madarakani. Kwahiyo, ni vema muswada huu ukaainisha aina ya taarifa zinazotakiwa kutolewa kwa msajili,” alisema.

KUKASIMU MADARAKA

Msemaji huyo alisema kifungu kipya cha 6A(3) kinaingilia utaratibu wa katiba za vyama kwa kutoa sharti kuwa Mkutano Mkuu au Kamati Kuu visikasimu madaraka yake.

“Huku ni kuingilia utaratibu wa kawaida wa vyama kwa mujibu wa katiba zao. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki hakileti afya kwa siasa za vyama vingi, hivyo kifutwe.

MWENGE WA UHURU

Aidha Bulaya alisema kifungu kipya cha 6A (5) kinachohusu ulazima wa chama cha siasa kuenzi na kudumisha uwepo wa mwenge wa uhuru hakina mantiki.

Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba kazi na madhumuni ya mwenge wa uhuru yalishakamilika, ila ni muhimu kuweka kumbukumbu hiyo katika makumbusho ya taifa na katika vitabu vya historia ila si kwenye sheria.

“Vilevile kutambua au kukumbuka mapinduzi ya Zanzibar ni jambo jema kwa kuwa ni sehemu ya historia ya nchi yetu, na vizazi vijavyo vitakuwa na haki ya kujua histora hiyo, ila Kambi Rasmi haioni mantiki ya kuweka suala hilo kwenye sheria,” alisema.

KUSAJILI CHAMA LAZIMA UWE MTANZANIA

Bulaya alisema kifungu cha 6B (a) kinaeleza kwamba ili mtu aweze kusajili chama cha siasa, ni lazima wazazi wake wote wawili wawe ni raia wa Tanzania.

Alisema kifungu hicho kinatoa taswira ya ubaguzi na kuonesha kuwa Tanzania kuna raia ambaye uraia wake ni wa juu kuliko wa mwenzake (first and second class citizen).

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaamini kuwa kama mtu ni raia wa Tanzania basi haina haja tena ya kuangalia uraia wa wazazi wake. 

“Aidha Ibara ya 13 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kuwa ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake,” alisema.

ORODHA YA WANACHAMA

Bulaya alisema kifungu cha 11 kinaanzisha vifungu vipya vya 8C, 8D na 8E. Kifungu cha 8C (1) na (2) kinatoa masharti kwamba chama cha siasa lazima kiwe na orodha halisi iliyohuishwa (the updated register) ya wanachama na viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali za chama husika.

 Alisema msajili anaweza kudai kupatiwa orodha hizo wakati wowote na taarifa zozote kuhusu rejista hizo kwa muda atakaoamua katika notisi atakayokipatia chama husika kuwasilisha taarifa hizo.

Bulaya alisema rejista ya orodha ya wanachama na viongozi wa chama ni mojawapo ya nyaraka muhimu za mikakati ya ushindi wa chama chochote cha siasa.

“Mheshimiwa Spika, jambo baya zaidi ni kwamba kushindwa kutekeleza masharti hayo chama kitapewa adhabu ya kusimama kufanya kazi za siasa.

“Pia kiongozi wa chama aliyeshindwa kuwasilisha taarifa hizo atakuwa ametenda kosa, na hivyo atakabiliwa na adhabu ya faini isiyopungua shilingi milioni 1 na isiyozidi milioni 3 na kifungo kisichozidi miezi sita au adhabu zote kwa pamoja.

“Mambo yote haya yanaonekana kuwa na hila mbaya za kufifisha na kudumaza shughuli za vyama vya siasa na kimsingi vyama vinavyolengwa na sheria hii ni vyama vya upinzani. Kwa mantiki hiyo, tunashauri kifungu hicho kifutwe,” alisema.

MSAJILI KUREKEBISHA KATIBA

Bulaya alisema kifungu kipya cha 8D(2) kinampa mamlaka msajili kuamuru chama fulani kufuta au kurekebisha kifungu cha katiba yake.

Alisema kifungu hicho kinakiuka haki za watu kujumuika na kuamua mambo yao ya ndani.

“Hii ni kwa sababu kabla chama hakijasajiliwa lazima kiwasilishe pamoja na mengine katiba yake kwa msajili. Na ukweli ni kwamba katiba za vyama zinaamuliwa na mikutano mikuu ya vyama husika na mikutano mikuu kwa vyama hukaa kila baada ya miaka mitano.

“Kwa muktadha huo, ni kwamba kifungu hiki hakitekelezeki kwa kuwa kinapoka mamlaka ya mikutano mikuu ya vyama kufanya marekebisho ya katiba zao.

“Aidha kifungu hiki kinatoa shinikizo kwa vyama kufanya marekebisho ya katiba zao hata kama marekebisho hayo hayaungwi mkono na vyama hivyo. Ikiwa kifungu hiki hakitaondolewa, basi katiba za vyama zitakuwa ni katiba za msajili/Serikali kwa kuwa zitakuwa zimetungwa kukidhi matakwa ya Serikali na sio ya vyama,” alisema.

VIKUNDI VYA ULINZI VYA VYAMA

Bulaya alisema kifungu kipya cha 8E kinazuia vyama kuwa na kikundi cha ulinzi.

Alisema kifungu hicho ni kibaya kwa sababu ulinzi ni jukumu la kila mtu kwa mujibu wa katiba.

“Kuzuia vyama visijilinde ikiwa ni pamoja na kulinda mali na viongozi wake ni kutoa nafasi kushambuliwa na watu wasiokuwa na nia njema na vyama vyetu.

“Kwa mtazamo wetu jambo hili lina nia ovu dhidi ya vyama vyetu ikiwa ni pamoja na wanachama, mali na viongozi wetu.

“Nyie ni mashahidi wa jambo hili, viongozi wetu wameshambuliwa mchana kweupe, katika chaguzi mbalimbali wanachama wameshambuliwa na wengine kuuawa na wengine hadi sasa ni vilema,” alisema.

VYAMA KUUNGANA

Mbunge huyo alisema katika kifungu cha 17, kinachoanzisha vifungu vipya vya 11A, 11B na 11C, Serikali imeleta marekebisho kwa kifungu cha 11A kwa kuingiza kifungu kipya cha 11A (6) kwamba masharti ya vyama kuungana au kushirikiana yaliyopo kwenye kifungu cha 11 A hayatakihusu chama kilichopo madarakani.

“Mapendekezo haya yanaonyesha ubaguzi wazi wa kisiasa na kudhihirisha kwamba chama tawala hapa kwetu Tanzania si miongoni mwa vyama vya siasa na kwamba sheria hii tunavitungia vyama vingine.

“Mapendekezo haya ya Serikali yanaonyesha kwamba CCM ambayo ndiyo chama tawala hapa kwetu hakifungwi na masharti ya sheria hii na kwamba hakipaswi kufuata taratibu za vyama vya siasa jambo ambao linaashiria kwamba hata kisiposhinda uchaguzi kitaendelea kung’ang’ania madaraka.

“Huu ni udikteta mkubwa ambao tunataka kuuhalalisha kisheria. Kambi ya Upinzani inayapinga kwa nguvu zote mapendekezo haya ya Serikali,” alisema.

SIASA KATIKA TAASISI ZA UMMA

Msemaji huyo alisema kifungu cha 19 cha muswada  kinachofuta kifungu cha 12(2) cha sheria na kukiandika upya, kinapiga marufuku shughuli zozote za kisiasa katika taasisi za umma, ikiwemo katika vyuo vya umma, majengo ya Serikali, sehemu za ibada na maeneo ya kazi.

“Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa msajili amesahau kuwa kuna fani inayohusiana na siasa zinafundishwa katika vyuo vya umma na tunapoelekea ili mwanafunzi aweze kuwa mzuri katika taaluma hiyo, itamlazimu kufanya mafunzo ya vitendo kwenye vyama vya siasa ili kulinganisha nadharia za darasani na uhalisia katika vyama.

“Na unatenganisha vipi wanafunzi na wakufunzi wa siasa vyuoni na siasa halisi? Wengi ni mashahidi hapa, mmetokea katika siasa za vyuoni na sasa ni viongozi wazuri na wale ambao hawakuwa wanasiasa vyuoni mnaweza kuona aina ya uongozi wao katika hali halisi ya siasa,” alisema.

RUZUKU KWA VYAMA VYA SIASA

Mbunge huyo pia aligusia kifungu cha 24 cha muswada kinachofanyia marekebisho kifungu cha 18 kwa kuongeza vifungu vidogo vya (6), (7), (8) na (9).

Alisema kifungu cha (6) kinaongozwa na hisia za msajili na hivyo kusababisha kusitisha ruzuku kwa chama cha siasa.

“Jambo hili la kutokuwa na ushahidi usiokuwa na mashaka bali hisia ni jambo la hatari sana katika nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora.

“Mheshimiwa Spika, kifungu cha 27 kinachoanzisha vifungu vipya vya 21D na 21E. Katika kifungu cha 21E kinampa msajili mamlaka ya kumfukuza mwanachama wa chama cha siasa.

“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa katiba za vyama kwa sababu msajili anakuwa juu ya katiba na vikao vya chama. Jambo hili linamfanya kuwa juu ya wanachama wakati yeye sio mwanachama wa chama husika na hivyo anakosa uhalali wa kuwa na maamuzi ya kufukuza au kusajili kiongozi wa chama husika,” alisema.

MAONI YA KAMATI YA BUNGE

Akitoa maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohamed Mchengerwa alisema licha ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho mbalimbali tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, lakini  bado kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa mfumo wa vyama vingi unafanya kazi kwa tija kwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa wananchi pamoja na kukuza demokrasia nchini.

 Mchengerwa alisema dhamana hiyo inahitaji mfumo wa sheria zinazosimamia vyama vya siasa ulio madhubuti na kwamba kwa sababu hiyo, kamati inaona kuwa muswada huo unatatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake wa sheria inayorekebishwa.

Alisema kupitishwa kwa muswada huo kutawezesha mfumo wa sheria nchini kubainisha majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambavyo ni pamoja na usajili wa vyama vya siasa, kutoa elimu ya uraia, kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi na kusimamia mienendo ya vyama vya siasa.

 Pia alisema sheria hiyo itamwezesha msajili kuzitaka taasisi zenye nia ya kutoa elimu ya uraia kimataifa na pia kumwezesha msajili kupata taarifa kutoka kwa chama chochote cha siasa na kwamba lengo la marekebisho hayo ni kumwezesha msajili kuratibu utoaji wa elimu ya uraia.

 Mchengerwa alisema marekebisho ya sheria hiyo yanayopendekezwa yataimarisha utendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuipa mamlaka zaidi ya kuratibu na kusimamia kwa ufanisi zaidi uanzishwaji na utekelezaji wa majukumu ya vyama hivyo nchini kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria nyingine za nchi.

Aidha mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kubainisha mapungufu mbalimbali katika mfumo wa kisheria nchini katika usimamizi na uratibu wa wa vyama vya siasa.

Pia kwa kuandaa marekebisho na kuyawasilisha bungeni kupitia muswada huo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria hiyo na kuimarisha misingi ya utaifa kwa vyama vyote na kwa maendeleo endelevu ya taifa kwa ujumla.

MICHANGO YA WABUNGE

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) aliwashangaa baadhi ya wanasiasa wanaoupinga muswada huo ambao una masilahi mapana kwa vyama na taifa kwa ujumla.

Alisema katika kipindi cha miaka 26 tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, Serikali imejitafakari na tafiti zimeonesha ipo haja ya kufanyia marekebisho sheria hiyo kutokana na mapungufu yaliyoonekana katika utendaji wa vyama.

 “Nchi imejitafakari na kuona katika kipindi hicho cha miaka 26 kuna mapungufu katika sheria hiyo na kuamua kuifanyia marekebisho ili vyama vijiendeshe kwa ubora zaidi na kwa kulinda demokrasia ya nchi.

Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama (CCM) alisema muswada huo unakwenda kujenga taifa lenye demokrasia, amani na utulivu huku akidai Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijauelewa.

“Inawezekana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijaulewa muswada huu na hivyo kuamua kupotosha umma kwamba muswada ni kandamizi.

“Naomba nielimishe kwamba muswada huu utaleta uwazi na uwajibikaji kwa vyama vya siasa, ambapo pamoja na mambo mengine vyama vyote vitakaguliwa na CAG ili kujua matumizi yao ya fedha ili baadhi ya watu wasitumie fedha hizo kiujanja ujanja kwa masilahi yao badala ya kuwasaidia wananchi,” alisema Mhagama.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijawahi kupinga kukaguliwa na CAG huku akidai kuwa wao ndio walitoa hoja mwaka 2009 kupitia Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma mjini – ACT Wazalendo) wakati huo akiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, kwamba vyama vikaguliwe.

Alisema CCM isijidanganye kuvitungia vyama vingi muswada wakati chenyewe hakijui kitakuwa wapi katika chaguzi zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles