23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awaonya Ma-DC wanaoweka watu ndani ovyo

ANDREW MSECHU-Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli ametoa onyo kwa wakuu wa wilaya (ma-DC) wanaoamuru watu kuwekwa ovyo ndani kwa saa 24, kwani wamekuwa wakiwaumiza wananchi bila sababu za msingi.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani, Rais Magufuli alisema ameamua kueleza hilo wazi kwa kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikilalamikiwa na watu wengi lakini havikomi.

Mbali na majaji, pia wakuu wa wilaya wawili na wakurugenzi 10 wapya wa halmashauri walikula kiapo cha uadilifu Ikulu Dar es Salaam jana.

 “Kwa wakuu wa wilaya, msizitumie vibaya sheria na mamlaka mlizopewa. Kuna hili mnamweka mtu ndani saa 24 halafu baadaye mnamtoa eti mnasema atakuwa amejifunza, na hata mahakamani hamumpeleki, ‘its not fare’ (si sahihi).

“Je mkuu wa mkoa naye akiamua kufanya hivyo kuwaweka watu ndani hovyo na kila mwenye mamlaka kama hiyo akiwa anafanya atakavyo si itakuwa vurugu! Kuna mambo mengine mnatakiwa mjipe nafasi ya kushauri na kuelekeza pale mnapoona watu wanakwenda isivyo,” alisema.

Alisema wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wanatakiwa kuhakikisha wanapambana kwa ajili ya kukusanya mapato ya Serikali ili kusaidia shughuli za maendeleo na si kuwindana na kutafutana katika utendaji wao.

“Nchi inahitaji kwenda mbele, siwezi kuvumilia kusikia malumbano ya wakurugenzi na wakuu wa wilaya. Nimesikia pia baadhi ya watendaji wa halmashauri na wakuu wa wilaya ambao wanalumbana na nimewaweka kiporo,” alisema.

Kauli ya Rais Magufuli inakuja wakati akiwa ametengua wakuu wa Wilaya ya Mwanga na Tarime ambao walilalamikiwa sana kwa kuweka watu ndani ovyo.

Akielezea hatua ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho, alisema amefanya hivyo kutokana na sababu ambazo kila mtu amezisikia kuhusu mvutano wake na mkurugenzi wake.

“Kwa Wilaya ya Mwanga kila mtu amesikia, kuna wakati DAS aliwekwa ndani, vurugu zote zinaanzia na yeye (mkuu wa wilaya), lakini yeye amesomea wadudu pengine na watu wote anawaona wadudu.

“Nikaona nimtoe aende kwenye sekta ya wadudu akafanye vizuri huko. Wakuu wa wilaya mna sheria na mamlaka mnazitumia vibaya. Sheria ya kuwaweka watu ndani msiitumie vibaya,” alisema.

Alisema kwa Tarime kuna changamoto nyingi, kwahiyo ameamua kumpeleka aliyekuwa kiongozi wa mbio za Mwenge ambaye aliwahi kumuona namna alivyokuwa akigomea kuzindua miradi iliyokuwa haieleweki, ili aende akawagomee na watu wa Tarime.

Katika uteuzi wake huo, Rais Magufuli pia alimteua aliyekuwa kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka 2018, Charles Kabeho kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime kuchukua nafasi ya Glorias Luoga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa huku nafasi ya Mbogho aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga ikichukuliwa na Thomas Apson.

UTEUZI WA MAJAJI

Akizungumzia uteuzi wa majaji, Rais Magufuli alisema alikutana na wakati mgumu wakati wa mchujo wa majina, ambapo alilazimika kutopitisha jina la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) ambaye alikuwa katika orodha, kutokana na majukumu makubwa aliyonayo, hasa ya kuwafikisha mahakamani mafisadi.

Alimtaja mwingine, John Kayoba ambaye japokuwa amesimamia kufanya mabadiliko mengi kwenye sekta ya mahakama na anaifahamu vyema, lakini alisita kumteua mwaka jana na mwaka huu amempitisha kuwa jaji.

Alisema ameamua kuteua majaji vijana akiwemo Upendo Madeha aliyekuwa Mahakama ya Shinyanga kutokana na ujasiri aliouonesha alipowaweka ndani watuhumiwa wa uchakachuaji sukari ambao ni wafanyabiashara wakubwa na alikabiliana na vishawishi na kusimamia haki.

“Majaji wana nafasi kubwa, hivyo wanapaswa kuwa kioo kwa jamii. Nafasi yao ni ngumu yenye changamoto nyingi, kazi zao zina vishawishi vingi na lawama, lakini wakimtanguliza Mungu watafanikiwa,” alisema.

MAKAMU WA RAIS

Awali, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema mkuu wa wilaya aliyepangiwa Wilaya ya Mwanga anatakiwa kwenda kurekebisha makosa yaliyofanyika awali kwa kuwa wilaya hiyo ni nzuri, lakini inashindwa kuendelea inavyotakiwa kutokana na viongozi kutowajibika ipasavyo.

Alisema kwa Wilaya ya Tarime, mteule anayekwenda huko anatakiwa akarekebishe matatizo ya uonevu yaliyoko huko hasa ya ukaidi, unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji ambayo yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi kutokana na tabia korofi za wakazi wa maeneo hayo.

WALIOAPA

Majaji wa Mahakama Kuu walioapishwa jana ni Cyprian Mkeha, Dunstan Ndunguru, Seif Kulita, Dk. Mtemi Kilikamajenga,  Zeferine Galeba, Dk. Juliana Masabo, Mustafa Ismail, Upendo Madeha, Wilbard Mashauri, Yohanne Masara, Dk. Lilian Mongella, Fahamu Mtulya, John Kahyoza, Athumani Kirati na Suzan Mkapa wote wa Mahakama Kuu.

Majaji wa Mahakama ya Rufani ni Sahel Barke, Dk. Rehema Sameji, Dk. Mary Levira, Ignas Kitusi, Winnie Korosso na Lugano Mwandambo.

Wakuu wa wilaya walioapishwa ni Kabeho kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime na Apson kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga.

Wakurugenzi 10 wapya walioteuliwa ni Isaya Mbenje (Pangani), Dk. Fatuma Mganga (Bahi), Regina Bieda (Tunduma), Jonas Malosa (Ulanga), Ali Juma Ali (Njombe), Misana Kangura (Nkasi), Diocres Rutema (Kibondo), Neto Ndilito (Mufindi), Elizabeth Gumbo (Itilima) na Stephen Ndaki (Kishapu).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles