26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Museveni ni Nyerere wa Uganda- Bukenya

yoweri-museveniKAMPALA, UGANDA

MAKAMU wa Rais wa zamani wa Uganda, Profesa Gilbert Bukenya, amemfananisha Rais Yoweri Museveni na Rais wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere huku akitoa mwito kwa Bunge kubadili katiba ili atawale maisha.
Akiwa katika hoteli yake ya Katomi huko Wakiso Ijumaa iliyopita, Mbunge huyo wa zamani wa Busiro, aliliambia gazeti la Observer kuwa Museveni ni mwasisi wa taifa na hivyo anapaswa kutendewa maalumu.

Kwa marais watakaofuata, hata hivyo, Bukenya alisema, wanapaswa watii ukomo wa umri wa miaka 75 uliowekwa katika katiba.

“Lakini kwa Rais Museveni, tumwache aendelee. Ana mawazo mazuri, lakini si kwa viongozi wengine, ambao lazima watii ukomo wa umri huo,” Bukenya alisema.

“Museveni ni Mahathir Mohamad wa Uganda; hivyo, anapaswa kuachwa aendelee ni kifaa maalumu, atuongoze hadi wakati wake utakapofika.”

Mahathir Mohamad, ambaye alitawala kwa miaka 22, alikuwa waziri mkuu aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi nchini Malaysia na anasifiwa kwa kuleta mabadiliko yaliyoitoa nchi hiyo kutoka dunia ya tatu kwenda ya kwanza.

Mbali ya Mahathir Mohamad na Nyerere, pia alimlinganisha Museveni na kiongozi wa zamani wa Singapore, Lee Kuan Yew, kwa kuongoza muda mrefu na kuzipeleka nchi mahali panapostahili.

Bukenya, ambaye alipoteza umakamu wa rais mwaka 2011 na kiti chake cha ubunge wa Busiro mwaka 2016, alisema Museveni amefanya mengi na hivyo anapaswa kupewa kipengele maalumu katika katiba.”

Kwa mujibu wa Bukenya ambaye pia aliwahi kufarakana na Museveni kiasi cha kutaka kupambana naye katika uchaguzi wa urais mwaka huu kabla ya wawili hao kupatana, alisema kati ya viongozi wa zamani ni Museveni pekee aliyeleta maendeleo makubwa kwa taifa hilo.

Museveni ambaye amekuwa akiwania urais pasipo ukomo wa mihula baada ya ile miwili kuondolewa, amebakiza miaka mitatu kufikisha umri wa miaka 75, ambao ni ukomo kwa mtu kuwania urais.

Tayari chama chake tawala cha National Resistance Movement (NRM) kimeanza harakati za kutaka kurekebisha kifungu cha katiba ili kumruhusu Museveni aendelee kugombea urais wakati atakapomaliza muhula wake wa tano mwaka 2021.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles