RAIS Yoweri Museveni wa Uganda alimsifu mwenzake wa Zambia, Edgar Lungu kwa kumkaribisha kuhudhuria maadhimisho ya 52 ya uhuru na kuuonya upinzani kujitenga na machafuko.
Zambia ilisherehekea uhuru wake uliopatikana Oktoba 24, 1964 kutoka Uingereza jana, ambako Museveni alikuwa mgeni mkuu rasmi.
Wakati wa dhifa ya kitaifa juzi usiku, Museveni alishukuru kwa kuwa nyumbani katika siku ya aina yake na ya kihistoria.
“Nina furaha kuwa nyumbani. Watu wa Zambia ni sawa na Waganda na wana lahaja ile ile,” alisema Museveni.
Pia aliwapongeza kwa kumrudisha madarakani Rais Lungu na kuwataka wapinzani washirikiane na Serikali badala ya kuchochea machafuko, aliyoonya hayatawaacha salama.
Museveni pia alimsifu Rais wa zamani, Kenneth Kaunda kwa kazi yake kubwa na nzuri ya maendeleo ya Zambia.
“Tunapaswa kumheshimu Mzee Kaunda. Alijenga Chuo Kikuu cha kwanza cha Zambia. Kwetu Uganda, Kenneth Kaunda ni shujaa,” alisema.