27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Museveni aongoza kura za awali

museveniKAMPALA, Uganda

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, anaelekea kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika juzi huku mpinzani wake mkuu, Dk. Kizza Besigye, akikamatwa na polisi kwa mara ya tatu ndani ya wiki moja.

Pia wafuasi wa mgombea mwingine wa urais ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Amama Mbabazi, nao walikamatwa nje ya nyumba yake.

Matukio ya kukamatwa kwa Dk. Besigye wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC) na wafuasi wa Mbabazi yanayofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na maofisa wa polisi yanatokea ikiwa ni siku ya pili baada ya uchaguzi huo kufanyika na matokeo ya awali kuanza kutangazwa.

Kabla ya Dk. Besigye kukamatwa, matokeo ya awali yaliyotolewa hadi mchana wa jana na Tume ya Uchaguzi ya Uganda (EC) yalionyesha kuwa Museveni wa Chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) alikuwa anaongoza kwa kupata kura 2,715,914 sawa na asilimia 62.82 na Dk. Besigye alipata kura 1,414,708 sawa na asilimia 32.72 ya kura zote zilizohesabiwa huku Mbabazi alipata kura 74,127 sawa na asilimia 1.71.

 JINSI BESIGYE ALIVYOKAMATWA

Kabla ya matokeo hayo kutangazwa, wanajeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na maofisa wa polisi walivamia na kuzingira ofisi kuu za FDC huku Dk. Besigye akiwamo ndani kisha wakamkamata na kuondoka naye katika gari lao.

Katika hatua nyingine, Kituo cha Televisheni cha NBS kiliripoti kuwa Dk. Besigye na Rais wa FDC, Mugisha Muntu, walikamatwa katika ofisi hizo zilizoko Najjanankumbi na wafuasi wa chama hicho wakatawanywa kwa kutumia mabomu ya machozi.

Ilielezwa kuwa viongozi wa FDC walikuwa wakijiandaa kuhutubia wanahabari kuhusu uchaguzi huo uliofanyika jana huku maofisa wa usalama walikuwa wanashika doria katika ofisi hizo na hii ni mara ya tatu kwa Dk. Besigye kukamatwa baada ya juzi jioni kukamatwa katika Kitongoji cha Naguru mjini Kampala katika nyumba ambayo upinzani ulidai wizi wa kura ulikuwa ukifanyika.

Pia Jumatatu alizuiliwa kwa muda wakati akifanya kampeni mjini Kampala.

Baada ya Dk. Besigye kukamatwa, wafuasi wake waliwatuhumu maofisa usalama wa nchi hiyo kuwa wanatumika kumsaidia Museveni kushinda uchaguzi huo ambao leo EC inatarajia kutangaza matokeo ya jumla.

MITANDAO YA KIJAMII YAFUNGWA

Hadi jana mitandao ya kijamii nchini humo bado ilikuwa imefungwa kwa siku ya pili na kwa muda mfupi usiku wa jana watu waliingia mitandaoni lakini asubuhi hawakuweza baada ya juzi Museveni kusema hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu za kiusalama.

MAWAZIRI WAANGUKA

Katika hatua nyingine, mawaziri kadhaa wa Serikali ya Museveni wameshindwa katika uchaguzi wa ubunge. Miongoni mwa walioshindwa ni Waziri wa Ulinzi, Crispus Kiyonga, Waziri wa Haki, Kahinda Otafiire, Waziri wa Habari, Jim Muhwezi, Waziri wa Elimu, Jessica Alupo, Mwanasheria Mkuu, Fred Ruhindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles