32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mchina wa kidato cha nne gumzo kila kona

mchinaNA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

TANGU Baraza la Mitihani nchini (Necta) litangaze matokeo ya kidato cha nne juzi huku mwanafunzi raia wa China aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari wasichana Feza ya jijini Dar es Salaam, Congcong Wang, akishika nafasi ya pili kitaifa, amezua gumzo kubwa kila kona kiasi cha kumfunika aliyeshika nafasi ya kwanza.

Congcong ambaye ni mtoto pekee kwa wazazi wake, Wanhong Wang na baba yake, Dacheng Wang, ni mzaliwa wa Jiji la Changchun nchini China, mbali na kushika nafasi hiyo pia ameshangaza watu kwa kuongoza katika somo la Kiswahili ambalo amepata alama B.

Katika mikusanyiko ya baadhi ya watu, mitandao ya kijamii hasa Facebook, Instagram na WhatsApp jina la Congcong ndilo lililochukua nafasi kubwa ya mijadala mbalimbali wengi wakijiuliza amewezaje kushika nafasi hiyo na hasa kupata alama ya juu katika somo la Kiswahili wakati si lugha yake?

Mbali na mitandao ya kijamii, Shirika la Utangazaji nchini Uingereza kitengo cha Kiswahili (BBC Swahili) wamechapisha mahojiano yake na Congcong pamoja na picha ambayo yupo na mama yake.

Wakati hayo yakizungumzwa kila kona, Congcong mwenyewe ameeleza mafanikio yake akisema yametokana na  ushirikiano alioupata kutoka kwa walimu na wanafunzi wenzake.

Akizungumza na gazeti hili shuleni kwake, Congcong alisema tangu alipotangazwa kushika nafasi ya pili kitaifa aliona picha zake mitandaoni watu wakimsifia hasa hatua yake ya kufaulu somo la Kiswahili.

“Nimefurahi kwa kuwa nimeona watu wananiongelea vizuri, wananipongeza, wananipa moyo, wanaonekana wamependa mafanikio yangu, nimefarijika sana,” alisema Congcong.

“Nilikuwa nashirikiana sana na wenzangu, nimefika Tanzania sijui Kiswahili wala Kiingereza lakini hapa shuleni tunaishi kama familia,” alisema Congcong.

Alisema alipofika Tanzania mwaka 2006 alianzia darasa la pili katika Shule ya Msingi Feza  na alitumia miaka mitatu ili kuweza kujua Kiingereza vizuri wakati kwa upande wa lugha ya Kituruki ambayo inafundishwa shuleni hapo aliweza kuifahamu ndani ya miaka minne.

“Kiswahili nilijifunza vizuri nilipofika sekondari kwa sababu niliogopa ‘penati’, siku hizi ukifeli Kiswahili alama zinashuka, chenyewe nililazimika hadi kusoma masomo ya ziada nilipofika kidato cha pili na cha tatu nikaanza kufaulu,” alisema Congcong.

Alisema pia alikuwa akisoma sana vitabu vya Kiswahili ambavyo alikuwa akijifunza maneno mbalimbali kupitia kamusi ya Kiingereza na Kiswahili.

Alisisitiza kuwa alama ambayo aliwahi kuipata katika somo la Kiswahili na ambayo hataisahau kwa kuwa alifeli ilikuwa 74 ambayo aliipata katika mtihani wa Taifa na alishika namba moja kitaifa katika somo hilo.

Alisema mbali na kupata B ya Kiswahili pia aliwahi kupata medali ambayo ilitolewa mwaka jana alipoenda kwenye mashindano ya lugha hiyo.

Alizungumzia mitaala ya hapa nchini akisema ni migumu tofauti na ya nje hivyo ukitaka kufanikiwa lazima ujishughulishe kwa kusoma sana.

“Mitaala ya Cambridge na Tanzania yote ni migumu lakini ya Tanzania ni zaidi hivyo kikubwa ni kujishughulisha, lazima utumie vizuri muda, vitabu na marafiki ili kuweza kukusaidia mawazo mbalimbali,” alisema Congcong.

Alisema kwa sasa ataendelea kusoma kidato cha tano na cha sita katika shule ya kimataifa ya Feza ambayo amepata ufadhili wa kuendelea na masomo yake.

Alisisitiza kuwa elimu ya juu angependelea zaidi kwenda kusoma nje ya nchi hasa nchi za Ulaya lakini si China.

Kilichomsibu kusoma Tanzania

Akizungumza na gazeti hili kwa lugha ya Kichina huku mwanaye Congcong akitafsiri kwa Kiswahili, mama yake mzazi, Wanhong alisema chanzo cha kuhamia Tanzania ni baada ya mumewe Dacheng Wang ambaye ni mkandarasi kuhamishwa kikazi kutoka nchini China.

Wanhong alisema awali Congcong alianzia masomo yake nchini China baadaye baba yake ambaye ni mkandarasi alihamishiwa nchini Tanzania kikazi ndipo aliamua kuhamisha na familia yake.

“Tulianza kuja huku na baba yake tukafanya uchunguzi tukagundua kuwa Tanzania kuna hali ya hewa nzuri, watu wakarimu maana kila tulipokuwa tunapita tulikuwa tukisalimiwa na kuchangamkiwa na kila mtu ndipo tuliona ni vema tukahamishia makazi yetu na familia nzima nchini Tanzania,” alisema Wanhong.

Alisema anafarijika mwanawe kujua Kiswahili kwa kuwa mpaka sasa yeye hajui kuongea Kiswahili fasaha pamoja na kukaa Tanzania miaka yote.

Alisema anaongea na kuelewa maneno machache ambayo huyatumia katika biashara zake kila siku.

Mwalimu wa Kiswahili wa Congcong anena

Mmoja wa walimu ambao walikuwa wakimfundisha mwanafunzi huyo somo la Kiswahili, Zakhia Ilembe, alisema moja ya vitu ambavyo vilimfanya Congcong afanye vizuri ni pamoja na ushirikiano.

“Tangu alipofika hapa tulikuwa tukiishi naye vizuri, hakuna mwalimu wala mwanafunzi aliyekuwa akimuonyesha kuwa yeye ni mwanafunzi wa kigeni, hakupata kikwazo chochote wakati wa kujifunza,” alisema Ilembe.

Alisema alipofika sekondari alipata shida katika Kiswahili lakini siku zote mwanafunzi huyo ni mtu wa kujichanganya na wenzake na kwa mara kadhaa amekuwa akiwafuata walimu kama kuna mahali hajaelewa.

“Mwenyewe alikuwa akipenda sana kushindana kielimu na alikuwa anataka siku zote kuwa mshindi katika masomo yote ukiacha Kiswahili, hajawahi kupata chini ya alama 90 tangu alipoingia  shule hii,” alisema Ilembe.

Mazingira na ubora wa elimu wachangia ufaulu

Alisema mafanikio ya wanafunzi hao pia yanaenda sambamba na mazingira mazuri yakujifunzia ikiwemo walimu wenye weledi wa hali ya juu na vifaa vya kujifunzia.

“Hakuna miujiza kwenye elimu sisi hapa kwa jinsi wanavyosoma hawa watoto lazima wafaulu, shule zina maabara zenye vifaa vya kutosha, tuna vitu vya kufundishia hapa hata vyuo vikuu hawana, walimu wengine wametoka nje ya nchi, ukiingia huko kwenye mabweni kulivyo hata nyumbani kwangu mimi pabaya, ndani uko kuna hadi mashine za kufulia,” alisema Ilembe.

Mwandishi wa gazeti hili pia alishuhudia  mazingira ya shule hiyo ambayo ni rafiki katika utoaji wa elimu.

Mbali na Shule ya Feza pia Shule ya Sekondari Kaizirege iliyopo Kagera ambayo imeshika namba moja kitaifa inaelezwa kuwa na mazingira mazuri.

Katika picha ambazo zimesambaa mitandaoni na gazeti hili imeziona imeonekana kuwa na vyumba vikubwa vya madarasa na vifaa vya kisasa.

Picha hizo pia zimewaonyesha wanafunzi hao wakiwa katika madarasa safi huku magari makubwa ya Yutong yanayofanana na ya kwenda mikoani yenye nembo ya shule hiyo yanayodaiwa kutumiwa na wanafunzi hao yakiwa yameegeshwa katika eneo la shule hiyo.

Mbali na hizo picha nyingine zilionyesha sehemu ya bweni ambayo ilikuwa imetandikwa zulia jekundu na vitanda vizuri vya kisasa ambavyo walionekana wanafunzi hao wakiwa wamekaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles