MCHEZAJI wa tenisi, Andy Murray, leo anatarajia kurusha karata yake nyingine katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Erste Bank Open dhidi ya John Isner, yanayotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Vienna, Austria.
Nyota huyo namba mbili kwa ubora wa viwango vya mchezo huo duniani alitinga hatua hiyo baada ya kumtoa Gilles Simon katika hatua ya mtoano kwa seti 4-6 6-2 6-2, ambapo kwa sasa atakutana na Isner.
Murray huenda akaibuka namba moja kwa ubora katika mchezo huo iwapo atafanikiwa kumfunga mpinzani wake huyo.
Hata hivyo, ushindi mwingine wa wiki iliyopita katika mashindano ya Paris Masters ulimaanisha kuwa, Novak Djokovic anatakiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali ndipo arejee katika nafasi yake ya mchezo huo.
Murray hadi sasa ameshinda michezo 12 na kufanikiwa kunyakua taji jijini Beijing na Shanghai, akijaribu kurejea katika namba moja ya ubora wa mchezo huo.
Akiwa katika mchezo huo jijini Vienna dhidi ya Simon, Murray alianza taratibu, lakini ilipofika mzunguko wa sita alianza kwa kishindo uliompa nafasi ya kusonga mbele.