22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mungai kuagwa leo Karimjee, mwili wa Sitta nao kuwasili nchini

oth_1303Na WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa   Dar es Salaam leo katika viwanja vya Karimjee.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.

Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.

Alisema pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile  kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.

“Hadi sasa familia tunajua kwamba marehemu aliugua tumbo la kawaida na tulimpeleka hospitalini ambako alifariki dunia, tunaomba familia iachwe, kwa sababu  bado tunashauriana na daktari wake.

“Tumekubaliana mwili wake uagwe kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na familia itasomwa,” alisema William.

Kifo cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa   alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika   hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.

Mmoja wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono  mabadiliko ya siasa.

“Hakuwa na kadi ya Chadema lakini alipenda mabadiliko, mwanaye William aligombea ubunge wa Mafinga kupitia  Chadema na baba yake alimuunga mkono,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.

“Hakuwa na kesho katika maisha yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya siku hiyo hiyo, alikuwa na msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.

Wakati huohuo, mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili leo ukitokea  Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.

Taarifa zilizotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Gerald Mongella, zinasema  mwili huo utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 9.00 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.

“Ijumaa(kesho) saa tatu asubuhi ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja vya Karimjee ambako ndugu na wakazi wa   Dar es Salaam watapata fursa ya kuaga,” alisema Mongella.

Mwili wa Sitta utasafirishwa hadi Dodoma ambako utaagwa na wabunge na baadaye utasafirishwa kwenda Urambo kwa mazishi   Jumamosi.

Sitta alifariki Novemba 07 mwaka huu katika Hospitali ya Technal University alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya tezi dume.

Habari hii imeandikwa na VERONICA ROMWALD, LEONARD MANG’OHA,  TUNU NASSOR NA FERDNANDA MBAMILA

DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles