23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Muleba yatengewa Bilioni 5.57 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa

Na Renatha Kipaka, Bukoba

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera imetengewa Sh bilioni 5.57 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 208 ambapo kwa shule za sekondari ni bilioni 4.16 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 26, aidha kutajengwa vituo shikizi katika shule za msingi saba.

Vituo hivyo shikizi vitajengwa kwa thamani ya Sh milioni 520, ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu umetengewa Sh milioni 80, nyumba za watumishi Sh milioni 90, majengo ya huduma za dharula Sh milioni 300 na ununuzi wa mashine za mionzi Sh milioni 420.

Akizungumza katika kikao cha dharula alichokiitisha Mkuu wa wilaya ya Muleba kwa ajili ya kuanza kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Toba Nguvila amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Sh bilioni 5.57 na kueleza kuwa fedha hizo zimekuja wakati muafaka ambapo wilaya imeanza mikakati ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa ajili ya watoto wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.

Nguvila amesema kuwa tayari kwa baadhi ya kata kuna benki za matofari, mawe, kokoto, mchanga na ujenzi wa misingi na kuinua maboma umeanza.

“Nimeona ni vema niwaite viongozi wenzangu ili tuanze kuweka mikakati ya pamoja, kujadiliana namna ya kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha iliyotolewa na Mheshimiwa rais ili twende kwa pamoja katika utekelezaji,” amesema Nguvila.

Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji kukaa na wataalamu wote wa taasisi za Serikali zilizopo wilayani ili kuandaa namna bora ya kutekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo hali itakayopelekea kumaliza ujenzi huo kwa wakati.

Nguvila amesema wataanza na madarasa ambayo tayari yalikuwa yameanza kujengwa kwa kukamilisha maboma yaliyopo ili yaweze kuwa tayari kutumika huku aki sekta ya misitu kupita na kukagua kwenye shule ili kuweza kupata idadi ya miti ambayo inaweza kuvunwa na kupata mbao zitakazosaidia katika kuezeka.

Ameongeza zaidi kuwa endapo hakutakuwa na mbao za kutosha ameeleza kuwa wilaya inaweeza kuagiza katika mikoa na wilaya ambazo mbao zinapatikana.

Sambamba na hilo ameeleza kuwa ni vema mahitaji yote ya vifaa kama saruji, nondo, mabati vikanunuliwa moja kwa moja viwandani ili kupunguza gharama za manunuzi ya vifaa hivyo.

“Nisingependa kwa wahandisi kuwa na ufujaji wa fedha kwa kuongeza bei za vifaa na ufundi na kwa viongozi wa kata, Vijiji, walimu wakuu pamoja na wenyeviti wa vijiji wahakikishe hakuna rasilimali inayopotea ambayo kila kifaa kitakachotolewa wasimamie kitumike kwenye eneo ambalo limepangwa na kwa wakati,” amesisitiza. Nguvila.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila amesema atahakikisha anasimamia ipasavyo fedha hizo ikiwemo kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na miundombinu hiyo ili kupata vyumba vingi zaidi ya vilivyokusudiwa huku akisisitiza kufuata maelekezo yanayotolewa ili fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wa Muleba.

Kwa upande wake Mbunge wa Muleba Kusini, Dk. Oscar Kikoyo amesema kwa kuwa tayari kuna akiba za benki za matofali katika baadhi ya kata ambayo yamefyatuliwa na kuchomwa na tayari kwa baadhi yao ujenzi wa vyumba vya madarasa umeanza ni vema kuanza kwa kuunga mkono nguvu za wananchi kabla ya kuanza ujenzi mpya.

Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage amewasisitiza viongozi kuhakikisha hawawakatishi kasi wananchi waliyonayo ya kujitolea ambapo amesema kuwa wanaweza wasichangishwe 10,000 za ujenzi wa vyumba vya madarasa badala yake wakashiriki kwenye ujenzi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Muleba, Magongo Justus amewasisitiza viongozi hususani wabunge kuwa na mpango mzuri wa kuwashirikisha viongozi na wananchi ili kushirikiana na kuhakikisha shule mpya na madarasa mapya yanajengwa.

Naye Mdhibiti Ubora wa Shule Mwl. Josephat Joseph ametoa angalizo kwa Wahandisi kuhakikisha wanapojenga vyumba vya madarasa wazingatie miundombinu rafiki kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles