27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

DC Bagamoyo atangaza kuanza kwa Tamasha la 40 la TaSuBa

Na Mwandishi wetu,Bagamoyo

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah, ametangaza kuanza kwa Tamasha la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Octoba 28 hadi 30 mwaka huu.

Akizungumza Jana Bagamoyo mkoani Pwani, Zainab aliwataka wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa nchini na nje ya nchi kushiriki katika Tamasha hilo.

Alisema katika tamasha hilo wanatarajia ushiriki wa viongozi mbalimbali wa kitaifa, mabalozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya, wabunge na viongozi kutoka Taasisi za serikali na sekta binafsi.

“Tamasha litarushwa mubashara na baadhi ya vyombo vya habari nchini ili kuwapa fursa wanachi ambao hawatafika waone wakiwa majumbani au sehemu nyingine.

“Litaonekana dunia nzima na hii inaitoa Bagamoyo na kuiweka katika ramani, Dunia na fursa zilizopo Bagamoyo kufahamika,”alisema.

Msanii wa Muziki kutoka Bagamoyo almaarufu kama Jiko Man alipata fursa ya kutoa vionjo ya muziki utakaokuwepo katika Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Hassan Abasi kwa kushirikiana na TaSUBa na Serikali ya Wilaya Bagamoyo kuhakikisha Tamasha la Sanaa Bagamoyo linafanyika.

Awali akimkaribisha mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dk. Herbert Makoye alisema tamasha hilo linabeba kaulimbiu isemayo, “Sanaa ni Ajira” ikiwa ni mahsusi katika kuonyesha kuwa sanaa ni zaidi ya burudani, inaweza kuwa ajira au biashara na chanzo cha kipato kwa msanii.

Dk. Makoye alisema tamasha hilo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) chini ya Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo.

Dk. Makoye alifafanua kuwa dhumuni la Tamasha ni kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa mtanzania, kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima viwango vyao vya umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.

Aliongeza kuwa lengo lingine la Tamasha ni kukutanisha watu wa tamaduni tofauti kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni, kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa, pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya sanaa na kutoa burudani kwa watanzania na wageni.

“Tamasha la mwaka huu litapambwa na ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, singeli, sarakasi, mazingaombwe, maigizo pamoja na maonyesho na biashara ya sanaa za ufundi,”alisema

Dk. Makoye alisema jumla ya vikundi ambavyo vimethibitisha kushiriki mpaka sasa ni 70, ambapo vikundi vya ndani ya nchi ni 60 na vikundi 10 kutoka nje ya nchi (India, Malawi na Mayotte). Pamoja na burudani hizo, kutakuwa pia na vyakula vya asili na vinywaji vya asili.

Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbertm Makoye akieleza mafanikio ambayo Tamasha la Bagamoyo limeyapata kwa kipindi cha miaka 40 wakati alipoongea na vyombo vya habari katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Kiagho Kilonzo alisema Taasisi hiyo inaungana na TaSUBa katika kufanikisha Tamasha la 40 la Sanaa na Utamaduni, ambapo katika kutekeleza hilo kutakua na hema kwa ajili ya kuonyesha filamu ambalo litabeba watu takribani mia moja.

Ndani kutakua na screen kubwa ambazo zitaonyesha filamu. Lengo kubwa likiwa ni kuendeleza na kudumisha filamu,kutakua na wasanii wa filamu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania hususani jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuipendezesha siku hiyo na kuleta hamasa kwa vijana,” alisema Dkt. Kilonzo.

Kaimu Katibu Mtendaji, Baraza la Sanaa Tanzania B. Matiko Mniko alisema tamasha la Bagamoyo ni fursa nzuri kwa Tanzania kuinua utalii wa utamaduni nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles