AVELINE KITOMARY
Mkurugenzi wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Lawrence Museru amesema hospitali hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandisha wa habari leo Jumanne Novemba 19, jijini Dar es salaam Museru amesema changamoto zilizotatuliwa ni ukosefu wa dawa, matengenezo ya mashine za MRI na CT Scan, kuongeza vitanda vya ICU na kupatia kero za wafanyakazi.
“Upatikanaji wa dawa hadi sasa wagonjwa wanapata dawa kwa asilimia 96 kutoka kwenye maduka ya hospitali ukilinganisha na asilimia 40 kabla ya uboreshaji jumla ya Sh bilioni 18 zinazotumika kununua dawa kwa kila mwezi.
“Kwa upande wa vitanda vya ICU sasa tumefikia 78 kwa sasa hakuna kero za wagonjwa kukosa vitanda na pia huduma zimekuwa za haraka hivyo wagonjwa hawakai hospitali muda mrefu kutokana na kutengeneza vifaa vya matibabu kama CT Scan na MRI,” amesema Museru.
Aidha amebainisha mafanikio mengine ni pamoja na huduma za upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto, upandikizaji wa figo na tiba radiliolojia.
Amesema wagonjwa 51 wamepata huduma ya figo ambapo jumla ya Sh. bilioni 4.6 zimeokolewa kwa wagonjwa wa figo na kwamba gharama ya ndani ni Sh. milioni 30 na gharama za nje ni Sh. milioni 100.
Kwa upande wa upandkizaji wa vifaa vya kusikia, watoto 34 wamepata huduma hiyo ambapo gharama za ndani ni Sh. milioni 36 huku gharama za nje zikiwa Sh. milioni 100 na kupelekea jumla ya Sh. bilioni mbili kuokolewa.
Huduma za radiolojia gharama za ndani Sh. milioni nane, gharama za nje Sh. milioni 90 ambapo jumla ya Sh. bilioni 24 zimeokolewa.