27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Muhimbili yabadili mbinu kukabili vifo vya watoto njiti

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kutumia mbinu nyingine mbadala kukabili vifo vya watoto waliozaliwa kabla ya kutimiza umri wa miezi sita (njiti).

Hapo kabla, mtoto njiti alipozaliwa madaktari walimchukua na kuanza kumpatia huduma wodini kwa kipindi fulani hadi hali yake inapoimarika kisha walimpatia mama yake aanze kumlea kwa njia ya kumbatio la kangaroo.

Kupitia mbinu mpya iliyoanzishwa sasa, njiti anapozaliwa moja kwa moja hupatiwa mama yake na kuanza kumlea kwa mtindo wa kangaroo, badala ya kuwatenganisha kama ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza hospitalini hapo juzi kuhusu Kongamano la Kwanza la Sayansi la Wataalamu Wanaohudumia Watoto Wachanga katika hospitali zote za rufaa hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wachanga MNH, Dk. Edna Majaliwa, alisema:

“Mbinu hii inaonyesha mafanikio katika kukabili vifo vya watoto wachanga (njiti), inatumika katika mataifa mengine, pia nasi tumeona vema kuitumia, mtoto njiti huhitaji joto la mama na kumsaidia kumuweka katika ziwa ili anyonye vizuri.

“Kangaroo ni njia kubwa inayotumika kuweza kusaidia kuokoa maisha ya watoto njiti, awali tulilazimika kuwaweka kwanza wodini ili kuwa-stabilize, lakini tunaona mbinu hii nyingine ya kumuweka kwa mama yake pindi tu anapozaliwa ni bora zaidi, inasaidia pia kumwepusha kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali na hivyo kuzuia vifo,” alisema.

Dk. Edna alisema hadi sasa hakuna sababu inayoweza kutajwa moja kwa moja kwamba ndiyo chanzo cha watoto kuzaliwa njiti.

“Lakini kuna sababu tofauti ambazo zinatajwa kuchangia hali hiyo kuweza kutokea, ikiwamo uzazi wa watoto pacha, mjamzito kuugua magonjwa mbalimbali, upungufu wa damu na shinikizo la damu,” alisema.

Pia alisema kwa kawaida katika kitengo hicho hupokea watoto kati ya 70 hadi 90, lakini kuanzia kipindi cha Oktoba hadi Mei hupokea idadi kubwa zaidi kati ya watoto 200 hadi 250.

“Ili kuepuka kupata mtoto njiti, ni muhimu mama anapohisi kuwa ni mjamzito awahi hospitalini kwa uchunguzi na kuanza kliniki mara moja kama itaonekana tayari ni mjamzito ili afuatiliwe hali yake kwa ukaribu zaidi,” alishauri.

Awali akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alisema takwimu zinaonesha kati ya asilimia 13 hadi 17 ya watoto wanaozaliwa nchini ni njiti.

“Serikali imekuwa ikiratibu programu mbalimbali kupunguza idadi ya vifo vya watoto hawa, lakini pia kwa kushirikiana na Tamisemi tumehakikisha kila hospitali nchini ina wodi ya kuhudumia watoto wachanga,” alisema.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania (PAT),  Dk. Sekela Mwakyusa, alisema mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu hao kupata mbinu mbalimbali za kuwahudumia watoto hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles