24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Majambazi 7 yauawa yakirushiana risasi na polisi kwa dakika 45

NA PETER FABIAN, MWANZA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, limewaua majambazi saba katika tukio la majibizano ya kurushiana risasi kwa dakika 45 na kufanikiwa kukamata silaha mbili eneo la mlima uliopo jirani na Shule ya Msingi Kishili wilayani Nyamagana.

Tukio hilo limetokea saa nne usiku baada ya kuwapo taarifa za kiintelijensia za polisi kutoka kwa raia wema kwamba kuna kikundi cha watu kinachojihusisha na uhalifu wa kutumia silaha kimeingia kikijiandaa kufanya matukio kadhaa katika maeneo mbalimbali ya jijini Mwanza.

Akizungumza katika eneo la tukio wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna, alisema baada ya taarifa za raia wema na kiintelijensia walianza kuwafuatilia majambazi hao.

Shanna alisema katika kufuatilia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aliyefahamika kwa jina la Hashim Abass (48) ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Shamaliwa, Kata ya Igoma akiwa anafuatilia eneo waliopanga kufanya uhalifu wa kutumia silaha ili kupora mali katikati ya mitaa ya Mwanza.

“Baada ya kufanikiwa kumkamata jambazi huyo na kuhojiwa ndipo alikiri kwamba yeye ni miongoni mwa majambazi saba ambao wamekuwa wakifanya uhalifu wa kutumia silaha na kupora fedha na mali za watu na wafanyabiashara katika mikoa ya Mwanza, Mara, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Geita,” alisema.

Shanna alisema mtuhumiwa huyo alikiri pia kuhusika katika matukio ya kumuua mfanyabiashara, Richard Slaa, ambaye ni mkazi wa Nyamagana, kosa jingine la unyang’anyi wa kutumia silaha mkoani Geita, unyang’anyi wa kutumia silaha wilayani Bukombe, unyang’anyi wa kutumia silaha wilayani Chato.

Alitaja matukio mengine waliyofanya ni unyang’anyi wa kutumia silaha katika duka la jumla la kuuza bia wilayani Geita, tukio la unyang’anyi kwa mfanyabiashara wa dhahabu eneo la Pida wilayani Bunda (Mara), matukio mawili ya unyang’anyi kwa kutumia silaha katika wilaya za Itilima, Bariadi, Meatu (Simiyu), pia alieleza kutumwa na wenzake waliopo eneo la mlima wa Shule ya Msingi Kishili.

“Ilipofika saa nne usiku walimchukua jambazi Abass na kuongozana naye huku akiwasiliana na wenzake kwa simu ya mkononi walipoweka kambi eneo hilo la Mlima wa Kishili na walipokaribia mtuhumiwa huyo akatoa ishara ya sauti kubwa ya neno shemeji ikiwa ni ishara ya kuwashtua wenzake waliokuwa mafichoni,” alisema.

Shanna alisema baada ya sauti hiyo ghafla majambazi hao sita wakaanza kufyatua risasi kujihami na kuwashambulia askari huku wakifanikiwa kumpiga risasi mwenzao na kufariki dunia papo hapo na askari aliyekuwa nyuma yake akijeruhiwa mkononi baada ya risasi kushindwa kupenya kwenye koti la kuzuia risasi.

“Askari wetu alichukua tahadhari ikiwamo kuwapa ishara wenzake ambao nao waliendelea kusogea kumsaidia kukabiliana na majambazi hao kwa mapigano yaliyodumu kwa dakika 45 na kufanikiwa kuwaua majambazi watatu waliokuwa wamejificha sehemu moja na kuwafuatilia wengine watatu waliokuwa wakikimbia huku wakiwafyatulia risasi askari kabla ya kufanikiwa kuwaua,” alisema.

Shanna alisema baada ya kuwaua walifanya msako eneo la tukio na kufanikiwa kupata silaha mbili za kivita, moja AK 47 yenye namba 56-3844714 ikiwa na magazini mbili na risasi 71 na silaha ya pili aina ya FN (G 3) yenye namba 865895 ikiwa na magazini moja na risasi tano.

“Tuombe wananchi wajitokeze ili kuwatambua majina yao na wanakoishi na watakaotambuliwa miili yao itakabidhiwa kwa ndugu na jamaa kuendelea na taratibu za mazishi, kwa sasa miili ya majambazi hao itapelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Mkoa ya Sekoutoure,” alisema.

Aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri ili kuwezesha kuwakamata majambazi na makundi ya uhalifu yanayopora fedha na mali za wananchi ikiwamo kupanga njama za kuvamia wakati askari wa kikosi maalumu kwa kushirikiana na wenzao wa Geita, Simiyu, Mara, Kagera na Shinyanga wakiendelea kuwatafuta majambazi wengine waliotajwa na wenzao.

RC MWANZA

Mongela aliyeambatana na Shanna katika eneo la tukio hilo na kuzungumza na wananchi wa kata za Kishili na Igoma, aliwapongeza askari kwa kufanikiwa kuzima mbinu chafu za majambazi hayo yaliyokuwa yamejipanga kufanya uhalifu na mauaji.

Mongela alisema kujitokeza kwa wananchi hao na kukesha katika tukio hilo ni kielelezo tosha kuwa wameanza kutambua dhana ya ulinzi shirikishi na watakuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili kusaidiana na askari ambao ni wachache kufika kila maeneo ya mitaa ya Mwanza.

“Tuwapongeze Shanna na askari wake kwa kuzima jaribio la kihalifu ambalo pengine lingetekelezwa na majambazi hao lingesababisha baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki kupoteza maisha huku mali zao zikichukuliwa na baadhi yenu mmetoa ushuhuda kuwa mlikuwa mkiwaona wakipanda mlimani na mlipojaribu kuwauliza waliwadanganya kuwa wanafanya utafiti wa madini hivyo ni vyema mkaendelea kutoa taarifa za siri kwa polisi na hamtatajwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles