25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

MUHIMBILI YAANZISHA UPASUAJI KUPANDIKIZA MISHIPA YA DAMU

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


muhimbiliJOPO la madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kutoka nchini Australia, wamefanikisha kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu na misuli (free gracilis muscle transfer) kwa mara ya kwanza nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo, daktari bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo, Ibrahim Mkoma, alisema wamepandikiza mishipa na misuli katika mguu wa mwanamume mwenye umri wa miaka 39 ambaye alipata ajali ya moto.

Alisema misuli na mishipa hiyo ilitolewa katika sehemu ya paja la kulia la mgonjwa huyo na kupandikizwa katika mguu wake wa kushoto.

“Ni upasuaji ghali mno, nchini Australia mgonjwa hutozwa kati ya Dola za Marekani 75 hadi 100 kwa kila dakika na huweza kuchukua kati ya saa sita au saba,” alisema.

Alisema mgonjwa huyo waliyemfanyia upasuaji huo aliwahi kupandikizwa ngozi katika eneo hilo, lakini haikushika kwa sababu misuli yake ilikuwa iko nje.

“Wagonjwa wengi wa aina hii huwa tunalazimika kuwakata viungo vyao, hasa miguu na mikono kwa sababu iwapo kidonda hakitapona mwisho huweza kusababisha madhara mengine katika mwili wake,” alisema.

Alisema hadi sasa tayari wagonjwa wanne wamekatwa viungo vyao kutokana na hali hiyo.

“Kuna mmoja ambaye alipata ajali ya moto tukalazimika kukata mikono yake yote miwili, mwingine tulimkata mkono na mguu, mwingine mkono mmoja na mwingine mguu mmoja,” alisema.

“Kwa hiyo, kufanyika kwa upasuaji huu kutatusaidia kujifunza namna ambavyo unafanyika ili tuweze kuwasaidia wagonjwa wetu kuokoa viungo vyao.

“Tumeanza mazungumzo nao, ili mwakani Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kianze kutoa mafunzo juu ya upasuaji huu,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema iwapo mgonjwa atakwenda kutibiwa nje ya nchi hugharimu hadi Dola za Marekani 40,000.

“Gharama hiyo ni pasipo kujumuisha za chumba cha upasuaji, malipo ya wapasuaji, gharama za wodini na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles