HARARE, ZIMBABWE
SIKU chache tu baada ya kusherehekea miaka 93 ya kuzaliwa, Rais wa Robert Mugabe amesafiri kwenda Singapore kwa uchunguzi wa kimatibabu.
Mugabe alionekana kuwa dhaifu wakati wa sherehe hizo zilizofanyika Jumamosi iliyopita wakati aliposimama kwa zaidi ya saa moja akisoma hotuba.
Alikuwa akisimama kwa muda kabla ya kuendelea kusoma hotuba hiyo, huku akimumunya maneno mara kwa mara.
“Rais aliondoka asubuhi kuelekea Singapore kwa uchunguzi wa kimatibabu. Tunamtarajia kurejea nyumbani wiki ijayo,” alisema katibu wake wa mawasiliano, George Charamba akizungumza na gazeti la Herald la Zimbabwe juzi.
Mugabe ni kiongozi mkongwe zaidi duniani, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980 katika uongozi ambao unadaiwa kujaa dhuluma, wizi wa kura na kudhoofika kwa uchumi.
Hivi majuzi alifanya ziara Asia na kukaa wiki kadhaa wakati wa likizo yake ya kila mwaka.
Chama chake tawala cha ZANU-PF, kimeonekana kuingia katika mpasuko wa makundi yanayowania kumrithi baada ya kukataa kutaja atakayechukua nafasi yake.
Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa, anaonekana kuwa na nafasi ya kumrithi Mugabe kama ilivyo kwa mke wa rais huyo, Grace Mugabe (51).