NA AZIZA MASOUD
TUNAELEKEA kipindi cha likizo, shule nyingi kwa sasa zinafungwa kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu mbalimbali, ikiwamo Krismasi na mwaka mpya.
Msimu huu wa likizo ni moja kati ya vipindi vinavyowafanya watoto wapumzike kwakuwa hufunga kwa muda mrefu, yaani zaidi ya mwezi mmoja.
Mbali na watoto kusafiri kwenda  maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusalimia ndugu na jamaa, pia ni kipindi wanachotumia muda mwingi kucheza na kufahamiana na marafiki wapya.
Kutokana na mazingira hayo, ambayo yanasababisha watoto kukaa muda mrefu nyumbani, mzazi usipokuwa makini mtoto anaweza kubadilika kifikra na kiakili.
Watoto ambao hawafuatiliwi na wazazi au walezi huhamishia akili zao kufikiri mambo tofauti na masomo.
Pamoja na kwamba likizo ni kipindi cha kupumzika, hata hivyo, haimaanishi mtoto akae bila kujikumbushia masomo na kusababisha anaporejea shuleni anakuwa kama anaanza upya.
Wapo baadhi ya watoto ambao wakifika shuleni baada ya likizo wanasahau kila kitu na kusababisha usumbufu kwa walimu wanaowafundisha.
Ni muhimu wazazi kupanga ratiba nzuri kwa mtoto anapokuwa likizo ili aweze kutumia muda wake pia kujisomea.
Tengeneza ratiba ambayo itamfanya mtoto wako ajisomee baada au kabla ya kumaliza kucheza.
Kama mzazi unaona umebanwa sana na kazi na huwezi kumsimamia mtoto ajikumbushie masomo yake, ni vema ukamtafutia sehemu au mwalimu ambaye atamfundisha masomo ya ziada.
Ratiba hii isifuatwe tu akiwa nyumbani, bali hata kama ikitokea mtoto kasafiri, ni vema ukatoa maelekezo hayo kwa wenyeji wake huko aendako, hali hii itamjenga kuwa na ratiba nzuri nyakati za likizo.
Hiyo itamsaidia si tu kuwa na kumbukumbu ya vitu vya darasani, pia itamjengea utaratibu mzuri wa kucheza kwa maana atakuwa anacheza huku akijua anapaswa kwenda kujifunza masomo ya ziada.
Ni vizuri kumwangalia mtoto kwa ukaribu ili kumwepusha na makundi hatarishi.