26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto albino azikwa chini ya ulinzi

Joseph KonyoNa Benjamin Masese, Geita
MABAKI ya mwili wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati (1) ambaye alitekwa Februari 16, mwaka huu na kuuawa kwa kukatwa mikono na miguu, jana yalizikwa kaburini chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika saa tisa alasiri katika Kijiji cha Ilelema, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, huku polisi wakiwa wameimarisha ulinzi.
Mabaki ya mwili wa mtoto huyo yalipelekwa kwanza nyumbani kwa babu yake, Misalaba Manyamche, saa sita mchana kabla ya kuanza kwa msafara wa kuelekea makaburini ulioongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo.
Katika msafara huo pia walikuwepo viongozi wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali.
Licha ya Kijiji hicho kuwa porini na kutokuwapo na idadi kubwa ya watu, vilio vya ndugu na jamaa wa mtoto huyo na shughuli ya maziko ya mwili wake ilifanywa na askari polisi walioongozwa na Konyo.

Akizungumza katika mazishi hayo, Kamanda Konyo alisema mauaji ya watu wenye ulemavu yanaichafua Serikali na kwamba hayupo tayari kuona mauaji hayo yakiendelea katika eneo la mkoa wake.
“Vitendo vya kikatili vya namna hii vinatangazwa dunia nzima. Kama mnavyojua hizi ni nyakati za utandawazi, kuna redio, televisheni na mitandao ya kijamii, kila kitu kinachofanyika kinajulikana duniani.
“Dunia inatafsiri kwamba Tanzania ni nchi ya uchawi, jambo ambalo ni fedheha kwa taifa na viongozi wake, hivyo Serikali haipo tayari kuvumilia vitendo hivi, tutahakikisha waliohusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la AIC Wilaya ya Chato, Daudi Kaswahili, aliwataka watekaji na wauaji wa mtoto Yohana wajitokeza, vinginevyo maisha yao yatakuwa hatarini siku za usoni.
“Mtu yeyote aliyehusika katika tukio hili ni vema akajitokeza na kuombewa, vinginevyo atapata adhabu kali kwa Mwenyezi Mungu, ipo siku aliyefanya kosa hili la kikatili kwa kutaka mali, damu ya huyu mtoto na sauti ya mtoto huyu ataisikia ikizungumza ndani,” alisema Mchungaji Kaswahili.
Naye Mwakilishi wa Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali mkoani Geita, Gerald Ruhere, alisema tukio ni la kusikitisha na serikali inapaswa kuonyesha uwezo wake wa kulinda raia.
“Aibu hii inapaswa kufanyiwa kazi na Serikali, taifa letu linasifika kama kisiwa cha amani na usalama, lakini watu wake wanakufa kama kuku, hivyo ni vema msako wa kuwakamata wauaji ufanyike,” alisema Ruhere.
Maziko ya mabaki ya mwili wa mtoto Yohana yamefanyika wakati mama yake, Ester Jonas akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando anakopatiwa matibabu, baada ya kukatwa mapanga na watekaji na baba yake anashikiliwa na Jeshi la Polisi akisaidia uchunguzi wa tukio hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles