30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto afanyiwa upasuaji wa moyo mara sita

daktariNa MWANDISHI WETU, DODOMA

MTOTO wa Mkurugenzi wa Kiwanda cha Magodoro cha Dodoma Asili, Haidary Gulamali, amekwisha fanyiwa upasuaji wa moyo mara sita.

Pia, mtoto huyo ambaye hakutajwa jina, atafanyiwa upasuaji mwingine India Desemba mwaka huu.

Taarifa hiyo ilitolewa na Gulamali mwenyewe alipokuwa akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyetembelea kiwanda chake mjini hapa.

“Mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo mara sita na Desemba mwaka huu atafanyiwa upasuaji mwingine  India. Mara zote nilizokwenda India, nimefahamiana na kujenga urafiki na madaktari wengi wa moyo.

“Kwa kuwa ninaguswa na matatizo ya moyo, nitawaleta nchini madaktari bingwa 14 wa moyo waje kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto watakaobainika kuwa na matatizo hayo,” alisema Gulamali.

Kwa mujibu wa Gulamali, madaktari hao ambao wanatarajia kuingia nchini hivi karibuni, wataanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza na baadaye katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mbali na kupeleka madaktari hao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, pia Gulamali aliahidi kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana magodoro mapya kwenye hospitali hiyo.

Wakati huo huo, Gulamali alisema anatarajia kujenga kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti kitakachogharimu Sh bilioni nne.

Alimkabidhi Waziri Mkuu magodoro 200 yenye thamani ya Sh milioni 10 kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu mkoani Kagera.

Waziri Mkuu alimshukuru Gulamali kwa msaada huo na kuahidi kuyafikisha mkoani Kagera kwa waathirika wa tetemeko hilo.

Alimpongeza Gulamali kwa uamuzi wake wa kuleta madaktari bingwa wa moyo kutoka India watakaotoa huduma ya upasuaji kwa watoto kwa kuwa baadhi yao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka  India.

“Pia, nimefarijika kukuta kiwanda chako kipo hai na kinafanya kazi nzuri ya kutengeneza magodoro bora.

“Nakupongeza kwa kutekeleza wito wetu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa kuajiri Watanzania 147 kati ya  watumishi 150 walioajiriwa kiwandani hapa,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles