Na JOACHIM MABULA
UTAFITI wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kansas, umegundua uwezezekano wa kuwapo uhusiano wa karibu kati ya matumizi ya maziwa na afya ya ubongo.
Utafiti huo mpya umebaini ukaribu kati ya matumizi ya maziwa na kiasi cha kichocheo cha asili kiitwacho Glutathione kinachopatikana kwenye ubongo wa mtu mzima mwenye afya njema.
Dk. In-Yung Choi ambaye ni Profesa Msaidizi wa Taasisi ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Kansas, anayejishughulisha na mfumo wa fahamu kwa pamoja na Dk. Debra Sullivan ambaye ni Profesa na Mwenyekiti wa Kitengo cha Lishe katika taasisi hiyo, walifanya kazi kwa kushirikiana katika utafiti huo, kuhusu maziwa.
Matokeo ya utafiti wao yalichapishwa katika jarida The American Journal of Clinical Nutrition, wakishauri kwamba unywaji wa maziwa unaweza kuleta faida mwilini.
Tunatambua kwa muda mrefu kuhusu maziwa kuwa ni muhimu kwa mifupa yetu na muhimu kwa nyama za miili yetu. Dk. Sullivan anasema; "Utafiti huu unaonyesha kwamba maziwa yanaweza kuwa muhimu kwa ubongo wako pia."
Kikundi cha Dk. Choi, kiliuliza washiriki 60 kwenye utafiti huo, kikihusisha ulaji wao pamoja na kupiga picha za ubongo wao, zilizotumika kupima viwango vya Glutathione ambayo ndio kichocheo chenye nguvu katika ubongo.
Watafiti walipata washiriki walioonyesha kwamba wamekunywa maziwa muda si mrefu na walikuwa na viwango vikubwa vya Glutathione kwenye ubongo wao.
Watafiti walisema Glutathione inaweza kusaidia kuondoa mkazo (Oxidative Stress) na kuondoa uharibifu unaoweza kusababishwa na utendaji wa kawaida wa ubongo.
Dk. Choi anasema mara nyingi mkazo huu huambatana na magonjwa tofauti na hali mbalimbali kama ugonjwa wa Alzheimer (ugonjwa wenye dalili za upungufu wa akili), ugonjwa wa Parkinson (ugonjwa wenye kuharibu mfumo wa fahamu & kuharibu ujongeaji/kutembea) na hali zingine nyingi.
Je, Kati ya maziwa ‘fresh’ na mtindi yapi bora?
Maziwa freshi au mtindi yana virutubishi muhimu hasa protini, madini na vitamini. Unaweza kutumia maziwa aina yoyote kutegemea matumizi yake. Hata hivyo maziwa ya mtindi huyeyushwa kwa urahisi zaidi tumboni, pia husaidia uyeyushwaji wa vyakula vingine na ufyonzwaji wa baadhi ya virutubishi.
Hivyo, maziwa ya mtindi yanapendekezwa zaidi hasa kwa wagonjwa kwani yanamsaidia mgonjwa kupata virutubishi vingi zaidi kwa haraka. Maziwa ya mtindi pia yana aina ya bakteria wazuri na salama ambao huweza kuzuia au kutibu fangasi katika mfumo wa chakula.