27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mtikila afariki dunia ajalini

MtikilaChristopherMtikilaNA Waandishi Wetu, Chalinze na Dar
MWANASIASA mkongwe na Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila (62) amefariki dunia kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Msolwa,   Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, barabara Kuu ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Jafary Ibrahimu alisema ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri usiku wa kuamkia jana alipokuwa akitoka mkoani Njombe kurejea Dar es Salaam.

 

“Ni kweli Mtikila amefariki dunia saa 11 alfajiri katika eneo la Msolwa karibu na mjini wa Chalinze lakini kifo chake kimesababishwa na ajali ya gari lililoacha njia na kupinduka kutokana na mwendo kasi,”alisema Kamanda Ibrahimu

 

Alisema Mtikila ambaye ni mkazi wa Mikocheni B  Dar es Salaam alikuwa na  wenzake watatu katika  gari  ya Toyota Corola ambayo ilipofika eneo la tukio  iliacha njia na kuingia porini   umbali wa mita 200 hali iliyosababisha tairi ya mbele kushoto   kupasuka na kupinduka na kusababisha kifo cha Mtikila huku wenzake watatu wakijeruhiwa.

Kamanda alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba ilitokea kwenye eneo ambalo siyo makazi ya watu jambo  lilisababisha waliopatwa na ajali  kukosa msaada wa haraka.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mchungaji Patrick Mgaya (37), Ally Mohammed (42) wote wakazi wa   Dar es Salaam.

Alisema polisi wanamshikilia dereva wa gari hilo, George Stephen (31) maarufu kama Ponela mkazi wa Dar es Salaam kwa   mahojiano zaidi.

Kamanda Ibrahim alisema   mwili wa marehemu Mtikila ulihifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi na majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema   gari hilo lilikua kwenye mwendokasi wakati linalipita kijiji Msolwa.
“Wakati gari hii inapita kijijini Msolwa alfajiri ya leo (jana) lilikua kwenye mwendo kasi sana hali iliyosababisha   ajali  hiyo,”alisema Mussa Omary mkazi wa kijiji hicho.

Mmoja wa majeruhi,   Mchungaji   Patrick Mgaya alipata  matibabu katika Hospitali ya Tumbi na kuruhusiwa kwa vile kuwa hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Mgaya, walitoka Njombe walkokuwa wakimnadi  mmoja wa wagombea  ubunge ambaye hakutaka kumtaja.

 

Alisema walipomaliza mkutano wa kampeni  walipumzika kabla ya kuanza safiri ya kurejea Dar es Salaam.

Mchungaji Mgaya  alisema  wakati wanapanga kurudi Dar es Salaam hawakuwa  na usafiri hivyo walilazimika  kukodi gari ya George (aliyekuwa dereva wa gari hilo) na kuanza safari  usiku.

Alisema  walipofika karibu na eneo la ajali  waliona dereva anaongeza mwendo na wao wakamwambia apunguze   na ndipo muda mfupi  baadaye waliona gari linaanza kuyumba na  kupoteza muelekeo hali ambayo iliyosababisha liache njia na kupinduka.

Mgaya alisema  muda mmfupi  baada ya ajali hiyo walitokea  a wasamaria wema ambao   waliwasaidia kuwaokoa  kabla ya kutokea  polisi kutoka Chalinze ambao waliwachukua  na kuwapeleka katika Kituo cha Afya Chalinze na wengine katika Hospitali ya Tumbi.
Hata hivyo alisema wakati wanatolewa katika gari, Mchungaji Mtikila alikuwa tayari amefariki dunia huku  Mohamed Ally akiwa katika hali mbaya.

Mfanyakazi mmoja wa chumba cha maiti  katika Hospitali ya Tumbi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema  wa alipokea mwili wa   Mtikila ambaye alionekana ameumia kidogo   kichwani na kiunoni   na hakuwa na majeraha makubwa.

“Niliona mwili wa Mtikila nikiwa chumba cha maiti lakini    majeraha yake ni madogo  kwa sababu  aliumia kidogo kichwani na   mgongoni lakini aliyeumia sana na yule Ally Mohamed,”alisema mfanyakazi huyo.

Kamanda Ibrahim alisema   uchunguzi zaidi wa ajali hiyo   unaendelea na   taarifa zitaendelea kutolewa   huku akitoa pole kwa familia ya Mchungaji Mtikila katika kipindi hiki kigumu.

Aliwataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani na   wazingatie sheria ikiwamo  kutumia mwendo ambao ni salama kwao na abiria wao.

 

 Nyumbani kwa Mtikila
MTANZANIA jana  ilifika nyumbani kwa marehemu Mtikila, Mikocheni B Dar es Salaam   na kushuhudia  watu wengi wakiwamo viongozi wa serikali   wakiomboleza   na kuwapa pole wafiwa.

Akizungumzia alivyopokea msiba huo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema    amepoteza mdau wa siasa na  ameshtushwa na kifo hicho ambacho kitawakutanisha watu wengi hivyo kitumike kama njia moja ya kusambaza amani.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha DP, Mshambichake Ferouz, alisema   chama hicho kimepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na pengo lake halizibiki kwa vile alikuwa mstari wa mbele kuhakikiksha chama hicho kinasonga mbele.

Habari hii imeandikwa na GUSTAPHU HAULE na Patricia Kimelemeta, Chalinze na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles