25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MTIFUANO WANAOTAJWA KUONDOKA CHADEMA

NORA DAMIAN Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


WIMBI la wapinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) linaonekana kutaka kukivuruga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya wabunge wengine kutajwa kutaka kukihama.

Baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya CUF, Chadema na ACT-Wazalendo, wamehama na kujiunga na CCM, huku wakisema kuwa wamevutiwa na sera za Rais Dk. John Magufuli.

Hata hivyo, wimbi hilo linaonekana bado linainyemelea Chadema kutokana na kuwapo kwa taarifa za baadhi ya wabunge wake kutaka kuhama na kujiunga CCM.

Wabunge ambao wanatajwa kutaka kukihama chama hicho na majimbo yao kwenye mabano ni Saed Kubenea (Ubungo), John Mnyika (Kibamba), James ole Milya (Simanjiro) na Ruth Mollel wa viti maalumu

 

MILYA

Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro, Milya, alisema hana mpango wa kuhama Chadema na kwamba anathamini heshima aliyopewa na wananchi wa jimbo hilo mwaka 2015.

“Niliweka msimamo nisijibu popote mpaka Ijumaa ifike, lakini kwa heshima yenu nimesema niwajulishe kwa sababu ninyi ndio marafiki na mabosi wangu.

“Heshima mliyonipa mwaka 2015 ni kubwa sana na mimi natambua hilo. Ninaomba wote mpuuze yanayoandikwa kwenye mitandao ya jamii, wapiga ramli waendelee kupiga ramli zao hasa kwenye nyakati hizi mbaya kwenye ukuaji wa demokrasia ya taifa letu,” alisema Milya.

 

KUBENEA

Mbunge wa Ubungo, Kubenea, alisema leo anakusudia kujivua uanachama wa Chadema.

Kwa takribani wiki tatu, Kubenea amekuwa akitajwa na watu mbalimbali kwamba ni kati ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao watakihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema litawekwa hadharani leo na kwamba litarushwa moja moja katika vituo vya televisheni.

 

Licha ya kushindwa kuthibitisha kwamba atahamia CCM, lakini alisisitiza kwamba anahama Chadema.

 

MNYIKA

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, alisema Mnyika hana mpango wa kukihama chama hicho na kwamba yuko kwenye mikono salama.

Alisema wapinzani wanapewa misukosuko na majaribu ili kupima imani yao, lakini wao wataendelea kuwa imara.

“Siasa ni maisha na kwenye kuishi si lazima mtu aishi sehemu moja, cha msingi ni kwamba Chadema kitaendelea kuwa imara na kila mwenye roho ngumu atuvumilie, tutavuka tu.

“Kama ugumu wa maisha ndio unawafanya watu wakimbie siasa au kuogopa biashara zao kufilisiwa, upinzani hauwezi ‘ku – guarantee’ mtu asifukuzwe kazi ama biashara yake isifungiwe.

“(Mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe ametikiswa, lakini hadi leo bado ni mwenyekiti, kwa hiyo siwezi kusema kwamba hakuna mwingine atakayehama… hiyo itategemea na roho ya mtu baada ya kupata majaribu, atakayeshinda tutabaki naye, atakayeshindwa ataondoka,” alisema Jacob.

Kuhusu wabunge wengine wanaotajwa alisema: “Kubenea sijawasiliana naye bado na Mollel, hizo zote ni tetesi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema kama kuna mwanachama, mbunge au kiongozi anataka kuhama, hakuna haja ya kuandika kwenye mitandao, aondoke tu.

“Tunajua kazi ya kuwa upinzani ni ngumu na inahitaji watu ambao wana ‘commitment’. Waliokuja upinzani wakifikiri kuna raha, lazima watashindwa kuendelea kuishi huku.

“Tunaamini kujenga chama cha siasa ni sawa na safari, wako watakaoshuka njiani na wengine watapanda, watu wataendelea kushuka kwa sababu wengine ndio wamefika na wengine wataendelea kuingia na tutakwenda nao hadi mwisho wa safari yetu.

“Mtu ambaye anajua anachopigania, tunaamini hawezi kutoka kwenye chama, lakini yule ambaye alikuja na kutaka fursa anaweza kutoka wakati wowote,” alisema.

 

 

RUZUKU

Katika hatua nyingine, mtu mmoja anayedai kuwa ni mwanachama wa Chadema, Mackdeo Shilinde, amemwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), afanye ukaguzi maalumu katika chama hicho kuhusu fedha za ruzuku na matumizi yake.

Katika barua yake ambayo MTANZANIA imefanikiwa kuiona, Shilinde alisema kuna manung’uniko miongoni mwa wanachama kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku na kudai kuwa viongozi wa kitaifa na kanda mbalimbali za chama hulipana mishahara minono na posho zisizozingatia mgawanyo rasmi.

“Mimi na wanachama wenzangu kutoka mikoa zaidi ya 12, tumekubaliana kutafuta ukweli wa matumizi hayo ya fedha za ruzuku kwa kutumia njia halali za kisheria.

“CAG ndio taasisi yenye mamlaka ya kufanya ukaguzi wa kimahesabu, hasa katika fedha zinazotokana na umma,” alisema Shilinde.

MTANZANIA ilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kujua kama amepokea malalamiko hayo, lakini alijibu kuwa yuko nje ya ofisi.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, Mrema, alisema hizo ni siasa za kuchafuana na wala hakuna mtu ambaye anakidai chama hicho Sh bilioni saba.

“Tamko tumeliona, lakini huyo aliyeliandika hatumfahamu kama ni mwanachama wetu, hajaandika hata namba yake ya kadi. Lakini hata kama angekuwa ni mwanachama, lazima aelewe kwamba vyama vyote vya siasa huwa vinakaguliwa na CAG,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles