25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MTIFUANO WABUNGE, MAKONDA


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM     |

NI mtifuano. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wabunge kupinga kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ya kukusanya watoto na wanawake waliotelekezwa na kudai inavunja sheria.

Pamoja na hoja hizo, tayari Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na mwenzake wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, nao walikosoa kampeni hiyo kutokana na kukosekana kwa faragha.

Licha ya hoja hizo, jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwajibu wabunge na kusema haogopi na yupo tayari kufungwa kwa kutetea haki za watoto.

Katika mjadala ulioibuka juzi jioni wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi kupitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, aliyeanza kuibua hoja hiyo, alikuwa Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), aliyesema kampeni ya Makonda imevunja Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

“Zoezi lilikuwa linaendeshwa kwa kamera, ilivunja pia Katiba, Naibu Waziri (Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile) alisema hapendi zoezi linavyoendelea, naomba ufafanuzi, bila hivyo nashika shilingi,” alisema Mlinga.

PROFESA KABUDI

Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Profesa Kabudi kutoa ufafanuzi.

“Suala la nani ni baba wa mtoto ni muhimu kwa sababu mbalimbali, moja mtu angependa kumfahamu baba yake ni nani, suala hilo ni tatizo kubwa zaidi kwa nchi za magharibi, lakini tulikuwa hatuhangaiki sana suala la baba mzazi.

“Kitu ambacho hawajui ni kuwa watoto ni mali ya taifa, kwahiyo zoezi zima lililokuwa likiendelea Dar es Salaam, limekuwa na msukumo huo na katika msukumo wa aina yoyote ile ya kampeni, linakuwa na udharura, kazi ya waliopewa kusimamia zoezi hilo ni kusimamia sheria.

“Nimpongeze sana Waziri wa Afya, alizungumza mbele ya Makamu wa Rais kwamba jambo hili linahitaji faragha na vyombo vya habari vilieleza, Naibu Waziri wa Afya naye ‘ali-tweet’ kueleza.

“Lengo zima ilikuwa kuhakikisha jambo hilo la kampeni ambalo ningeshauri Watanzania tusipende sana kuiga mila zaMagharibi za kung’ang’ania kuwa wewe ni baba mzazi, badala yake tukubali kuwa baba walezi, lakini tukiendelea na kampeni za namna hii zina matatizo,” alisema.

GOODLUCK MLINGA

Pamoja na maelezo hayo ya Waziri Kabudi, Mbunge Mlinga alisema: “Naomba niseme kitu kimoja, madhara ya hili jambo ni makubwa, Sheria ya mtoto hii ukiivunja faini yake ni milioni tatu mpaka 15, wakinamama walioenda pale ni 17,000. Ukizidisha na shilingi milioni 15,000 kama wakishtaki, hapo hatujapata Bombardier tatu?” alihoji.

Alisema pia kulifanyika udhalilishaji wa mihimili mingine, ikiwamo Bunge kwa kutaja wabunge 45 wakati hata kama wabunge hao walifanya hivyo, walikuwa hawajavaa mwamvuli wa Bunge.

Baada ya Mlinga kutoa hoja, suala hilo lilichangiwa na baadhi ya wabunge.

MARIAM MSABAHA

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), alisema kilichofanywa na mama wa watoto hao ni starehe zao, sasa iweje waende kudhalilisha watu mbele ya hadhara na kudhalilisha watoto wao?

“Wengine walisema ni watoto wa viongozi wakubwa, alafu baadaye wakaja kukataa waliyosema na kuomba radhi, sasa wale viongozi waliodhalilishwa wataweka wapi nyuso zao?” alihoji.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=7HFqjrO2_S4[/embedyt]

JOSEPH MUSUKUMA

Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), alisema: “Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nyingi nzuri wanazofanya, naona tunakoelekea tunaenda kutokuwa na wakuu wa mikoa kwa sababu mawaziri, waziri mkuu na rais wanafanya kazi mpaka wakuu wa mikoa wanakosa kazi wanaanza kushughulika na hizi kazi (kukusanya kina mama waliotelekezwa na watoto).

“Lakini mimi nilitaka kujua, kwamba wako watu tunawafahamu, hawajapata bahati ya mtoto, baba na mama imeshindikana kupata watoto, wakaenda kupandikiza ikashindikana kwa sababu labda mayai yanafanana, sasa baada ya kushindikana ikabidi mama akanunue mayai hospitali, sasa huyu mtoto atakapozaliwa naye ataitwa pale ili baba yake aje amtunze?” alisema na kuhoji Musukuma.

KASUKU BILAGO

Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema ni vyema Makonda akachukuliwa hatua kwa sababu amedhalilisha na familia kuwa shakani kuvunjika.

“Huwa najiuliza mara nyngi sana, huyu Makonda anapata wapi huu ujasiri, imefika hatua tunapigiwa simu huko familia zinataka kupasuka,” alisema.

WAZIRI UMMY

Kwa upande wa Waziri, Ummy, alisema: “Zoezi ambalo limekuwa likiendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lilikuwa halali kwa sababu Sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, inatoa mamlaka kwa ofisa ustawi wa jami kusimamia masuala ya mtoto.

“Sheria imekasimu madaraka kwa maofisa ustawi wa jamii wa halmashauri na mikoa ambao wako ndani ya ofisi ya RC Makonda, zoezi lile liliendeshwa na maofisa ustawi wa jamii.

“Kama alivyosema Waziri wa Katiba na Sheria, kasoro iliyojitokeza ilikuwa suala la faragha, hasa kulinda haki ya mtoto, baada ya kutoa tahadhari ile sasa hivi tumeona zoezi lile likiendeshwa bila kuwaonyesha watoto, kwa kiasi fulani zoezi lile ni halali.

“Naomba Mlinga arudishe shilingi kwa sababu marekebisho yalifanywa baada ya tahadhari ile.”

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=LjqcEm3pZO8[/embedyt]

 RC MAKONDA

Jana, Makonda alisema wale wote wanaosema kampeni yake ya kuwasaidia akina mama waliotelekezwa na watoto imevunja sheria, pengine wana watoto nje na wanaogopa kujitokeza.

Hayo aliyasema katika uzinduzi wa hospitali ya kisasa ya mama na mtoto iliyopo Chanika, iliyojengwa kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Kimataida la Korea (Koica).

“Eti wanasema navunja sheria, natakiwa nifanye faragha, kama unataka faragha tunza mtoto.

“Mimi siogopi, nipo tayari kufungwa, lakini kwa ajili ya kutetea haki za watoto. Pengine hao wanaosema navunja sheria wana watoto wao nje, wanaogopa kujitokeza,” alisema.

Alisema hivi karibuni Ustawi wa Jamii wamefanya utafiti na kubaini kuna watoto zaidi ya 5,000 katika Jiji la Dar es Salaam, ambao wanarandaranda mitaani bila baba wala mama.

“Achilia mbali mimba zilizotolewa, achilia mbali watoto wachanga waliotupwa kwenye majalala na wengine wakaokotwa kama nyama. Achilia mbali kina mama wanaoteseka usiku na mchana kutafuta matibabu, ambao hawana gharama za kulipia.

“Tunajenga taifa linalotengeneza mashoga, ombaomba na hata watu kuteketea kwa magonjwa ya Ukimwi kwa sababu ya kina baba mnaotelekeza watoto.

“Nawasikia sikia tu wanapiga kelele, ohoo Makonda kavunja sheria, ohoo hakuna faragha, wewe ungetaka faragha ungetunza mwanao,” alisema Makonda.

Alisema watoto waliokuwa hawatambuliki, sasa baba zao wamethibitisha na wanatoa fedha za matumizi.

“Niko tayari kufungwa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoteseka mitaani, sasa hunitishi,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles