22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

ACT YATAKA BUNGE LICHUNGUZE TRILIONI 1.5/-

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


CHAMA cha ACT- Wazalendo kimemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutaka uchunguzi maalumu ufanyike kuhusu Sh trilioni 1.5 ambazo hazijulikani zimetumikaje.

Kimesema uchambuzi wao juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uliibua masuala 48, lakini waliamua kuyaainisha manane ya hatari kwa sababu ya unyeti wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema wamemwomba Spika atoe kibali maalumu kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imwagize CAG kufanya ukaguzi huo.

“Tunatarajia kuwa Spika atazingatia ombi letu kwa sababu ya unyeti wa suala hili kwa nchi yetu. Tunatoa wito kwa Watanzania na vyama vyote vya siasa tuungane pamoja kupaza sauti juu ya jambo hili,” alisema Shaibu.

Alisema fedha hizo ni nyingi kwa sababu  zingeweza kutumika kukopesha Sh milioni 100 kwa kila kijiji katika vijiji 15,000 nchi nzima, kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na kinamama, zingeweza kujenga hospitali 10 na kuwasomesha bure vijana vyuoni, wanaoomba mikopo kwa miaka minne mfululizo.

Kuhusu hoja zilizotolewa juzi kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, chama hicho kilidai zilijaa upotoshwaji na kuwahadaa Watanzania juu ya fedha hizo.

Alisema ukaguzi wa CAG ulihusu fedha zilizokusanywa na si mapato ghafi wala fedha tarajiwa.

“CAG ameonyesha kuwa Serikali iliweza kukusanya Sh trilioni 25.3 kutoka vyanzo mbalimbali, kwa ushahidi huo utaona hakuna fedha ghafi kama anavyodai Polepole, bali alikagua fedha ambazo Serikali imeshazikusanya,” alisema Shaibu.

Alisema pia hakuna fedha za Serikali ya Zanzibar na kwamba kama zingekuwapo zingeripotiwa.

“Kama kuna fedha za Zanzibar, Serikali ilikuwa na miezi mitatu ya kuzionyesha (Julai – Septemba, 2017) na ilipata wasaa wa kukutana na CAG kwenye kikao cha kujadili hoja alizoziibua Januari mwaka huu.

“Nyakati zote hizo Serikali imeonyesha namna ilivyokusanya Sh trilioni 25.3 kwa uwazi na hakuna mahali imesema kuwa kuna fedha za Zanzibar. Je, Mwenezi wa CCM anapingana na Serikali yake?” alihoji.

Katibu huyo alisema uchambuzi wa ripoti za CAG hauna uhusiano na udogo au ukubwa wa chama cha siasa, bali kinachohitajika ni weledi, ujuzi na uzoefu.

“Mwenezi (Polepole), ameeleza kwamba ACT ni chama kidogo, hakina uwezo wa kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, hoja hii ni dhaifu na ni dhihaka ya kututoa kwenye mstari,” alisema Shaibu.

Alisema kiongozi wa chama hicho, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ana ujuzi wa kutosha juu ya masuala ya uchumi na ukaguzi kutoka kwenye vyuo ndani na nje ya nchi, na kwamba ana uzoefu wa miaka minane wa kuchambua ripoti za CAG kwa sababu ameongoza kamati za Bunge za PAC na POAC kwa miaka hiyo.

Juzi, CCM kupitia kwa Katibu Mwenezi wake, Polepole, ilivunja ukimya na kutaka kukamatwa kwa Zitto.

Uamuzi huo wa CCM unatokana na taarifa ya uchambuzi wa Zitto kuhusu ripoti hiyo.

Katika uchambuzi wake, Zitto alihoji zilipo Sh trilioni 1.5, ambazo alidai hazijulikani zilipo huku pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikitangaza mapato yasiyo yake.

Polepole, alisema katika uchambuzi na taarifa ya Zitto, amepotosha umma na akataka vyombo vya ulinzi na usalama kumchukulia hatua.

Wakati Polepole akisema hayo, Zitto alisema yupo tayari kukamatwa na hata kuuawa kwa kusema hivyo, kwa sababu  mawazo yake hayatakufa.

Licha ya kauli hiyo ya Zitto, Polepole, alisema viongozi wa vyama vya siasa wanapotosha ripoti hiyo na inafaa iwekwe utaratibu waanze kuchukuliwa hatua za sheria dhidi yao.

Alisema Zitto ndiye anaongoza kupotosha ripoti ya CAG kwa kukurupuka na ripoti asizozielewa na kusema taarifa hiyo walikuwa wamekwisha kuipitia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles