NA CHRISTIAN BWAYA
UTAMADUNI wetu umetujengea matarajio makubwa kwa mwanamume. Tangu mtoto wa kiume anapozaliwa, jamii inamtegemea aoneshe tofauti yake na mwenzake wa kike.
Kazi atakazopewa, kwa mfano, kwa kawaida zitakuwa ni zile zinazohitaji nguvu, kuonesha ustahimilivu na ushujaa. Inapotokea amekutana na hali ya kukatisha tamaa, akaonesha huzuni au akalia, jamii itamkejeli. Mtoto huyu ataambiwa aache mambo ya kike.
Ufahamu wake unajengwa kuamini kuwa kuonesha hisia ni udhaifu. Hata hivyo, imani hizi zilikuwa na sababu ya msingi. Jamii zetu zilihitaji mashujaa wanaoweza kulinda jamii. Ushujaa ukaonekana lazima uambatane na ubabe, ukorofi, kutokuonesha hisia na umwamba. Huyo ndiye mwanamume aliyehitajiwa na jamii.Â
Kadri anavyoendelea kukua ndivyo anavyokabiliwa na majukumu. Umri wa kuanza kujenga ukaribu na wanawake unafika.
Kazi ya kuanzisha mapenzi inamhusu. Yeye kama shujaa, lazima ajifunze kujenga ushawishi kwa mwanamke. Mwanamume, kwa mfano, ndiye atakayepambana kuhakikisha ‘mtoto wa watu’ anamwamini na kumkubali.
Haya ni mapambano ya kujitahidi kupenda hata kama kimsingi anatamani tu. Bidii hizi zikilipa hatimaye mwanamume huyu anakubaliwa. Mwanamke anaumimina moyo wake kwake akiamini sasa amepata mtu wa kumlinda, kumfanya ajisikie salama na kubwa zaidi kumpenda kama tamthilia za ki-Filipino zinavyomwaminisha. Â
Kupenda tu haitoshi. Kwa wanawake wengi, kwa mfano, kupata mpenzi kunabeba tafsiri sawa na kupata ajira mpya.
Najizuia kucheka. Kuanzia hapo mwanamume ndiye atakuwa mfadhili wa kuwezesha maisha ya mwanamke yaendelee. Ndiye atakayenunua muda wa maongezi; kulipia gharama za saluni; kodi ya nyumba; mitoko na kila aina ya mahitaji kulingana na mtindo wa maisha aliouchagua mwanamke.
Hata pale mwanamke anapokuwa na kipato, bado mwanamume ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha maisha ya mwanamke yanafadhiliwa. Taratibu za kufunga ndoa zitakapoanza, mwanamume ndiye anayefanya mipango yote. Mahari atalipa yeye.
Harusi nayo, katika jamii zetu nyingi, hilo ni jukumu lake. Haya ndiyo yanayochangia vijana wengi wa kiume siku hizi kuogopa kuoa. Ingawa ni kweli wakati mwingine wasiwasi wao ni kutokutabirika kwa tabia za mwanamke, lakini mara nyingi, hofu kubwa inatokana na majukumu yanayoambatana na familia.Â
Akishaingia kwenye ndoa, kazi ya kuonesha naye ana akili za maendeleo inaanza. Kama alikuwa hajajenga, sasa ana shinikizo la kupambana kufa kupona ahamie kwake. Kama alikuwa hana usafiri, inabidi apambane awe na usafiri wake. Mungu akiwajali watoto, shule nazo zinaanza kudai ada.
Familia tandaa nazo hizi hapa. Jukumu la kuwatunza wakwe zake na familia yake mwenyewe hawezi kulikwepa. Haya yote yanaanza kula muda wake. Kipato hakitoshi. Ndoto zake zinaanza kugeuka kuwa ndoto kweli. Huu ndio wakati ambao yale matumaini yake alipokuwa kijana yanaanza kufifia. Kichwa cha mwanaume kinajazwa mambo mengi.Â
Mkusanyiko wote huu unatengeneza sonona ya ndani kwa ndani ambayo, wakati mwingine, inaweza kuathiri urijali wake. Muda wa kufikiri mahaba na mapenzi haupo kwa sababu kichwa kinaumizwa na maswali yasiyo na majibu. Kafundishwa kwamba mwanamume wa kweli hasemi semi shida zake kwa mke wake.
Kaaminishwa kumshirikisha mke kila kitu kinachokusumbua huo ni udhaifu. Ingawa anakutana na wanaume wengi, kimsingi hana rafiki anayeweza kumwambia masuala halisi. Moyo wake unajaa mambo mengi yanayomsumbua ingawa kwa nje, lazima aoneshe kuwa yeye ni mtu ngangari.Â
Kama ni mcha Mungu, huu ndio muda wa sala na ibada. Tafiti zinaonesha kuwa wanamume wanaoamua kukimbilia ibadani wanakuwa salama.
Huko wanakutana na mazingira yanayowaweka karibu na watu wenye matumaini.
Lakini kama ataamua kutafuta faraja kwa watu, uwezekano ni mkubwa akaanza kutumia muda mwingi akilewa. Huko ndiko atajifunza kuwa pombe zinaweza kukusahaulisha matatizo. Kuchelewa kurudi nyumbani kunaanza kulipa kwa sababu anaepuka ‘makelele’ ya mke wake. Kwa upande mwingine, mke wake naye anaanza kushindwa kuelewa.
Inakuwaje mwanamume aliyewahi kutumia muda mwingi kumpenda, leo amekuwa mgomvi, mnyanyasaji, asiyejali? Malalamiko haya yana ukweli ndani yake. Mwanamke ameanza kujihisi kama mtu asiyependwa tena, aliyetelekezwa, asiye na mwenyewe.
Moyo wake unakata tamaa lakini hajaweza kuelewa kile hasa kinachoendelea kwenye maisha ya siri ya mume wake. Kwa mwanamke unayesoma hapa, hoja yangu ni kwamba wakati mwingine mume wako anapitia mambo mengi kimya kimya.
Kikubwa anachokihitaji kwako ni kumtia moyo, kutambua juhudi anazofanya na angalau kumfanya aamini wewe ndiye mwandani wake. Badala ya kumlalamikia, kumkosoa, kumhukumu na kumdhalilisha, mume wako anahitaji angalau uelewe kuwa anapambana kukulinda.Â