24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Aliyoyafanya JPM miaka minne ndani ya Ikulu

Na Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es salaam

SERIKALI ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, imefanikiwa kutimiza ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi wakati wa kampeni za urais, mwaka 2015, na wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Novemba 2015.

Rais alihutubia Bunge kwa mujibu wa matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91, ibara ndogo ya kwanza inayomtaka rais aliyechaguliwa kufungua rasmi Bunge hilo.

Akihutubia bungeni, Rais Magufuli aliwaambia wabunge kuwa wananchi waliwachagua wakiwa na matarajio makubwa na watawapima kwa namna watakavyokidhi kiu na matarajio yao.

“Wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi cha awamu ya tano ambapo matarajio yao ni makubwa, sote tuliahidi kuwatumikia na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali  na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Mimi na Samia (Makamu wa Rais) tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na kuhakikisha kuwa katika utumishi wetu, tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida.” 

Ni dhahiri uchapakazi wake umeonyesha mabadiliko makubwa ya kiutendaji, tumeshuhudia Rais akifanya mikutano mbalimbali na viongozi kuanzia ngazi ya mawaziri hadi watendaji wa kata Tanzania Bara na kuzungumza nao masuala mbalimbali ya kiuongozi ikiwamo wajibu wao kwa wananchi.

Mkutano kati ya Rais na watendaji wa kata ni mwendelezo wa mikutano yake na watendaji wa serikali wakiwamo wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya, makatibu tawala wilaya na makatibu watendaji wa tarafa.

Akizungumza na makatibu watendaji wa tarafa Rais alisema: “Ninyi ni wawakilishi wangu ngazi ya kata, tunapozungumzia mafanikio ya Serikali, ninyi ndio wasimamizi wa mwanzo wa mafanikio hayo.”

Hatua ya Rais kuwaita watendaji hao wa tarafa kutoka Tanzania Bara na kuzungumza nao, ni kitendo kinachoonyesha jinsi anavyowajali viongozi wote kuanzia ngazi ya chini hadi juu. Pia kinachoonyesha kuwa uongozi wa chini ukifanya kazi vizuri utawezesha hata uongozi wa juu kutenda kazi kwa ufanisi na yenye tija kwa Taifa na wananchi kwa ujumla.

Katika bunge hilo, pia aliahidi kusimamia matumizi ya mali za umma na rasilimali za Taifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu zinatumika kwa manufaa ya umma na si mtu binafsi. Aidha, kuhakikisha kuwa ugawaji wa rasilimali hizo unafanyika kwa haki.

Katika siku za mwanzo za utawala wake, alianza kwa kufanya ufuatiliaji wa rasilimali zetu ambapo aliunda kamati maalum ya kuchunguza mchanga na madini yaliyokuwa yanasafirishwa nje ya nchi. Kamati hiyo ilionyesha upotevu mkubwa wa mapato na rasilimali za nchi ambapo nchi ilikuwa inapoteza kiasi cha bilioni 829.4 hadi trilioni 1.439 kwa kusafirisha mchanga nje ya nchi.

Ili kuhakikisha anazuia upotevu huo, kamati ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo Rais aliyakubali. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni usitishwaji wa  usafirishaji wa mchanga huo hadi mrabaha stahiki utakapolipwa, na kujengwa kwa vinu vya kuchakata madini yote ili yaweze kufahamika na kutozwa kodi.

Aidha, Rais aliwaagiza wakuu wa mikoa inayozalisha madini kuanzisha masoko ya madini ili kudhibiti utoroshaji na uuzaji holela wa madini. Hadi sasa baadhi ya  masoko yamekwisha anzishwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Dar es Salaam, Mtwara, Manyara, Morogoro, Kagera na Arusha. Kwa upande wa wilaya masoko hayo yamefunguliwa Simanjiro na Chunya.

Ufunguzi wa masoko hayo umeleta neema si kwa Serikali tu bali hata kwa wauzaji wa madini hayo ambao walikuwa wakiyauza kwa kudhulumiwa na wanunuzi wakubwa. Kwa Serikali na nchi kwa ujumla masoko haya yameongeza pato la taifa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la upatikanaji wa madini.

Eneo lingine ambalo Rais aliahidi kulishughulikia ni kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma. Katika kutimiza ahadi yake kwa upande wa kusimamia mapato tumeshuhudia Rais akifanya mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzindua kituo kikuu cha Taifa cha kuhifadhi mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ambapo makusanyo ya Septemba 2019 yalikuwa trilioni 1.7 sawa na asilimia 97.20 kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa na mamlaka hiyo tangu kuanzishwa kwake Julai mosi, 1996. 

Ni dhamira ya TRA kukusanya mapato kwa utaratibu rahisi na wa wazi na walipakodi watapata urahisi wa kupata huduma zinazotolewa kwa wakati.  Matokeo ya kuongezeka kwa ukubalifu yatadhihirika kwa kuongezeka kwa mapato kwa ajili ya Serikali kutoa huduma za jamii zinasostahiki na kwa ubora. Hii itaifanya jamii ya walipakodi kufurahia manufaa ya kijamii na kiuchumi kutokana na kodi wanazolipa katika kuboresha hali ya maisha.

Kituo hiki ni mashirikiano ya pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), ambacho kimeundwa ili kusaidia kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali zote mbili.

Akizindua kituo hicho Rais alizitaka taasisi mbalimbali zikiwamo za Serikali, kampuni na benki kujisajili katika kituo hicho ili kuweza kukusanya kodi kwa ufanisi. ‘Kituo hicho ni muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya nchi ili kulinda usalama wa taifa, taasisi za serikali na kampuni binafsi zinazoendesha shughuli zake nchini na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo,” alisema Rais Magufuli.  

Katika kuhakikisha kuwa Serikali inakuwa kinara wa utawala bora, aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi. Awali akihutubia Bunge la kwanza, aliwaambia wabunge kuwa mojawapo ya maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi wakati wa kipindi cha kampeni ni rushwa ambapo sehemu nyingi wananchi walisema kuwa rushwa ni mojawapo ya kero kubwa wanazokumbana nazo.

Baadhi ya mafanikio ya mapambano ya vita dhidi ya rushwa ni pamoja na kuanzishwa kwa ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Hadi ngazi za wilaya. Pia Serikali hii inajipambanua kwa uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa umma, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu rushwa na madhara yake.

Katika mkutano wa 32 wa wakuu wa nchi za Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwaka 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika ufuatiliaji na utekelezaji wa mapambano dhidi ya rushwa.

Taasisi ya Transparency International imesifu juhudi za Rais Dk. Magufuli na kuitaja Tanzania kuwa ni  nchi ya pili kwa kupunguza rushwa  na kufanikiwa kuifanyia kazi mianya mingi ya rushwa. 

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP. Diwani Athuman alisema kuwa utafiti uliofanywa na taasisi za kimataifa za Transparency International na Afro Barometer inayoitwa Global Corruption Barometer Africa 2019, alisema kuwa Tanzania ni ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika katika kipengele cha juhudi za serikali katika kupambana na rushwa kwa mwaka 2019. 

Aliongeza kuwa Tanzania imefanya vizuri katika maeneo mawili ambayo ni utendaji mzuri wa Serikali na kukuza imani kwa wananchi dhidi ya Serikali yao na jitihada za kupambana na rushwa.

Kuhusu kero ya migogoro ya ardhi, Serikali imefuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekeri 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na kuyagawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji, na misitu saba yenye ukubwa wa  ekari 46,715 kurudi kwa wananchi.

Hatua hii ilifuatiwa na kubaini uwapo wa vijiji 975 vyenye migogoro, ambapo iliamuliwa kuwa vijiji 920 vibaki ndani ya hifadhi na mipaka irejerewe upya na kupatiwa vibali vya ardhi vya kijiji. Pia serikali iliridhia kumega misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.

Ahadi nyingine ambazo Rais amezitimiza ni katika sekta ya afya na elimu ambapo katika elimu aliahidi elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Kutokana na utekelezaji wa ahadi hiyo, kumekuwapo mwamko mkubwa wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza shule ya msingi ambao idadi yao imefikia 1,670,919 mwaka 2019 kutoka 896,584 mwaka 2016. Kwa upande wa shule za sekondari idadi ya wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka 2019 ni 710,436 kutoka wanafunzi 238,365 walioandikishwa mwaka 2016 wakati sera ya elimu bure ilipoanza kutekelezwa nchini. 

Katika sekta ya elimu pia tumeshuhudia maboresho mbalimbali ambapo vifaa vya kufundishia na kujifunzia vimeongezwa, michango isiyo ya lazima imeondolewa, kuongezewa madawati na kujengwa kwa nyumba za walimu.

Aidha, katika eneo la afya, dhamira ya Rais kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umaskini amelipa msukumo wenye tija ili kuwa na wananchi wenye afya bora. Tumeshuhudia uboreshaji wa sekta hii ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Lengo likiwa ni kuwaondolea usumbufu wananchi na kutolazimika kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi. 

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa awamu ya tano, tumeshuhudia mafanikio mengi katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, miundombinu, nishati na madini, ikiwa ni kutimiza ahadi ambazo ziliahidiwa na Rais wakati anaingia madarakani. Maendeleo yote haya yamewagusa wananchi kwa kiasi kikubwa kwa sababu yameweza kutatua kero nyingi walizokuwa nazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles