21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Kinondoni waongoza ukaidi uvaaji helmet

Na CHRISTINA GAULUHANGA

LICHA ya harakati zinazofanywa kwa ushirika wa wadau na serikali katika kuihamasisha jamii kuvaa kofia ngumu (helmet) pindi watumiapo usafiri wa bodaboda kwa usalama wao, bado raia wengi wanapuuza.

Ifahamike kuwa matumizi sahihi ya helmet hupunguza madhara ya majeraha na uwezekano wa kufariki kwa dereva na abiria pindi ajali inapotokea. 

Akifafanua umuhimu wa helmet kwa wasafiri wa bodaboda, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Asasi ya Ushauri ya Vaccine Helmet, Alphero Nchimbi, anasema huepusha sehemu ya kichwa kugongana moja kwa moja na sehemu ambayo abiria au dereva atagonga iwe kwenye chombo, ardhi au barabara ya lami. 

Anasema badala ya kichwa kugonga sehemu hiyo helmet iliyovaliwa ndio itagonga kwanza.

Anasema: “Muundo wa helmet unasaidia kuzuia madhara katika ubongo hasa ajali ikitokea kwa kuwa kuna sponji na muundo mzuri inayozuia kichwa kuumia.”

Lakini licha ya umuhimu wake huo, bado baadhi ya wanajamii wamekuwa hawabadilishi mtazamo wao katika matumizi ya helmet hizo licha ya hata ya kuelimishwa faida zake.

Uvaaji wa helmet unapokewa kwa mitazamo tofauti, wapo wanaoona kuwa kuvalia helmet ni kero huku wengine hawajui hata njia bora ya uvaaji.

Nafasi ya polisi kuhakikisha zinavaliwa

MTANZANIA limezungumza na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salam, ZTO, Marisson Mwakyoma ili kufahamu hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na wasiotii kanuni ya uvaaji wa helmet hasa zile zinazokidhi kiwango kilichowekwa na Shirika la ViwangoTanzania (TBS). TZS 1478:2013.

Anasema hadi sasa makosa 5,027 kuhusiana na matumizi ya kofia ngumu (helmet) kwa watumiaji wa usafiri wa pikipiki (bodaboda) yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polis mkoani Dar es Salaam kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.

Mwakyoma anasema kwa kipindi kinachoanzia Januari hadi Juni mwaka huu, kikosi cha usalama barabarani Dar es Salaam kimekamata idadi ya makosa hayo 5,027 huku Mkoa wa kipolisi Kinondoni ukitajwa kuongoza kwa makosa hayo.

Anasema kuwa sababu kubwa ni ukubwa wa mkoa huo wa kipolisi ambapo una miundombinu nyingi za barabara zinazowawezesha watumiaji wa bodaboda kutumia kwa wingi huku wengine wakipuuzia matumizi ya kofia hizo.

Anasema: “Jeshi la Polisi limekuwa likiendelea mara kwa mara kuwaelimisha watumiaji wa huduma za usafiri wa bodaboda kuhusiana na umuhimu wa kuvalia kofia ngumu, lakini bado kumekuwapo changamoto kadhaa zinazochangia watumiaji hao kukaidi.

Sababu kubwa ni kwamba baadhi ya watumiaji wana kiburi cha kudharau matumizi ya kofia hizo ngumu lakini waendesha bodaboda wengine hawana kofia hizo hivyo, abiria wanakosa za kuvaa, pia kukosekana kwa hamasa kati ya wenye bodaboda kuhusiana na umuhimu wa kuvaa kofia ngumu.

Anasema kati ya makosa hayo wapo waliotozwa faini na kuachiwa huku wengine wakishikiliwa kwa muda vituoni ikiwa ni sehemu ya adhabu na wengine wamechukuliwa hatua kadhaa.

Anaongeza kuwa polisi Dar es Salaam wanaendelea kutoa elimu na kuwachukulia hatua kali za kisheria watumiaji wa usafiri huo ambao wamekuwa wakikiuka taratibu na kanuni za matumizi ya helmet hizo na kuhatarisha usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Mwongozo wa kimataifa usalama barabarani

Gazeti hili limefuatilia wwongozo uliotolewa na Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na ajali za barabarani wa mwaka 2011 hadi 2020 na kubaini kati ya mambo yaliyogusiwa kwenye nguzo namba nne kati ya nguzo tano za Umoja wa Mataifa zinazotoa mwongozo wa kuzikabili ajali za barabarani ni umuhimu wa uvaaji wa kofia ngumu kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa pikipiki.

Nguzo hiyo ambayo kwa ujumla inagusia suala zima la matumizi sahihi na salama ya barabara, imegusia umuhimu wa kuongezeka kwa matumizi ya sheria na viwango husika vya helmet huku pia ikigusia umuhimu wa utolewaji wa elimu na kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya matumizi ya helmet.

Mambo mengine yaliyogusiwa ni ufungaji wa mikanda, kupunguza unywaji wa pombe wakati wa kuendesha vyombo vya moto na mwendokasi.

Nguzo namba moja ni usimamizi wa masuala ya usalama barabarani ambapo kati ya mambo yaliyopo kwenye nguzo hiyo ni uwapo wa sheria inayoendana na matakwa hasa ya kimataifa.

Upungufu Sheria ya Usalama Barabarani

Gazeti hili pia limefuatilia matakwa ya kisheria kwenye sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 na kubaini upungufu kadhaa ambapo sheria hiyo imemtaja dereva kuwa ndio mtu anayepaswa kuvalia helmeti hiyo huku abiria akionekana ni kama mtu asiyeguswa kutakiwa kisheria kuvaa helmet.

Ila kinachofanywa na askari hao wakiwakamata ni kufuata kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) inayotoa adhabu ya Sh 30,000 kwa dereva wa bodaboda atakayekamatwa akiendesha bila ya kuvalia helmet na abiria atakayepanda pia bila ya kuvalia kofia.

Mapendekezo

Imependekezwa kuwa sheria itamke rasmi kukubali viwango vya helmet vilivyowekwa na Shirika la ViwangoTanzania (TBS) kutambua kiwango cha TZS 1478:2013 kuwa ndio kiwango cha kufuatwa na waagizaji wa helmet nchini.

Pia wameshauri kutungwa kwa sheria za kuwabana watumiaji wa usafiri huo wasiovalia kofia ambapo kati ya mapendekezo yao ni kuwepo kwa hatua kali zaidi za kuwachukulia watakaokamatwa kutovaa  helmet wakituia bodaboda.

Waendesha bodaboda

Akizungumzia suala hilo, mwendesha bodaboda wa Kawe, Juma Handunga, anasema kunahitajika abiria kuelimishwa zaidi kuhusiana na matumizi ya kofia ngumu kwa sababu wapo ambao wanakataa kuzivaa hata wakisisitizwa kufanya hivyo.

Aliongeza: “Kuna wakati tunakamatwa na polisi kwa kosa la abiria kutovalia helmet na wakati mwingine wanakamatwa abiria wenyewe kwa kosa la kukaidi kuvaa helmet na hii inatokea zaidi iwapo kama askari wakibainisha kuwa bodaboda tunazo.”

Naye abiria mmoja aliyezungumza na gazeti hili, Mwajuma Rajabu, anasema kuna haja ya kutolewa kwa elimu zaidi ya matumizi ya kofia hizo kwa sababu kuna wakati abiria wanazivaa kwa woga wa kukamatwa na askari na sio kutokana na umuhimu wake. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles