22.6 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

Mtandao wa TikTok unavyompa umaarufu mchekeshaji MC Raji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MTANDAO wa TikTok umeendelea kujizolea mashabiki na watumiaji lukuki kadri siku zinavyokwenda hasa katika upande wa sanaa za muziki na ucheshi.

Mastaa wakubwa wa muziki huwatumia watu maarufu kwenye TikTok kutangaza nyimbo zao yaani kwa ufupi ukiona wimbo wako ume-trend TikTok basi ujue tayari umeliteka soko.

Miongoni mwa watu maarufu kwenye mtandao wa TikTok ni mchekeshaji wima (stand up comedian), MC RAJI, mkongomani anayeishi nchini Marekani na amejizolea umaarufu mkubwa kwa vituko vyake ndani na nje ya jukwaa la TikTok.

MC Raji a.k.a Nonsense Abracadabra mwenye wafuasi zaidi ya milioni moja katika mtandao wa TikTok, amejiwekea heshima kwenye sanaa ya uchekeshaji jukwaani na sasa hakamatiki mtandaoni.

Raji anasema TikTok imekuja kurahisisha sanaa yake kwani alianza kuchekesha kitambo kabla ya Facebook na Instagram na anaamini yeye sio mchekeshaji wa mitandaoni pekee bali anaishi uchekeshaji.

“Maisha yangu ni uchekeshaji tosha, nashukuru mashabiki ambao wamekuwa na mimi tangu enzi hizo hakuna mitandao na nilikuwa nachekesha kwenye majukwaa kwenye kumbi na katika sherehe mbalimbali ambako nilipata umaarufu mkubwa,” amesema MC Raji.

Utandawazi umemfungulia njia mpya ya mafanikio kidijitali kwasababu ana wigo mpana wa kuchekesha na kuwafikia mashabiki wa mataifa mbalimbali kupitia mitandao hasa TikTok.

“TikTok imenifungulia njia mpya ya kuchekesha ulimwengu, sasa hivi nina wafuasi milioni moja, kwahiyo naweza kuwachekesha watu wote hao kwa wakati mmoja, ni suala la kutengeneza maudhui mazuri na kuyarusha mtandaoni ili kuendelea kujenga ufalme wangu,” amesema MC Raji.

Anaongezea kwa kusema sio jambo dogo kupata wafuasi milioni moja kwenye mtandao wa TikTok, kwahiyo ukiona umefikisha idadi hiyo ya watu basi ujue kuna kitu cha ziada unafanya.

“TikTok kuna wachekeshaji wengi lakini sio wote wana wafuasi milioni moja kama mimi. Nimefanya kazi kubwa kuhakikisha kila maudhui yanayopanda TikTok yanakuwa na nguvu ya kuniongezea mashabiki ndio maana nimefanikiwa na bado naendelea,” amesema MC Raji.

Katikati ya mafanikio hayo MC Raji anaweka wazi changamoto anazokutana nazo kwenye sanaa yake ya ucheshi katika mtandao kuwa ni baadhi ya watu kuchukulia poa sanaa yake.

” Huwezi kupendwa na kila mtu, kwahiyo hata mimi naweza kutengeneza maudhui mazuri sana ya kuchekesha lakini akaibuka mtu au watu wachache, wakaponda, ni changamoto japo nimeshazoea na inaniongezea nguvu ya kusonga mbele,” amesema MC Raji.

Mchekeshaji huyo ameendelea kutanabaisha kuwa ili mchekeshaji ufanikiwe mtandaoni unapaswa kuwa mbunifu kila siku hata kama wataibuka watu watakaoponda sanaa unayofanya usikate tamaa.

“Sijawahi kukata tamaa kwenye sanaa yangu ndio maana nilianza kuchekesha kwenye majukwaa, harusi na sherehe zingine kabla ya mitandao, hivyo wachekeshaji wadogo wanatakiwa kupambana bila kukataa tamaa maana sanaa ya ucheshi ni ngumu inahitaji ujuzi na ubunifu mpya kila siku ili ufike kwenye mafanikio,” amesema MC Raji

Aidha, MC Raji ameendelea kuwakaribisha mashabiki zake kwenye mtandao wa TikTok @mcrajiofficial ili kumpa sapoti kwenye sanaa yake ambayo ndio kwanza imeanza kuchanua kupitia mitandao huo wenye nguvu kubwa duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles