31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yaweka wazi ushiriki wake katika kutekeleza ajenda ya maendeleo Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Benki ya NMB imeweka bayana ushiriki wake katika kutekeleza ajenda ya maendeleo Visiwani Zanzibar kwa kufadhili harakati za kuboresha maisha na shughuli za uzalishaji kwa njia kadhaa ikiwemo kuwekeza sehemu ya faida yake kwenye miradi ya kijamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) akipokea maelekezo kutoka kwa meneja wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Shaame (Wapili Kushoto) alipotembelea banda la NMB katika sherehe za kufunga tamasha la Kizimkazi visiwani Zanzibar. Rais aliambatana na mke wa Rais wa Zanzibar, Mariam Mwinyi, waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa na mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Khalid Rashid. Kushoto ni mkaguzi mkuu wa ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa.

Taasisi hiyo imesema mwishoni mwa juma lililopita kwenye kilele cha wiki ya Tamasha la Kizimkazi kuwa mbali na huduma bunifu za kibenki pia inachangia ustawi wa visiwa vya marashi ya karafuu kupitia mipango kama ushirika wa kibiashara na kukuza utalii.

Akizungumza kwenye hafla ya Siku ya Kizimkazi Jumamosi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la tamasha hilo ambalo alisema linazidi kukua na kuvutia watu wengi likitoa fursa za kiuchumi na maendeleo ya kijamii.

“Tunajivunia kuwa mshiriki mkubwa wa maendeleo ya hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na tunaahidi kuendelea kujitoa zaidi kwa maslahi makubwa ya taifa letu,” amesema.

Zaipuna alimwambia Mama Samia aliyekuwa mgeni rasmi na kuipongeza NMB kwa mchango wake hasa ukopeshaji wananchi wa kawaida.

Mkuu huyo wa nchi aliyeambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwachagiza Wazanzibar kuchangamkia huduma za NMB, ambayo ndiyo iliyokuwa mdhamini mkuu wa siku ya tamasha hilo, na hasa mikopo ambayo zaidi ya kutohitaji dhamana lakini pia inapatikana hadi kwa kiasi cha Sh 5,000.

“Tunajivunia zaidi uwezo wetu mkubwa na ubunifu wa kiteknolojia kutoa masuluhisho na kuwahudumia watanzania popote walipo yaani ndani na nje ya nchi,” amesema Zaipuna.

Aidha, amesema NMB imefanya makubwa katika sekta ya utalii ikiwemo kushirikiana na wadau kama ZATO na HAT ambavyo ni vyama vya waongoza watalii na wamiliki wa hoteli lengo likiwa ni kuhakikisha wageni wanapata huduma bora za kifedha.

NMB imefanikiwa katika hilo, alifafanua, na imekuwa benki ya kwanza nchini kuleta mashine za kubadilisha fedha za kigeni zinazowawezesha watalii na wananchi wengine kubadili hadi dola za Kimarekani 2,000.

Zaipuna amesema ATM hizo tayari zipo kwenye viwanja vitatu vya Kimataifa nchini ukiwemo ule wa Abeid Amani Karume.

Zaipuna amesema NMB imekuwa mdau mkubwa wa Tamasha la Kizimkazi ambalo aliahidi wataendelea kulidhamini na mshirika mkubwa wa shughuli za kijamii kwenye hasa nyanja za ujasiriamali, elimu na afya.

“Mkuu wa Mkoa tayari amebainisha vizuri mchango wetu katika hilo lakini ngoja niongeze kidogo kwa kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 268 kwa shule 32 na vituo vya afya 28 hapa visiwani Zanzibar, yaani Unguja na Pemba.

“Kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema, Royal Tour na Uchumi wa Bluu ni Chachu ya Maendeleo, NMB tayari imetekeleza programu ya mafunzo kwa wakulima wadogo na tayari tumeshatoa elimu kwa wananchi karibia 3,800 ikiwemo vikundi zaidi ya 50 vya akinamama wanaojishughulisha kwenye sekta ya uvuvi, kilimo cha mwani na chumvi pamoja na kuwakopesha,” amesema Zaipuna.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Khalid Rashid, alisema wakazi wa mkoa huo wana thamini ushiriki wa NMB kwenye maendeleo yao na benki hiyo imekuwa mdau nyeti wa maendeleo ya Zanzibar yote.

Alisema uwekezaji wake kwenye shughuli za kijamii siku za hivi karibuni ni pamoja na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 17 katika skuli ya Kizimkazi Mkunguni, visaidizi vya walemavu vya Sh milioni 10 na kutoa Sh milioni 19.9 kujenga jengo la skuli ya Ndijani.

“Pia NMB imetoa mafunzo kwa wanawake 500 na ina mpango wa kutoa mashine 50 za kukusanya mapato ya utalii na tayari vifaa hivyo 12 vinatumika kwa ajili ya majaribio. Tayari tumefanya mazungumzo nao kuona jinsi watakavyotoa mikopo ya kununua boti za uvuvi na kusafirisha watalii,” amesema Rashid.

Tamasha la Kizimkazi lilianza mwaka 2015 likijulikana kama Siku ya Samia na kubatizwa jina lake la sasa na kuwa na hadhi ya sasa hvi mwaka uliofuata ambapo limekuwa la kitaifa zaidi la kuchochea maendeleo na kukuza uchumi jumuishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles