Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka madiwani wa halmashauri zote katika mkoa huo, kutokuwa chanzo cha migogoro kwenye maeneo yao huku akipiga marufuku tabia ya kuazimia kuwafukuza wafanyakazi bila ya sababu za msingi.
Mtaka amesema kuwa hatokuwa tayari kukubali madiwani wa halmashuari yeyote kukaa kikao na kuanza kumwazimia mtumishi yeyote wa serikali awe mkurugenzi, mkuu wa aidara au kitengo na badala yake watumie njia sahihi katika kufanya uhamuzi huo.
Mkuu huo wa Mkoa ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Desemba 13, wakati wa kikao kazi kilichofanyika mjini Bariadi ambacho kiliwashirikisha madiwani wote wa mkoa mzima, viongozi wa Wilaya na halmashuari wakiwemo watumishi wa serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa ambapo kilikuwa na lengo la kuelezea mwelekeo wa mkoa kwa miaka mitano ijayo.
Amewaeleza madiwani hao kuwa na upendo kwa watumishi wao na kushirikiana nao kila wakati, na siyo kutumia nafasi yao kutaka kuwafukuza au kuwakataa wasifanye kazi kwenye halmashuari zao.
Amesema kama wataona kuna mtumishi yeyote wa serikali utendaji kazi wake siyo mzuri, washauriane kwanza na ofisi yake kupitia kwa katibu tawala wa mkoa ili kuona njia gani sahihi ya kumwajibisha mtumishi huyo.
“Mkitaka kufanya kazi vizuri wapeni heshima watumishi wa serikali, lakini kama mnakwenda kwenye baraza kuazimia mtu, hamtamtoa hilo niwaambie niko hapa mwenyewe, hakuna mtu utamwazimia umtoe, hautamwazimia mkurugenzi, mkuu wa idara wala afisa,” amesema Mtaka.
“Fanyeni kazi Kama kuna jambo kwenye halmashuari uongozi wa mkoa upo, katibu tawala yupo, Mkuu wa mkoa yupo, twambieni, tukishindwa tunapeleka TAMISEMI , vitumieni vyombo vya dola, Takukuru na wengine na siyo kuazimia,” amesema Mtaka.
Amewataka madiwani hao kwenda kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, kama ambavyo waliwahidi wakati wa kampeini na siyo kuanzisha migogoro isiyokuwa na tija huku akiwasisitiza kutambua kuwa kipaumbele cha mkoa ni elimu kwanza.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Miriam Mmbaga amewataka viongozi hao wapya wa kisiasa kutumia muda mwingi kuwatumikia wananchi, kwa kuzingatia sheria ya maadili kwa viongozi wa umma.
Nae Mkuu wa Takukuru, Joshua Msuya, akawataka viongozi hao kutojihusisha na vitendo vya rushwa, ikiwa pamoja na kuwa wasimamizi wa fedha za serikali ambazo zinapelekwa kwenye vijiji na kata