Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, ameagiza kukamatwa mara moja wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Giyuki iliyoko kata ya Nkololo Wilayani Bariadi, ambao wanadaiwa kuoana baada ya kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.
Kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa imekuja baada ya Ofisa Elimu Utamaduni wa Mkoa, Charles Maganga, kuwasilisha taarifa ya kikosi kazi kilichoundwa kuchunguza chanzo cha Mkoa wa Simiyu kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2018 kwenye kikao kilichofanyika leo mjini Bariadi.
“Kufika leo jioni wawe wamekamtwa na watasherekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya mahabusu, hili jambo siyo la kunyamazia lazima kama serikali tuchukue maamuzi, yanatusababishia kushuka kielimu,” amesema Mtaka.
Katika taarifa hiyo Maganga amesema katika shule hiyo walibaini kuwa wazazi wa wanafunzi hao walikubaliana na kutoleana posa ili watoto wao waoane na baada ya kufanya mtihani harusi ya kufunga ndoa ilifanyika kijijini hapo.
“Kwenye matokeo yao mvulana alifaulu lakini msichana hakuweza kufaulu, taratibu zote za kufanikisha jambo hilo zilifanywa na wazazi wa pande zote mbili kabla ya wanafunzi hao kufanya mtihani huo,” amesema Maganga.