27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli afuta ndoto za fidia

ELIZABETH HOMBO Na ANDREW MSECHU

RAIS Dk. John Magufuli, amehitimisha suala la kulipwa fidia kwa wakazi wa Kimara jijini Dar es Salaam waliobomolewa nyumba zao, kupishaujenzi wa barabara ya njia nane, akisema hakuna fidia itakayotolewa kwa mtu yeyote.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa barabara hiyo inayoanzia Kimara wilayani Ubungo hadi Kibaha mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema wakati mwingineni vyema watu waambiwe ukweli ili waondoke mapema kuliko kudanganywa nakupoteza muda wao.

“Fidia haipo, nasema fidia haipo, ninarudia tena mara ya tatu fidia haipo. No, fidia haipo, huo ndio ukweli, fidia haipo,”alisema RaisMagufuli kwa msisitizo.

Alisema ukweli kuhusu kutokuwapo fidia kwa wakazi hao, unatokanana kesi ya mwaka 2007  ambayo ilikuwainapinga kuvunja nyumba hizo ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo iliyokuwa ijengwe kwa msaada wa Serikali ya Denmark.

Alisema kesi hiyo namba 39 ambayo Serikali ilishinda,ilifunguliwa na Bounce & Others dhidi ya Serikali chini ya usimamizi wawataalamu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakiongozwa na Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo.

Alisema kwa wakati huo, kesi hiyo ambayo Serikali ilishinda ilikwamisha mradi huo.  Kwa mujibu waRais Magufuli mchakato wa kubomoa nyumba hizo ulianza alipokuwa waziri waujenzi.

Alisema katika kipindi cha miaka 20 aliyokuwa waziri, alitumia muda mwingi kutoa ufafanuzi kuhusu hifadhi ya barabara na utaratibu wa kutolipwa fidia kwa watu wanaojenga katika hifadhi hiyo.

“Niliwaambia tangu nikiwa naibu waziri na hadi sasa nimekuwa Rais, ukisogelea hifadhi ya barabara umekaribisha umasikini. Lakinipia ni kwamba kutokana na uamuzi wa kesi hiyo niliyoitaja ambao ulitolewaMahakama Kuu, hata uende wapi huwezi kushinda,”alisema.

Alisema suala hilo la bomoabomoa linamgusa hata yeye kwa sababu anao ndugu zake walioathirika, akiwemo mmoja aliyemtaja kwa jina la Mzee Masabila (yeye na mkewe ni marehemu kwa sasa).

Alisema ndugu zake hao, walijenga nyumba zao na wamezikwa katika eneo hilo la Kimara lakini zilibomolewa, huku wakiacha watoto watatu.

Rais Magufuli alisema kutokana na ukweli huo, ni vyema wananchi wakaheshimu sheria ili wairuhusu Serikali itekeleze miradi mikubwa kwakutoingilia maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo.

Rais Magufuli alitoa hitimisho hilo alipokuwa akijibu maombi ya Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) ambaye alimshukuru kiongozi huyo wa nchi kwa kutambua umuhimu wa kutumia kodi za wananchi katika miradi ya maendeleo.

Mnyika alisema pamoja na ujenzi wa barabara ya njia naneyenye urefu wa kilomita 19.2, ni vema Rais atafakari pia kuhusu wananchi waliobomolewa makazi yao kupisha ujenzi huo ambao hawakulipwa fidia.

“Ninakuomba mheshimiwa Rais kwa kutanguliza utu mbele, Mwalimu Julius Nyerere alisema maendeleo ya vitu lazima yaendane na maendeleo ya watu.

“Pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nane, utafakari pia kuwalipa fidia wananchi waliobomolewa kupisha ujenzi wa barabara hii,” alisema.

Alisema katika kusalimia kwake anafikisha salamu kwa niaba ya wananchi wengi waliopo kwenye uzinduzi huo, ambao wanamwomba Rais kama ambavyo aliomba Arumeru na Watanzania wamemwombea, kwamba asiwe na kiburi nakuwa wananchi hao wana malalamiko yao kuhusu bomoabomoa iliyofanyika katikaeneo hilo.

Alisema kwa kuwa demokrasia na maendeleo ni mapacha, alimwomba Rais Magufuli kutumia fursa hiyo kuzungumzia kuondoa vikwazo vinavyoikabili demokrasia nchini, kwa kuwa wanaamini kwa kufanya hivyo itasaidia nchi kusongambele zaidi kimaendeleo.

Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,  alitumia nafasi hiyo kumweleza Rais kuhusu mambo matano kutoka kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambayo anawaomba Watanzania akiwemo Rais Magufuli kuyatafakari wanapoingia mwaka 2019,huku akimwahidi kumpatia ili naye ayafanyie kazi.

Akiendelea kujibu maombi ya Mnyika, Rais Magufuli alisemasuala la demokrasia halina mjadala kwa kuwa ipo ya kutosha na hatakuwa tayari kuvumilia kuona watu wakiandamana na kufanya fujo mitaani na kukwamisha shughuli za maendeleo kwa kisingizio cha demokrasia.

“Tunaona leo tumekusanyika, tumekaa pamoja hapa, hata yeye (Mnyika) tumempa nafasi ya kuzungumza na wengine wamezungumza, sasa sijui anataka demokrasia ya aina gani? Demokrasia siyo kufanya fujo,” alisema.

Alisema ingawa kodi za wananchi ndizo zinazotumika kufanya miradi ya maendeleo nchini, ni vyema Mnyika akaonyesha hata shukrani kwa kumpongeza akiwa hai kwa kuwa naye ataona amefanya jambo.

“Ni sawa, hizi ni kodi zenu ndiyo zinazotumika, lakini kwani miaka mingine yote mlikuwa hamlipi kodi? Mbona hata hii barabara haikujengwa? Kwa hiyo mtambue kuwa ni juhudi zangu binafsi pia kuelekeza nguvukatika ujenzi wa barabara hii.

“Mara nyingi hizi fedha zinazotumika kujenga hizi barabara zilikuwa zinapangwa lakini hazitumiki, sasa msiniulize zilikuwa zinakwendawapi, hilo siyo jukumu langu,”alisema Rais Magufuli.

Alisema Serikali yake inaonyesha uungwana mkubwa sana. “Hatakatika maeneo ambayo watu wanakukataa unawapelekea miradi mikubwa ya maendeleo lakini bado wanashindwa kushukuru kwa sababu najua maendeleo hayana chama,”alisema.

Rais Magufuli alisema katika Mkoa wa Dar es Salaam pekeyake, amewekeza zaidi ya Sh bilioni 660 katika miradi ya ujenzi, kiwango ambacho hakijawahi kutokea, ndiyo maana kwa sasa wakandarasi wanaonekana wakifanya kazi karibu maeneo yote ya Jiji.

Aliwataka pia wakandarasi wa ndani waliopewa kazi za ujenzi, ikiwamo kampuni ya Esteem Construction iliyopewa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo, ambayo pia ndiyo iliyojenga barabara ya Bagamoyo-Msata, wahakikishe wanamaliza kazi ndani ya muda uliowekwa na kwa viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema barabara hiyo ya Morogoro itakayoitwa Tanzania One, ina hifadhi ya kutosha na kwa sasa inapitisha magari 50, 000 kwa siku hivyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Alisema Serikali itasimamia sheria ili kuhakikisha barabarahiyo inadumu kwa kuzingatia matumizi yake ikiwemo uzito wa magari yanayo pitakatika barabara hiyo.

“Kuanzia Januari Mosi mwakani, tunaanza kusimamia udhibitiwa uzito wa magari, sisi watanzania tumeruhusu uzito wa magari  tani 56 kutumia barabara zetu, Afrika Kusini wanabeba tani 51, katika Afrika yote Tanzania ndiyo tunabeba tani nyingi, hivyo tutasimamia sheria katika kutunza barabara zetu,”alisema Kamwelwe.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara hiyo itajengwa kwa muda miezi 30 kuanzia Julai mwaka huu.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2, itagharimu Sh bilioni 141.5

Alisema usanifu wa awali wa ujenzi huo, ulifanywa na Tanroads wenyewe ambapo gharama za Sh milioni 182 zilitumika.

Mhandisi Mfugale alisema mkandarasi anayesimamia ujenzi huo ni wa ndani kutoka kampuni ya Esteem Construction na tayari ameshalipwa malipo ya awali Sh bilioni 21.1 huku mhandisi mshauri ambaye ni kutoka Tanroad naye amekwishalipwa Sh milioni 86.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisema kuwa miradi yote inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inapitia bungeni na wabunge kutoka vyama vyote vya siasa wanapata nafasi ya kushiriki na kuchambua kwa karibu miradi hiyo ya Serikali.

“Nawaomba Watanzania waiamini Serikali ya Awamu ya Tano kwani imeendelea kufanya maajabu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali mfano huu wa barabaraya njia nane, pia tulipe kodi ili tutekeleze miradi ya maendeleo ya umeme, afyana maji,”alisema Kakoso.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kazi ya Bunge si kupinga Serikali, hivyo hawana budi kuunga mkono bajeti za maendeleo.

Upana wa barabara

Rais Magufuli alisema sheria ya barabara ilizungungumza wazi kwamba barabara kutoka posta kwenye Mnara wa Askari hadi Ubungo,upana  wake ni mita 22.5 kila upande hivyo kufanya upana wa mita 43.

Alisema kutoka Ubungo hadi Kima Stop over upana wake ni mita 90 kila upande, yaani unasimama katikati unahesabu mita 90 upande mmoja na mita 90 upande mwingine, hivyo kuifanya barabara kuwa na mita 180

Alieleza kuwa kutoka Kimara Stop Over hadi Tanita Kibaha upana wa barabara ni mita 121 kila upande inayofanya barabara kuwa na upama wa mita  242 au futi 800.

Alisema kutoka eneo la Tanita Kibaha hadi, Mlandizi upanawa barabara unapungua na kurudi kuwa mita 22.5 na kutoka hapo hadi eneo la Mto Ruvu unaongezeka kufikia mita 90 tena kwa upande mmoja.

“Baadaye, mwaka 2007 sheria hiyo ilifanyiwa mabadiliko ambayo yaliongeza upana katika maeneo yote yaliyokuwa na upana wa mita 22.5 kwa upande mmoja kufikia mita 30 kwa Tanzania nzima na yale mengine yaliyo kuwa naupana wa mita 90 na mita 121 kubaki kama yalivyo,” alisema.

Mchezo mchafu stendi mpya

Aidha Rais Magufuli alisema anafahamu mwenendo wa mameya wa Dar es Salaam na madiwani namna walivyokuwa wakipinga ujenzi wa stendi mpya ya Mbezi.

“Mwita (Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita) nafahamu mlivyokuwa mnafanya vikao kupinga ujenzi wa ile stendi mpya, mkamfuata mkandarasi akakataa eti mkajipiga picha ili aonekane anawahonga.

“Nafahamu mienendo yetu yote…nimefuatilia kila kitu na Kubenea alikuwepo na Sitta (Meya wa Kinondoni, Benjamin) nao walikuwepo sasa acheni mchezohuo msirudie,”alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo alimpongoza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, kwa namna alivyosimama katika kusimamia sheria kwenye suala hilo la ujenzi wa stendi.

CCM chadema waonyeshana ubabe

Katika hali ambayo si ya kawaida, jana katika uzinduzi huo wa barabara hiyo, wanachama wa CCM na Chadema ambao walivalia sare za vyama vyao walijitokeza kwa wingi kushiriki katika hafla hiyo.

Wanachama wa vyama hivyo walikaa sehemu moja huku wakiimbana kucheza huku wale wa CCM wakinyanyua vidole gumba juu na Chadema wakinyanyua vidole viwili juu ikiwa ni ishara ya alama ya vyama vyao.

Wakati wale wa CCM walikuwa wakiimba nyimbo za chama chao, wa Chadema walikuwa wakinyoosha mikono juu na kuonyesha vidole viwili huku wakiwa na baadhi ya wanachama wa CUF.

Mbali na wanachama hao, pia wabunge wa upinzani kutoka Mkoawa Dar es Salaam ambao mara nyingi wamekuwa hawashiriki kwenye matukio ya Rais Magufuli lakini jana  walihudhuria.

Wabunge wa upinzani waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na John Mnyika (Kibamba) na Saed Kubenea wote kutoka Chadema.

Meya wa Ubungo, Bonifance Jacob na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita wote kutoka Chadema pia walihudhuria.

Wengine walihuodhuria ni waliokuwa wenyeviti wa CCM mikoa na wilaya ambao juzi, Halmashauri Kuu ya chama hicho ilitangaza kuwasamehe nakuwarejesha uanachama wakiwemo Ramadhani Madabida (aliyekuwa Mwenyekiti wa CCMMkoa wa Dar es Salaam) na Salum Madenge (aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya yaKinondoni).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles