31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Msukumo wa Rais Samia Sekta ya Madini, Wachangia Trilioni 1. 19 Madini ya Viwandani

*Waziri Biteko ataka wenye Viwanda kununua Madini kwa bei Elekezi, watakiwa kuwasikiliza wadau

*Awasisitiza Wachimbaji Wadogo kuzalisha madini yenye ubora kuepusha hasara

*Azindua Kalenda ya Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo, ashuhudia utiaji saini makubaliano kati ya STAMICO, taasisi za fedha na wauzaji wa vifaa vya uchimbaji

*STAMICO kuwafikia wachimbaji wa Chumvi, Vito

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Imeelezwa kuwa msukumo uliowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Samia Suluhu katika Sekta ya Madini umewezesha kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ndogo ya madini ya Viwandani ambapo katika kipindi cha miaka miwili madarakani, mchango wa madini hayo umefikia Sh trilioni 1 na bilioni 19 kutoka milioni 451.6.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko wakati akifungua mkutano wa Siku mbili wa Wachimbaji wadogo na wadau wa Madini ya Viwandani ulioandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Chama cha Wachimbaji Wadogo Mikoa ya Dar es Salaama na Pwani na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Akizungumza katika ufunguzi, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wananunua madini hayo kutokana na bei elekezi iliyowekwa na Serikali huku akiwataka wachimbaji wadogo wa madini hayo kuzalisha madini yenye ubora ili kuepusha hasara kwa wenye viwanda.

Katika hatua nyingine, ameitaka makubaliano yaliyowekwa kati ya STAMICO, taasisi za fedha na wauzaji wa vifaa za uchimbaji madini kutoa matokeo chanya kwa kuwa wajibu wa kuwalea wachimbaji wadogo si hisani bali takwa la kisheria.

Akizungumzia mchango wa wachimbaji wadogo, kwenye maduhuli ya Serikali amesema yamefikia asilimia 40 kutoka asilimia 4 na na kutaka watu wenye ulemavu na wanawake kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini ili wasibaki nyuma.

Aidha, amepongeza juhudi zilizofanywa na STAMICO kuwafikia wachimbaji mbalimbali na kusema kwamba viwanda vinahitaji maligafi hivyo, mikutano kama hiyo itawezesha ukuzaji wa viwanda nchini kupitia sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Venance Mwasse amesema Shirika hilo litaendelea kuwafikia wachimbaji wadogo wa madini kwa umuhimu wao na kueleza baada ya wadau wa madini ya viwandani, watakaofuatia ni wachimbaji wa madini ya chumvi na vito.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mwasse amesisitiza STAMICO imeanza na mfumo huo wa kuyafikia makundi mbalimbali kwa kuwa inaamini kuwa mfumo huo utaleta mapinduzi kwenye sekta ya uchimbaji mdogo wa madini.

“Tunajiuliza kwanini malighafi itoke nje wakati tunayo madini ya kutosha. Tuko hapa kwa ajili ya kupata suluhu ya changamoto hizi. Tumewaalika wadau wezeshi zikiwemo taasisi za fedha, wasimamizi wa sheria,wenye viwanda, maabara, taasisi za elimu na wengine, lengo ni kupata suluhu ya matatizo yetu,’’ amesema Mwasse.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo akizungumza kwa niaba ya Katibu amesema, mkutano huo ni mkakati wa ukweli wa kutafuta njia ambazo zitasaidia masuala yaliyokwama yaweze kutekelezwa na kazi kufanyika vizuri.

“Sekta yoyote ili iweze kuendelea na kupata matokeo yenye tija ni lazima ishirikishe wadau na makundi yote na sisi kwetu Sekta ya Madini mkutano huu pamoja na makubaliano yaliyoingiwa leo ni mikakati ya kuhakikisha sekta hii ndogo ya madini ya viwandani inaendelea,’’ amesisitiza Mbibo.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula amesema msukumo ambao umewekwa na STAMICO kuwafikia wachimbaji wa madini mbalimbali ni eneo linalokwenda kufungua ajira zinazotokana na madini hayo na kuongeza kwamba, kama taifa ni matarajio kuwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa utafikia zaidi ya asilimia 10 kabla ya kufika mwaka 2025.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), John Bina ametumia fursa hiyo kuzipongeza baadhi ya benki nchini ambazo hivi sasa zimeweza kuielewa Sekta ya Madini ambapo hadi sasa benki ya CRDB imeweza kutoa mkopo wa Sh bilioni 200 kwa wachimbaji wadogo.

Pia, ameishauri Serikali kutumia amani iliyopo nchini kuvutia uwekezaji ili kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda kupitia Sekta ya madini pamoja na kuiomba serikali kuziangalia changamoto inazowakabili wachimbaji wadogo ikiwemo masoko, mitaji, tozo mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji nchini kufanya shughuli zao kwa tija na kuendelea kuchangia zaidi katika uchumi na maendeleo ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles