RAMADHAN HASSAN Na ASHA BANI – DODOMA/ DAR
HALI ya mshikemshike ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, inazidi kupamba moto baada ya wanachama wake watatu sasa kutangaza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa siku ya jana waliotangaza kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Irnga Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu huku Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu naye alitangaza kuwania nafasi hiyo bado akiwa ughaibuni
Hatua hiyo sasa inafanya idadi waliotangaza nia kufikia wagombea watatu ndani ya chama hicho.
Akizungumza kuhusu vipaumbele vyake Mchungaji Msigwa, alisema kuwa iwapo chama chake kitampa ridhaa atafanya mageuzi makubwa katika elimu na teknolojia, utawala bora na uwajibikaji pamoja na kuwapo kwa mageuzi makubwa ya uchumi.
Akizungumza jana na waandishi wa habari ambapo alikuwa ameongozana na Mbunge wa Mbeya Mjini,J oseph Mbilinyi,Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema na wabunge wa viti maalumu Rhoda Kunchela na Susan Lyimo.
Msigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho alisema, amejipima na kuona kwamba ana uwezo wa kuongoza Nchi iwapo chama chake kitampa nafasi hiyo.
“Vipaumbel vyangu vikuu ni vitatu kwanza ni mageuzi makubwa katika elimu na teknolojia hatuwezi kufanikiwa katika jambo lolote kuzidi kiwango cha fikra ulichonacho, kama tunafikra ndogo tutapata mafanikio madogo.
“Uelewa wetu kuhusu kila jambo unategemea na fikra tulizonazo, mazingira yanaweza kuwa yale yale lakini namna ya kuhama ndio inakuwa ni shida,” alisema
Alisema kipaumbe chake cha pili ni utawala bora na uwajibikaji ambapo alisema kukosekana kwa mambo hayo kumesababisha Tanzania kutokufikia malengo yake.
“Serikali yangu itarejesha uhuru wa kutoa maoni ya demokrasia ya vyama vya siasa na asasi za kiraia na matumizi ya fedha za umma,”alisema Msigwa.
NYALANDU
Naye aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne, Lazaro Nyalandu ametangaza rasmi azma yake ya kugombea urais huku akiweka bayana vipaumbele vyake 23 atakavyoanza kuvifanyia kazi ndani ya siku 100.
Hayo aliyasema jana alipokuwa akitangaza nia yake ya kuwania nafasi hiyo na kueleza kwamba tayari ameshamwandikia baria Katibu Mkuu wa chama hicho kuhusu kusudio langu la kutia nia katika kinyang’anyiro cha kuwa mgombea urais kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2020, “.
“Nasimama mbele yenu na mbele ya umma wa Watanzania, huku moyo wangu ukiwa umejaa shauku kubwa nikitamani kuiona Tanzania, nchi tuipendayo kwa moyo wote inapata ustawi na kuendeleza matamanio, matarajio na ndoto za watu wake katika kuwapatia maendeleo endevu,” alisema Nyalandu.
Alisema mopja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha serikali yake inarekebisha sheria ya ardhi kuruhusu wananchi kumiliki ardhi bila ukomo na kuwapimia wananchi maeneo ya ardhi kote nchini ili kurasimisha utajiri wa Watanzania wote kupitia ardhi wanayomiliki.