30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

MSHUMAA WATEKETEZA WANNE WA FAMILIA MOJA

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole
Na ANNA RUHASHA - SENGEREMA  |  

MOTO wa mshumaa umeteketeza watoto wanne wa familia moja katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, baada ya kuchoma chumba walichokuwa wamelala.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, amethibitisha tukio hilo lililotokea saa tano usiku wa Februari 28, mwaka huu.

Aliwataja waliopeza maisha katika tukio hilo ni Lidya Elias  (12), mwanafunzi wa darasa sita, Modesta Elias (8),   Steven Deo (10) mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Pambaru na Catherine Elias (6)   mwanafunzi wa darasa pili katika Shule ya Msingi Muslim.

“Chanzo cha moto huo ni mshumaa uliowashwa ndani ya chumba na kuendelea kuwaka wakati watoto hao wakiwa wamelala, ghafla moto ulishika kwenye godoro na kuanza kuenea sehemu nyingine za chumba hicho.

“Ni pigo kwa jamii ya Sengerema na taifa kwa ujumla kupoteza watoto wanne kwa mpukupuo, hili  limetusikitisha sana, niseme ajali ikitokea inaacha fundisho kwa jamii, lazima tujifunze watoto kukaa bila uangalizi kwenye vyumba na kuwasha mishumaa usiku kucha si jambo salama,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, dada wa marehemu hao   ambaye alikuwa amelala ndani ya chumba hicho, Thabiza Elias (17), alisema wakati anashtuka kutoka usingizini, alikuta moto umesambaa katika vitanda vya watoto hao.

“Wakati nimelala nilistuka nikakuta moto mkali unawaka, ndipo nilianza kupiga kelele na kumwamsha mama chumba cha pili, lakini wadogo zangu walikuwa wameishajeruhiwa sana.

“Wakati tunalala tuliwasha  mshumaa, nahisi ndio huo ulisabibisha moto,” alisema Thabiza.

Lucas Bahati, ambaye ni jirani, alisema walijitahidi kuwaokoa watoto hao kwa kuwakimbiza hospitalini, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda baada ya kupoteza maisha wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mission Sengerema.

Tukio hili ni moja ya matukio makubwa ya moto yaliyotokea mwaka huu na kuteketeza watu wa familia moja.

Februari 2015, watu sita wa familia moja akiwamo Kapteni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), walikufa baada ya kuteketezwa kwa moto jijini Dar es Salaam.

Moto huo ulitokea Kipunguni A, Ukonga Banana, wilayani Ilala.

Februari ya mwaka huo pia, watu tisa wa familia moja walifariki dunia baada ya kuteketea kwa moto Buguruni, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles