Ramadhan Hassan,Dodoma
BOHARI Kuu ya Dawa (MSD) imetaja vipaumbele tisa kwa mwaka wa fedha 2022-2023 ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa dawa hadi kufikia asilimia 90 ya mahitaji kwa kuingia mkataba wa muda mrefu na wazalishaji wa bidhaa za afya.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 17, jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji MSD, Mavere Tukai wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2022-2023.
Mtendaji huyo ametaja kipaumbele kingine ni kufanya mabadiliko ya kimuundo na kimfumo ambapo yapo katika hatua za mwisho za kuhakikisha inapata menejimenti mpya.
Aidha, inaendelea na mabadiliko ya ndani ya Taasisi yanayolenga kuimarisha utendaji na upatikanaji wa bidhaa za afya.
Amekitaja kipaumbele kingine ni kuongeza kasi ya ununuzi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.
Amesema wanaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao kuhakikisha taratibu zote za ndani zinawekwa kwenye mfumo ili kuongeza ufanisi katika eneo la manunuzi.
“MSD inafanya mapitio ya maboresho ya mfumo mzima wa mnyororo wa ugavi kwa kuhusisha wadau mbalimbali kwani lengo la kuhakikisha uendeshaji wa taasisi unaendana na mahitaji ya vituo vya afya na wadau wengine.
“Tutaendelea na utekelezaji wa mchakato wa kumpata mbia wa ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya vya ndani kwa kutumia PPP.
“Tutaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu yetu na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kufanya ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Kagera na Ruvuma.
“Kuongeza ushirikiano na wadau wetu wakuu wakiwemo wafadhili, washitiri, wateja pamoja na sekta nyingine ambazo tunafanya nao kazi,”amesema Mkurugenzi huyo.
Amesema wanashirikiana na sekta zingine kuhakikisha wananyanyua wazalishaji wa ndani ya nchi hasa kwenye kuwakaribisha wawekezaji wenye nia ya dhati ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za afya.
Aidha amesema MSD ina majukumu manne ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za afya na vituo binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali ilitoa Sh bilioni 134.9 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya.
“MSD inaendelea na zoezi la usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vyote vya afya vya Serikali 7,153 kupitia kanda zake 10 zilizowekwa kimkakati.MSD ina maduka ya jamii sita yaliyopo katika mikoa ya Katavi, Arusha, Lindi, Mbeya, Geita na Dar es Salaam ili kusaidia kusogeza huduma kwa wananchi,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali ina Sera inayotaka kuwepo kwa dawa, vifaa na vifaa tiba vitendanishi vya kutosha, vyenye ubora, na Watanzania wavipate kwa bei wanayoweza kumudu.
“Mpaka sasa, kwenye hospitali zetu za Mikoa, Kanda, Rufaa na kitaifa upatikanaji wa dawa uko asilimia 80 kwa sababu wanapata dawa kutoka MSD na zingine wanazipata kutoka kwenye maeneo mengine,”amesema.